Saturday, March 29, 2014

JESHI LA POLISI MKOANI RUVUMA LAWATAKA ASKARI WAKE KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Akili Mpwapwa upande wa kulia akizungumza na wadau mbalimbali (hawapo pichani) katikla ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, juu ya dhana ya ulinzi shirikishi na kuwataka askari wake na wananchi kushirikiana kwa pamoja ili kuepukana na vitendo vya uhalifu ambavyo vinahatarisha usalama wa raia na mali zao.

Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Godfrey Ng'humbi, akisisitiza jambo juu ya kuitaka jamii na Wadau mbalimbali wilayani Mbinga kushirikiana kwa pamoja katika kuendeleza masuala ya ulinzi shirikishi. (Picha zote na gwiji la matukio Ruvuma)









Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limesema Serikali kamwe haitavumilia kuona askari wake wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu, badala yake itahakikisha kwamba inachukua hatua mara moja kwa yule anayekiuka maadili ya utumishi wa umma ili kuwafanya wananchi na mali zao wanaishi katika hali ya usalama. 

Kauli hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Akili Mpwapwa alipokuwa katika ziara yake ya kikazi akizungumza na askari polisi na wadau mbalimbali wa mkoa wa Ruvuma, kwa lengo la kusisitiza juu ya uimarishaji wa ulinzi shirikishi.

Mpwapwa alisema lengo la ziara hiyo ni kutaka kutambua maeneo yake ya kazi, kubaini uhalifu, vikundi vya ulinzi shirikishi na wadau ambao wamekuwa wakichangia jeshi la polisi katika kuleta ufanisi wa masuala ya ulinzi katika maeneo yao. 

Friday, March 28, 2014

RAIS JAKAYA KIKWETE KUFUNGUA STENDI YA KISASA MBINGA


Mkuu wa mkoa wa Ruvuma(katikati) Said Mwambungu akizungumza na viongozi waliokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga, wakati wakiwa katika eneo la stendi mpya ya abiria ambayo imejengwa mjini hapa.(Picha na Kassian Nyandindi)











Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete anatarajia kufanya ufunguzi wa kituo kikuu cha stendi mpya ya magari ya abiria ambacho kimejengwa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.

Ufunguzi huo utafanyika mwezi Mei mwaka huu wakati atakapokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alieleza hilo wakati alipokuwa akizungumza na uongozi wa wilaya ya Mbinga, katika ziara yake ya kikazi iliyofanyika hivi karibuni wilayani humo.

Mwambungu aliupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa ujenzi wa stendi hiyo iliyopo mjini humo, ambayo ni kitega uchumi kizuri cha kuiingizia mapato halmashauri ya wilaya hiyo.

Wednesday, March 26, 2014

MENEJA TANROAD RUVUMA AKALIA KUTI KAVU ANYOSHEWA KIDOLE MBELE YA BOSI WAKE

Msafara wa magari ziara ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma, ukiwa umekwama katika kijiji cha Mahenge wilayani Mbinga mkoani humo, wakati ukielekea leo katika kata ya Litembo.

Jitihada zikiendelea kunasua gari moja baada ya jingine katika msafara wa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu baada ya kukwama kwa muda wa saa moja, leo katika kijiji cha Mahenge ukielekea kata ya Litembo wilayani Mbinga. (Picha zote na gwiji la matukio Ruvuma)

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

DIWANI wa kata ya Litembo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Altho Hyera amemtuhumu Meneja wa wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani humo, Abraham Kissimbo kwamba amekuwa kiongozi mwenye kauli zisizoridhisha ambazo hazionyeshi uadilifu kama mtumishi wa umma.

Hyera alisema hali hiyo ilimkuta wakati alipokwenda ofisini kwake kupata ufafanuzi juu ya maendeleo ya ujenzi wa barabara yenye kilometa 26 kutoka Mbinga mjini kwenda Litembo, ambayo hivi sasa ina hali mbaya kutokana na magari kushindwa kupita katika kipindi hiki cha masika.

Diwani huyo alimnyoshea kidole Injinia Kissimbo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi uliofanyika katika kata hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa leo alikuwa katika ziara yake ya kikazi kutembelea kata ya Litembo kwa lengo la kujionea kero hiyo ya barabara ambayo malalamiko yake yamedumu kwa miaka mingi.

MWAMBUNGU AUTAKA UONGOZI WA WILAYA KUCHUKUA HATUA ZA HARAKA KUNUSURU CHANZO CHA MAJI KIGONSERA

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga (Aliyesimama) akisoma taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ambaye amekaa upande wa kushoto, amevaa suti nyeusi. (Picha na Kassian Nyandindi)



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ameutaka uongozi wa wilaya ya Mbinga mkoani humo, kuchukua hatua mapema ya kunusuru hali ya chanzo cha maji kilichopo kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera, ambacho kimevamiwa na watu wachache ambao huendesha shughuli za kilimo.

Aidha watu hao wameweka makazi karibu na chanzo hicho kwa kujenga nyumba za kuishi jambo ambalo linahatarisha kupotea kwa uoto wa asili katika chanzo.

Mwambungu alitoa agizo hilo alipokuwa wilayani humo katika ziara yake ya kikazi, mara baada ya kusomewa taarifa ya maendeleo ya wilaya ambayo ilisomwa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga.

“Hili jambo tusilifumbie macho, tuchukue hatua sasa kwa kuhakikisha wale watu wanahamishwa haraka ili kuweza kunusuru usalama wa chanzo kile”, alisema.

Monday, March 24, 2014

MWAMBUNGU ALIA NA UJENZI WA BARABARA WILAYANI NYASA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu.



















Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.


MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, leo ameanza ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali wilayani Nyasa na ifikapo Marchi 25 mwaka huu, ataendelea wilayani Mbinga.

Huo ni mwendelezo wa ziara zake za kikazi hapa mkoani Ruvuma.

Akiwa katika wilaya hizo Mwambungu atapokea taarifa za  maendeleo ya wilaya hizo, kuongea na wananchi na kukagua miradi mbalimbali kama vile barabara, mashamba ya kilimo cha mahindi, skimu za kilimo cha mpunga na zahanati.

Taarifa zilizotufikia hivi punde kutoka wilayani Nyasa, zinaeleza kuwa Mkuu huyo wa mkoa amelalamikia ujenzi wa barabara za wilaya hiyo kwa kiwango cha chini jambo ambalo linadhihirisha kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Pia amezitaka mamlaka husika hususan watendaji wa wilaya hiyo kufanya kazi kwa weledi na kufuata misingi ya utawala bora kama sheria za nchi zinavyotaka.

KIGONSERA AFYA ZAO ZIPO HATARINI, WANANCHI WATISHIA KULALA BARABARANI KUZUIA MSAFARA WA RAIS


Hivi ndivyo ilivyo katika chanzo cha maji Kigonsera ambako maji yametegwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, hali ni mbaya hatua husika zinapaswa kuchukuliwa mapema.(Picha na Gwiji la matukio Ruvuma)










Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

AFYA za wakazi wa kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, zipo mashakani kutokana na maji wanayotumia kwa ajili ya kuendeshea maisha yao ya kila siku kuwa machafu na kutofaa kwa matumizi ya binadamu.

Hali hiyo imesababisha wakazi hao kutoa tamko na kutishia kwamba siku ya ujio wa Rais Jakaya Kikwete, katika ziara ambayo anatarajia kuifanya hivi karibuni katika kipindi cha mwezi Mei mwaka huu mkoani humo hususani katika wilaya ya Mbinga, wapo tayari kulala barabarani kwa lengo la kushinikiza msafara huo usimame ili waweze kutoa kilio chao kwa kiongozi huyo wa kitaifa na kiweze kufanyiwa kazi haraka.

Walisema kufanya hivyo kunatokana na uongozi wa wilaya hiyo kuwa na kasi ndogo, ya uchukuaji wa hatua za kuwahamisha watu waharibifu katika eneo ambako chanzo cha maji kimejengwa na kugharimu mradi mzima wa maji uliosambazwa kijijini hapo kufikia shilingi milioni 479 kwa ufadhili wa benki ya dunia.

Tuesday, March 11, 2014

TANROADS RUVUMA YAENDELEA KUNYOSHEWA KIDOLE

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


SERIKALI mkoani Ruvuma imeombwa kuchukua hatua za haraka juu ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mbinga mjini, kwenda hospitali ya Litembo iliyopo wilayani humo, kutokana na barabara hiyo kuwa katika hali mbaya.

Rai hiyo ilitolewa na Wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani humo walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, ambapo walieleza kuwa kutokana na barabara hiyo kuwa na mashimo mengi ambayo ni makubwa, magari ya abiria na yale yanayobeba wagonjwa yamekuwa yakikwama na kuleta adha kubwa kwao.

Walisema wamechoshwa na ahadi hewa ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na viongozi wa serikali wa mkoa huo, kwamba wataifanyia matengenezo na hakuna matokeo mazuri yanayoonekana kuzaa matunda juu ya kumaliza tatizo hilo ambalo limedumu kwa miaka mingi.

"Tunachohitaji hapa waifanyie matengenezo tumechoka na kauli zao ambazo hazina utekelezaji sisi ni wananchi kama walivyo wenzetu katika maeneo mengine ambayo serikali inawapelekea huduma za msingi",
walisema.

Monday, March 10, 2014

WANAWAKE MKOANI RUVUMA WALALAMIKIA UKATILI UNAOSABABISHWA NA HISIA ZA KIMAPENZI

Kutoka kulia ni Diwani wa viti maalum tarafa ya Mbinga mjini, Grace Millinga akifurahia jambo pamoja na Wanawake wenzake kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani, ambazo mkoani Ruvuma zilifanyika katika kijiji cha Kihereketi wilayani Mbinga.


Akina mama wa mkoa wa Ruvuma, wakiendelea kwa pamoja kufurahia maadhimisho ya sherehe za siku ya mwanamke Duniani.

Joseph Mkirikiti Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, akipokea maelezo mafupi kutoka kwa mjasiriamali ambaye anatengeneza kinywaji cha asili aina ya "Wine". {Picha zote na Gwiji la matukio Ruvuma}


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

WANAWAKE mkoani Ruvuma wamelalamikia na kupinga vikali vitendo vinavyoendelea kushamiri, ambavyo hufanyiwa miongoni mwao mkoani humo ikiwemo ukatili, kupigwa na kuuawa kutokana na hisia za kimapenzi.

Aidha wamesema kuwa upande wa watoto wa kike kumekuwa na ukosefu wa usawa katika kupata elimu, hivyo kusababisha watoto wengi kuishi katika mazingira hatarishi.

Kilio hicho kilitolewa na Wanawake hao kupitia risala yao iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti, katika sherehe za maadhimisho ya kilele cha siku ya wanawake duniani kilichofanyika katika mkoa huo kijiji cha Kihereketi kata ya Nyoni wilayani Mbinga.

Akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya wanawake wenzake, Cosma Mbawala ambaye ni mkazi wa kijiji hicho alisema wanawake ni kichocheo kikubwa katika harakati za kuleta maendeleo lakini inasikitisha kuona wamekuwa wakinyanyaswa na kunyimwa haki zao za msingi.

Friday, March 7, 2014

WANAFUNZI WAJISAIDIA PORINI KUTOKANA NA SHULE KUKOSA VYOO



Na Kassian Nyandindi,

Nyasa.

SHULE ya msingi Ndingine iliyopo katika kata ya Ngumbo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa vyoo kwa muda mrefu sasa jambo ambalo lina hatarisha usalama wa afya kwa walimu na watoto wanaosoma shuleni hapo.

Mwandishi wa habari hizi amebaini na kushuhudia pia wanafunzi wakijisaidia pori lililopo jirani na shule hiyo, huku walimu wao nao wakiomba msaada katika vyoo vya wakazi wanaoishi jirani na shule hiyo.

Huenda hatua zisipochukuliwa mapema hususani katika kipindi hiki cha masika magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu na homa zingine za matumbo, zinaweza kujitokeza na kuleta madhara makubwa kwa binadamu.

Ndingine ni shule ambayo ina jumla ya wanafunzi 306 wakiwemo wavulana   163 na wasichana 143 ambapo hata mazingira ya shule hiyo sio mazuri hivyo jitihada za makusudi zinahitajika katika kunusuru hali hiyo isiweze kuendelea.

HOSPITALI YAPEWA MSAADA WA VIFAA TIBA



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

HOSPITALI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imepewa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 5,530,000 kwa lengo la kusaidia utoaji wa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa.

Vifaa hivyo vilitolewa na Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo wakati alipokuwa ametembelea hospitalini hapo, kwa lengo la kujionea changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha utoaji wa huduma za matibabu.

Kayombo alikabidhi vifaa vya kitengo cha maabara ambavyo ni Darubini mbili, mashine za kupimia magonjwa ya sukari na moyo ambapo hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa vifaa hivyo.