Saturday, January 31, 2015

WAZIRI MKUU AWASILI MJINI SONGEA KUSHIRIKI SHEREHE ZA KITAIFA KUZALIWA KWA CHAMA CHA MAPINDUZI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwasili katika uwanja wa ndege mjini Songea mkoani Ruvuma, na kulakiwa na Katibu wa Itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye, kushiriki maadhimisho ya miaka 38 ya kuzaliwa CCM yanayofanyika kitaifa leo mkoani humo na mgeni rasmi ni Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete. kulia ni Katibu mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akiwapungia mkono wananchi na wanaccm waliofika kumlaki uwanjani hapo.

Vikundi vya sanaa vikitumbuiza wakati wa mapokezi ya Pinda, Kinana na Philip Mangula.

Thursday, January 29, 2015

MGOMO WA WENYE MADUKA WAZIDI KUSAMBAA NCHINI

                                    Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Na Waandishi wetu, 
 
MGOMO wa Wafanyabiashara wa mduka umesambaa mikoa kadhaa hapa nchini, kupinga matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs).

Mgomo huo ulioanzia kwa wafanyabiashara wa maduka Kariakoo Jijini Dar es Salaam kuanzia juzi, kupinga Mwenyekiti wao Johnson Minja, kukamatwa na polisi, sasa umesambaa hadi miji ya Mwanza, Iringa, Songea na Dodoma.

APANDISHWA KIZIMBANI:

Minja (34) jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma kwa makosa mawili, likiwamo la kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia EFDs na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Rebbeka Mbiru.

Wakili wa Serikali, Godfrey Wambari alidai kuwa Septemba 6 mwaka 2014 katika ukumbi wa Chuo Cha Mipango Dodoma alitenda kosa la kushawishi wafanyabiashara, kutenda kosa la jinai kwamba wasilipe kodi.

Katika shitaka la pili, siku na mahali pa tukio la kwanza mshtakiwa anadaiwa kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za EFD. Upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi la dhamana.

Mshtakiwa alikana mashitaka yake;

Hakimu Mbiru alisema mshtakiwa huyo, atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili akiwemo mtumishi wa serikali mmoja, watakaosaini hati ya dhamana ya shilingi milioni nne.

Wakili wa utetezi, Godfrey Wasonga alidai kuwa mshtakiwa ni mfanyabiashara maarufu nchini na kwamba anaaminika hawezi kutoroka, hivyo mahakama ipunguze masharti ya dhamana.

Hata hivyo, mshtakiwa alitimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa Februari 11, mwaka huu.

BABA KANUMBA: NILIMTEMEA MATE KABROTHER AWEZE KUFANIKIWA KATIKA KAZI ZAKE

Msanii wa filamu nchini, Senga upande wa kulia akiwa na msanii mwenzake katika picha ya pamoja, Gidion Kabrother.
Na Kassian Nyandindi,

Ruvuma.

CHARLES Kanumba ambaye ni baba wa aliyekuwa nguli wa filamu hapa nchini, Marahemu Steven Kanumba amefunguka akisema kuwa alimtemea mate msanii Gidion Simon maarufu kwa jina la Kabrother, ili aweze kufanikiwa katika kazi zake za uigizaji wa filamu kama alivyokuwa mwanae Kanumba.

Alisema aliamua kufanya hivyo, ili ikiwezekana amrithi mwanae huyo ambaye alikuwa ni rafiki yake kipenzi akishirikiana na mwanae, katika kazi za uigizaji wa filamu kwa muda mrefu.

“Nilimtemea mate huyu mtoto, kwa sababu katika kazi zake alikuwa mtu wa karibu sana na mwanangu wakishinda hapa nyumbani, hivyo niliona nifanye hivi niweze kumpatia baraka na Mungu akimbariki aweze kuonyesha maajabu kama mwenzake”, alisema.

Alifafanua kuwa, Kabrother wakati anaanza kazi zake za uigizaji alikuwa akijifunza kupata ujuzi wa fani hiyo, kutoka kwa marehemu Kanumba.

Hayo yalisemwa na Baba Kanumba, wakati alipokuwa akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu ambapo aliongeza pia kwa kuwataka waigizaji wa filamu hapa nchini, kuwa na ushirikiano katika kazi zao ili waweze kusonga mbele katika tasnia yao ya sanaa na maigizo ya aina mbalimbali.

“Namsifu Kabrother kwa juhudi anazozifanya, ameanza kazi hii kwa muda mrefu mpaka hapa alipofikia katika kukuza kipaji chake”, alisema Baba Kanumba.

Sunday, January 25, 2015

AKUTWA AMEJINYONGA KATIKA MAHABUSU YA KITUO KIKUU CHA POLISI MBINGA

Na Kassian Nyandindi,


Mbinga.

MTUHUMIWA ambaye alikuwa akishikiliwa katika Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Bosco Ndunguru (40) amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia shati ambalo alikuwa amelivaa, wakati alipokuwa kwenye mahabusu ya kituo hicho cha polisi wilayani humo.

Ndunguru aliwekwa mahabusu, kwa tuhuma ya kuvunja jengo la polisi na kuiba Radio call ya kituo hicho mwaka jana, ambapo alitoroka kusikojulikana na Jeshi hilo lilikuwa likimtafuta kwa muda mrefu.

Taarifa zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea Januari 23 mwaka huu majira ya asubuhi, ambapo baada ya kukamatwa na kuswekwa rumande ilikuwa afikishwe Mahakamani kwa ajili ya kujibu tuhuma, ambazo zilikuwa zinamkabili.

Imedaiwa kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kuingizwa mahabusu, muda mwingi alikuwa akilia na kulalamika sana, huku akidai kuwa ndugu zake hawampendi.

Saturday, January 24, 2015

IKULU YAFANYA MABADILIKO YA MAWAZIRI

Wa kwanza kuapa alikuwa, Samwel Sitta.
Na Waandishi wetu,


Dar.

HATIMAYE Rais Kikwete Ikulu Jijini Dar es Salaam, amefanya mabadiliko madogo ya mawaziri na mawaziri hao wameapishwa, kabla ya Rais huyo kuondoka kwenda Davos Uswisi.

Mawaziri Kamili:

George Simbachawene- Waziri wa Nishati na Madini
Mary Nagu -Waziri wa nchi Mahusiano na Uratibu
Harrison Mwakyembe - Waziri wa Afrika Mashariki.
Wiliam Lukuvi - Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi
Steven Wassira - Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika
Samwel Sitta - Waziri wa Uchukuzi
Jenista Mhagama - Waziri wa Sera na Uratibu wa Bunge
Christopher Chiza- Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji


Manaibu Waziri:
 
Steven Masele - Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano
Angellah Kairuki - Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi
Ummy Mwalimu- Naibu Waziri wa Katiba na Sheria
Anna Kilango- Naibu waziri wa Elimu
Charles Mwijage - Naibu Waziri wa Nishati na Madini

Walioapishwa leo hii:

-Wa kwanza kuapa ni Samweli sitta
-Wapili kuapa ni Mary Nagu
-Watatu kuapa ni Steve Wassira
-Wanne Kuapa ni William Lukuvi
-Watano kuapa ni Christopher Chiza
-Wasita Kuapa ni Harrison Mwakyembe
-Wasaba kuapa ni George Simbachawene
-Wanane kuapa ni Jenista Muhagama
-Watisa kuapa ni Ummy Ally Mwalimu
-Wakumi kuapa ni Steven Masele
-Wakumi na moja kuapa ni Angellah Kairuki
-Wakumi na Mbili kuapa ni Anne Kilango Malecela
-Wakumi na tatu kuapa ni Charles John Mwijage

VIONGOZI WACHAGULIWE KWA RIDHAA YA WANANCHI

Padre Baptiste Mapunda.

Na Padre Baptiste Mapunda,

SERIKALI iliyopo madarakani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado tumeshuhudia vituko vya hapa na pale, katika ulingo huu wa kisiasa huku ikijigamba ndiyo inayoendesha mambo yake kwa kutumia demokrasia, na utawala bora.

La hasha, mfano mzuri ni ule katika kipindi cha kampeni, upigajikura na utangazaji matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umefanyika hivi karibuni Desemba 14 mwaka jana, CCM kilionekana kufanya rafu kwa wapinzani wao wa kisiasa, ili kujihakikishia kinapata ushindi. 

Chama hiki tawala kilionekana kutumia mbinu nyingi, kama vile kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani katika maeneo mbalimbali hapa nchini, kwa namna moja au nyingine ikiwemo hata wakati mwingine, kutumia vyombo vya dola kama polisi ikiwa ni mbinu tu ya kutafuta ushindi.

Aidha baadhi ya matokeo katika vituo vya kupigia malalamiko yalijitokeza kwamba yalibatilishwa, na sio hilo tu bali hata pale yalipokuwa wazi kwamba wapinzani wameshinda  bado CCM haikukubali bali ulikuwa ni mwendo tu wa kulazimisha ushindi, kitu ambacho siasa za namna hii zinaweza kuiingiza jamii katika vurugu au machafuko kama yaliyotokea kule Kenya na sehemu nyinginezo.

Tuesday, January 20, 2015

DIAMOND PLATINUM KUTUMBUIZA SHEREHE ZA CCM KITAIFA MKOANI RUVUMA

Nassib Abdul, maarufu Diamond Platinum

Na Mwandishi wetu,
Songea.

MKOA wa Ruvuma, umepata heshima kubwa ya kuandaa sherehe za kutimiza miaka 38 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaifa mwaka huu.

Mbunge wa Songea Mjini Dokta Emmanuel Nchimbi ameanza kuratibu sherehe hizo ambazo zitafanyika mkoani humo, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya Kikwete. 

Dokta Nchimbi alisema hayo alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari mjini hapa, ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni; Umoja ni Ushindi, Katiba yetu nchi yetu.

Mbunge huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi, alisema kila kitu kimekamilika juu ya maandalizi ya sherehe hizo ambazo zitafanyika Februari Mosi mwaka huu, badala ya Februari tano kama ilivyozoeleka. 

Monday, January 19, 2015

MBUNGE GAUDENCE KAYOMBO AENDELEA KUKALIA KUTI KAVU MBINGA



Gaudence Kayombo.
Na Mwandishi wetu,

Ruvuma.

WAFANYABIASHARA wa wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametishia kutomchagua tena Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Gaudence Kayombo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, kwa kile walichodai kwamba ameshindwa kuwatetea Bungeni na badala yake ameunga mkono ongezeko la kodi la asilimia 100. 

Aidha walisema Mbunge huyo mara kwa mara wanapomtaka azungumze na wafanyabiashara hao kupitia vikao mbalimbali, kwa lengo la kusikiliza kero zao amekuwa hajitokezi huku wakidai amekuwa akitoa sababu nyingi kwamba amebanwa na majukumu.

Hayo yalijiri walipokuwa wakizungumza kwenye kikao cha wafanyabiashara hao kilichoketi kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (FDC) mjini hapa, na baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka makao makuu ya mamlaka hiyo na mkoa huo, mmoja wa wafanyabiashara hao, Benedict Luena alisema wameumizwa na Mbunge wao kushindwa kuwatetea kuhusu suala hilo. 

KATIBU WA MADIWANI NA BAADHI YA VIGOGO MBINGA, WADAIWA KUSUKA MPANGO MCHAFU WA KUVUNJA KAMATI YA MIPANGO NA FEDHA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

ULE mpango wa kutaka kuvunjwa kwa Kamati ya mipango na fedha katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, mapya yameendelea kuibuka ambapo imeelezwa kwamba, ni mpango ambao umesukwa na vigogo wachache wa wilaya hiyo huku Madiwani wake wakiendelea kulalamika kutoshirikishwa juu ya suala hilo. Mtandao huu unaripoti.

Taarifa za uhakika zilizotufikia leo zinaarifu kuwa, mkakati huo wa kuvunja kamati hiyo huenda ukagonga mwamba kufuatia baadhi ya Madiwani kuja juu na kueleza kwamba Katibu wao wa baraza la madiwani, Adolph Mandele ambaye naye ni diwani wa kata ya Mpapa, ndiye anayewachanganya na kuwauza wenzake, akidaiwa kutumiwa na vigogo hao (majina tunayo) kusuka mipango mibaya kwa lengo la kuhakikisha vigogo hao wanafanikisha jambo hilo.

Mandele analalamikiwa kutengeneza muhtasari hewa ambao unaonyesha kwamba wajumbe wa baraza hilo kwa maana ya madiwani wenzake, walikutana pamoja na kuketi kupitia kikao cha dharula (CCM) na kukubaliana kufanya hivyo jambo ambalo, madiwani wenzake wanamshangaa na kuanza kumjia juu wakisema sio kweli anadanganya.

Wengi wanapinga vikali kuhusika katika kufanya kikao hicho, ambapo Mandele alipofanya mahojiano na mwandishi wetu alithibitisha kwa kauli yake akisema kikao hicho kilifanyika Desemba Mosi mwaka huu, katika ofisi za makao makuu ya CCM wilayani Mbinga na madiwani hao walikubaliana juu ya kuvunjwa kwa kamati hiyo.

WASIMAMIZI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA MBINGA WAENDELEA KULALAMIKIA KUPUNJWA MALIPO YAO, WAMTAKA WAZIRI MWENYE DHAMANA KUINGILIA KATI


Hawa Ghasia, Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI.
Na Mwandishi wetu,

TUMEKUWA tukijiuliza maswali mengi lakini majibu hatuna, kubwa zaidi juu ya hatma yetu kama wafanyakazi ndani ya Halmashauri ya wilaya yetu ya Mbinga hapa mkoani Ruvuma, licha ya kuishi katika mazingira magumu baadhi yetu tumekuwa wafanyakazi tusiosikilizwa, tunaobezwa, kuzarauliwa, hata hatupaswi kuhoji wala kudai na kutimiziwa haki zetu za msingi.

Katika hali ya kawaida utumishi au kufanya kazi katika wilaya hii naweza nikasema imekuwa ni kero na mtihani mgumu mithili ya Swala ndani ya ngome ya Simba na Chui au utumwa katika nchi yao.

Tunajiuliza haya yote yanafanyika yanabaraka kutoka wapi? hivi jee Mkurugenzi wa wilaya hii, Hussein Ngaga ambaye ndiye mwajiri wetu anajua au kutambua thamani ya utumishi wa umma? au uongozi katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga imekuwa kama jambo la mzaha lisilohitaji busara weledi na taaluma,……………wakati wote tumekuwa tukijiuliza maswali haya kwa mwenendo uliopo sasa tunabaki kuumia kichwa tu.

Tulitaraji uongozi wa halmashauri ukiongozwa na mkurugenzi akiwa ndiye mwajiri, uwe makini katika kushughulikia matatizo ya watumishi wenzake lakini cha ajabu amekuwa kimya na chanzo cha kubeza kero na changamoto za watumishi wake, zaidi kumekuwa na manyanyaso yanayochangiwa na ofisi yake hasa kwa kupuuza haki stahiki za wafanyakazi.

Sunday, January 18, 2015

TUACHE KUCHEZEA AMANI YA TANZANIA, POLISI TUPATIENI UKWELI JUU YA PANYA ROAD

Padre Baptiste Mapunda.

Na Padre Baptiste Mapunda,

WATAALAMU siku zote wanasema mwanzo mbaya huashiria mwisho mbaya, hivyo basi kwa kauli hii mwaka huu 2015 Watanzania waishio Jijini Dar es Salaam  wameuanza vibaya kwa kutikiswa na kikundi cha “Panya Road.” 

Siku ya tarehe moja Januari ya kila mwaka duniani husherehekewa kama siku ya amani duniani, na amani hii tunayoitamka hapa ni ile inayotoka kwa Mungu na siyo ya bunduki wala mabomu.

Baba Mtakatifu kila mwaka huwa anatoa ujumbe wa amani kwa watu wote waliowakristo na wasiowakristo, mwaka huu ujumbe wake ulibeba kauli ya “sasa hakuna mtumwa” kwani sote ni kaka na dada. 

Nilivyomwelewa Baba Mtakatifu Francis anamaanisha kwamba utumwa wa aina yeyote ile ni alama ya kukosekana kwa amani moyoni, familia, jamii na dunia kwa ujumla wake. 

Duniani tumwa ni nyingi mathalani utumwa wa mawazo, wa kukosa uhuru, haki za binadamu, utumwa wa dhambi, wa kutawaliwa na hata ule wa umaskini. Watu wa jiji la Dar es Salaam mwaka huu walianza na utumwa wa kukosa amani ya kutembea kwa uhuru na furaha, kwa sababu ya  ujambazi, uhuni na uhalifu wa kikundi cha Panya Road.

MPANGO WA KUVUNJWA KAMATI YA MIPANGO NA FEDHA BARAZA LA MADIWANI MBINGA WAVUJA, MADIWANI WALALAMIKA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake alivyoketi hapa mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIKA hali ya kushangaza, hoja ambayo inadaiwa kupelekwa kwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga juu ya kutaka kuvunjwa kwa Kamati ya mipango na fedha ya halmashauri hiyo, imelalamikiwa na baadhi ya Madiwani wa wilaya hiyo na kuelezwa kuwa ni batili. Mtandao huu umeambiwa.

Ngaga anashutumiwa na madiwani wake kwamba, mpango huo wa kutaka kuvunja kamati hiyo amekuwa akiufanya chini kwa chini na tayari suala hilo, limefikishwa mezani kwake kwa utekelezaji, katika kikao cha baraza la madiwani kinachotarajiwa kuketi Januari 23 mwaka huu, wilayani humo.

Mpango huo umeelezwa kuwa unajidhihirisha pale mkurugenzi huyo alipovunja ratiba za vikao vya kamati husika, ambapo hata baraza hilo ilibidi liketi mwishoni mwa mwezi huu na sio tarehe hiyo, ambapo madiwani wake wameshangazwa na hali hiyo.

“Ratiba ya vikao vyote vya kamati amevivuruga na kupanga tarehe anazozitaka yeye, hata baraza hili la madiwani anataka kulifanya mapema kwa lengo la kuwakusanya baadhi ya watu wake (madiwani) ili waweze kufanikiwa mipango yao waliyojiwekea”, walisema.

Malalamiko hayo yametolewa kwa nyakati tofauti na kufafanuliwa kuwa hakuna kikao ambacho madiwani hao walikaa na kukubaliana kuvunja kwa kamati hiyo, ambayo ndio mhimili wa kamati zote za baraza la madiwani.

Thursday, January 15, 2015

WADAU WA ELIMU WALIA NA SERIKALI, KATIBU MKUU TAMISEMI AWASHANGAA NA KUWALAUMU MADIWANI WA MBINGA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Na Kassian Nyandindi,

Ruvuma.

BAADHI ya Madiwani na Wadau wa elimu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuacha kufumbia macho tatizo la mgogoro uliopo kati ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein Ngaga na baadhi ya watumishi wake wa idara ya elimu msingi huku wakieleza kuwa hatua zisipochukuliwa mapema huenda wilaya hiyo ikarudi nyuma kimaendeleo, hususani katika sekta ya elimu ambayo wilaya inaonekana kwa sasa ikifanya vizuri.

Wadau hao wameinyoshea kidole ofisi ya TAMISEMI wakidai kuwa, imekuwa ikimbeba Mkurugenzi huyo licha ya matatizo yaliyopo hapa wilayani kuwafikia.

Aidha walisema kuwa Ngaga amekuwa chanzo cha migogoro kazini, ambapo muda mwingi haelewani na baadhi ya watumishi wenzake, hususani wa idara ya elimu msingi.

Imedaiwa kuwa matatizo hayo yapo mezani kwa viongozi wa TAMISEMI ikiwemo hata kwa Katibu Mkuu, Jumanne Sagini lakini wanashangaa kuona kutochukua hatua madhubuti ikiwemo kumwajibisha mkurugenzi huyo, ambaye sasa amekuwa kero kwa madiwani hao na wananchi wa wilaya hiyo.

Walisema ni wakati sasa kwa ofisi hiyo kuchukua hatua na sio kukaa kimya, ukizingatia kwamba kilio cha wanambinga juu ya kukerwa na migongano kazini ambayo anaiendekeza mkurugenzi huyo, imedumu kwa muda mrefu.

Wednesday, January 14, 2015

TAMISEMI NAPATA SHIDA KUMUONA MKURUGENZI WENU WA MBINGA ANAPOENDELEA KUPANDIKIZA MIGOGORO NA SERIKALI KUWA KIMYA KUTOMCHUKULIA HATUA

Jumanne Sagini, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM - TAMISEMI)

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

KATIKA hali inayoonesha kwamba ni utendaji mbovu katika kuongoza sekta ya umma na kuendelea kupandikiza chuki miongoni mwa jamii, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani hapa, Hussein Ngaga ameendelea kulalamikiwa na baadhi ya Madiwani wake kwamba amekuwa akisambaza pesa (Rushwa) kwa lengo la kushinikiza madiwani hao wajenge hoja ya kumkataa Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias Mkali. Mtandao huu umeelezwa.

Kadhalika inadaiwa pia Gaudence Kayombo, Mbunge wa jimbo la Mbinga naye amekuwa akishiriki kwa namna moja au nyingine kushawishi baadhi ya Madiwani wamkatae afisa elimu huyo, kwenye kikao cha baraza la madiwani hao ambacho kitaketi mwishoni mwa mwezi huu.

Siri hiyo imevuja baada ya wengi wao wakishangaa na wengine kuchukizwa na kitendo hicho wakihoji kwa nini wanafanya hivyo, na kuwataka waachane na tabia hiyo ambayo huenda baadaye ikawageuka wao wenyewe na kuwaweka mahali pabaya.

Mwandishi wa habari hizi ameelezwa na vyanzo vyetu mbalimbali kuwa, kwa nyakati tofauti vikao vimekuwa vikifanyika ofisini kwa mkurugenzi huyo na hata nyumbani kwake, kupanga mikakati ya kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa kwa njia yoyote ile.

Saturday, January 10, 2015

HALMASHAURI YA MBINGA YAINGIA KATIKA KASHFA MPYA, YALALAMIKIWA KUKUMBATIA FEDHA ZA MRADI WA MAJI KIGONSERA

Waziri wa maji, Profesa Jumanne Maghembe.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKAZI wa kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameutaka uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo  kurejesha haraka iwezekanavyo fedha zao za mradi wa maji wa kijiji hicho, ambazo zimekaa kwa muda mrefu na mradi kushindwa kuendelea kufanyiwa ukarabati.

Shilingi milioni 11.3 ambazo wananchi wa kijiji hicho walichangiana kwa ajili ya kuboresha mradi wao wa maji kijijini hapo, ndizo ambazo wanalalamikia na mradi huo wa wananchi umesimama kufanyiwa ukarabati kutokana na kukosa fedha.

Akitolea ufafanuzi juu ya fedha hizo, Mwenyekiti wa mradi wa maji katika kijiji hicho cha Kigonsera Izack Komba alisema baada ya kukamilisha kazi ya kuchangisha fedha hizo waliambiwa waziingize kwenye moja kati ya akaunti ya halmashauri ya wilaya hiyo, mpaka baadae watakapokamilisha kufungua akaunti yao ya mradi katika benki ya NMB tawi la Mbinga.

Mwenyekiti huyo alisema licha ya kukamilisha taratibu husika za kufungua akaunti katika benki hiyo, ni mwaka mmoja sasa umepita fedha hizo hazijaingizwa kwenye akaunti ambayo wameifungua katika tawi hilo, na wanashindwa kuendelea kufanya ukarabati wa mradi wao wa maji hapo kijijini na hivi sasa upo katika hali mbaya.

WAFANYABIASHARA MBINGA WALALAMIKIA SERIKALI KUPANDISHA KODI YA MAPATO

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
CHEMBA ya Wanyafabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imeshangazwa na kitendo cha serikali kupandisha kodi kwa asilimia miamoja huku ikielezwa kuwa ongezeko hilo halilingani na ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo ni vyema mahesabu hayo ya kodi ambayo yalipitishwa na Bunge yakaangaliwa upya na kufanyiwa marekebisho, ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara yanayoendelea kujitokeza miongoni mwa jamii.

Aidha walihoji ni kiwango kipi kilitumika na serikali kukokotoa na kuweka ongezeko hilo ambalo ni kubwa, wakati wakijua fika hali ya uchumi wa nchi kwa sasa sio nzuri na kwamba kufanya hivyo ni sawa na kuwaumiza wafanyabishara, hasa kwa wale wenye mitaji midogo.

Hayo yalisemwa na wafanyabiashara hao, katika kikao cha pamoja walichoketi kwenye ukumbi wa chuo cha maendeleo ya wananchi (FDC) mjini hapa, na kuhudhuriwa na Afisa msemaji mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Hamis Lupenja, ambaye alikuwa akimwakilisha Kamishna mkuu wa mamlaka hiyo hapa nchini.

Philemon Msigwa ambaye ni afisa mtendaji mkuu wa TCCIA wilayani humo, alisema wafanyabiashara wa wilaya hiyo kwa muda mrefu wamekuwa pia wakilalamikia kodi ya mapato wanayolipa hapa Mbinga ni kubwa, kutokana na makampuni yanayofanyabiashara wilayani humo kulipa kodi nje ya wilaya hiyo.

TANZANIA TUIMARISHE AMANI TUSIINGIE KATIKA MACHAFUKO UCHAGUZI MKUU MWAKA HUU

Padre Baptiste Mapunda.

Na Padre Baptiste Mapunda,

MIMI siyo nabii lakini leo hii napenda kutoa maono yangu juu ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huenda kutakuwa na uwezekano wa kumwagika damu  kutokana na usomaji wa alama za nyakati. Tukubali kwamba dunia ya leo inaogopa sana maono hasa yanayotishia madaraka ya wanasiasa wetu mufilisi.

Maono ni elimu inamhusu Mwenyezi Mungu awezaye na  ajuaye yote, hivyo basi mwanadamu kujidai anajua sawa na Mungu ni kufuru ya hali ya juu. Lakini Mungu huyo aliyemuumba mwanadamu kwa mfano na sura  yake anaweza kumfunulia mambo fulani ili aweze kuwaeleza wanadamu kuwaonya, kuwahabarisha au kuwaelekeza.

Maovu yanavyoendelea kutokea katika nchi yetu kwa  kusoma alama za nyakati najiuliza  swali moja; Je Tanzania  inakwenda kuingia katika historia ya umwagaji damu  uchaguzi mkuu wa mwaka huu? Hakika kwa maovu mengi ya nchi yetu sasa hivi ni wazi nchi haipo salama.

Nchi yetu kwa muda wa miaka mitatu sasa  imepitia  katika matukio na maovu ya ajabu ambayo yanashitua mustakabali wa  jamii  mzima, kumekuwa na mauaji   ya Albino, na utekaji wa raia wema na kujeruhi mfano Dokta Ulimboka, marehemu Dokta Mvungi, yakiwemo mauaji ya mwandishi wa habari David Mwangosi.

Thursday, January 8, 2015

WANUSURIKA KIFO BAADA YA KUPIGWA RISASI NA MAJAMBAZI



Na Gideon Mwakanosya,

Songea.


JESHI  la Polisi mkoani Ruvuma linawasaka watu wanne  wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao wanadaiwa kuwapiga risasi watu wawili, katika matukio tofauti likiwemo la mwanamke  ambaye ni mhudumu wa baa kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi mgongoni, kisha kunyanganywa simu ya  mkononi yenye thamani ya shilingi 35,000 na kutokomea nayo kusiko julikana.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa matukio yote mawili yametokea majira ya saa za usiku  huko katika maeneo ya Mabatini kata ya Misufini na Mfaranyaki mjini songea.

Kamanda Msikhela alisema kuwa  tukio la kwanza lilitokea  majira ya saa mbili usiku huko katika mtaa wa mabatini kwenye eneo la kando kando ya ukuta  wa msikiti wa , uliopo kata ya Misufini ambapo Fatuma Hamisi (29) ambaye ni mhudumu wa baa ya Olympic iliyopo mjini hapa, wakati akielekea kazini kwake ghafla alifuatwa na kijana  mmoja mwembamba aliyevalia kofia aina ya mzura ambaye hakufahamika kwa jina, na kumuamuru Fatuma asimame.

JESHI LA POLISI RUVUMA LABAINI MTANDAO WA KIGAIDI



Na Mwandishi wetu,
Songea.

JESHI la polisi mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na  vyombo vingine vya ulinzi na usalama limefanikiwa kukitambua  kikundi cha mtandao wa kigaidi  ambacho kinadaiwa kujihusisha na  majaribio matatu, ya  kuwashambulia  askari polisi wakiwemo wa kikosi cha usalama barabarani  na tayari linawashikilia watuhumiwa  kadhaa ambao majina yao yamehifadhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa,  Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela alisema kuwa Jeshi la polisi limefanikiwa kumtambua mtuhumiwa aliyelipukiwa na bomu hivi karibuni,  pamoja na mtandao wote unaojihusisha na matukio matatu ya  kigaidi ya ulipuaji mabomu, yaliyolenga kuwashambulia askari hao.

Alisema marehemu huyo jina lake limehifadhiwa, ambapo imebainika kuwa ni mzaliwa wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, ambaye alizikwa  Desemba 31 mwaka jana baada ya Baba yake mzazi kujitokeza  na kuchukua mwili wa mtoto wake na kwenda kuuzika.

MWANDISHI WA HABARI JINO KWA JINO NA GAUDENCE KAYOMBO, UCHAGUZI MKUU MWAKA HUU

Humphrey Kisika.
Na Kassian Nyandindi,


Mbinga.

KWA vyovyote iwavyo, mapigo ya moyo ya Mbunge wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, Gaudence Kayombo yataongezeka mara dufu baada ya kijana msomi ambaye ni Afisa Habari wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Humphrey Kisika (32) kutangaza nia ya kuwania ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
 
Kisika ambaye ni msomi mwenye shahada ya kwanza ya uandishi wa habari, pia ni mwanafunzi wa chuo Kikuu cha Iringa, anayesoma shahada ya pili ya uandishi wa habari na utawala, anataka kuwania nafasi hiyo kupitia chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na wanahabari kijijini kwake Ukata wilayani Mbinga, alisema anataka kupokea kijiti toka kwa Mbunge huyo wa sasa, ili atumie maarifa aliyonayo kusukuma zaidi maendeleo ya jimbo hilo.

Alisema anautambua na kuuthamini mchango wa mbunge wa sasa katika kusukuma maendeleo ya jimbo hilo, lakini kuna haja akampokea kijiti hicho ili aongeze kasi yake.

SERIKALI KUJENGA RELI KUTOKA MTWARA HADI MBAMBA BAY, WALIOVAMIA MAENEO YA UWANJA WA NDEGE SONGEA NA KUJENGA MAKAZI WATAKIWA KUONDOKA

Dokta Harrison Mwakyembe.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAZIRI wa uchukuzi Dokta Harrison Mwakyembe amesema, serikali nchini imedhamiria kujenga reli kuanzia Mtwara hadi Mbamba Bay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, jambo ambalo litarahisisha kazi ya ubebaji wa mizigo mizito ya makaa ya mawe na chuma kutoka Liganga wilayani Ludewa mkoa wa Njombe.

Akizungumza na Wadau wa usafirishaji jana katika ukumbi wa Ikulu ndogo mjini hapa, Dokta Mwakyembe alisema ujenzi wa reli hiyo unatarajiwa kuanza mapema mwakani na kwamba utakamilika mwaka 2018.

Alisema kujengwa kwa reli hiyo kutasaidia barabara za lami zilizopo na zinazoendelea kujengwa katika mikoa ya kusini, kutoharibika mapema kutokana na kupitisha magari yanayobeba mizigo ya makaa ya mawe na chuma na kuzifanya zidumu kwa muda mrefu.

Monday, January 5, 2015

VIONGOZI WA DINI TANZANIA BADILIKENI MWAKA 2015

Na  Padre Baptiste Mapunda,

NIMEANDIKA mara nyingi sana juu ya wajibu wa viongozi wa dini katika jamii. Hao ni viongozi wa dini lakini pia hawawezi kusahau kuwa ni viongozi wa jamii ambao wanaaminiwa na watu wengi sana.

Viongozi wa dini ni wadau wakubwa sana katika suala nzima la ujenzi wa demokrasia, hakiza za binadamu, maendeleo ya nchi, na utawala bora lakini kubwa zaidi viongozi hawa lazima  wahamasishe  uhuru  wa mawazo  pamoja na kuutetea ukweli na haki sawa hasa kwa wanyonge.

Mimi sitegemei kiongozi kuwa mwoga wa kusema ukweli pale ambapo serikali inapokosea halafu viongozi wa dini tunageuka kuwa wanafiki. Hii siyo injili ya Yesu Kristo na siku zote injili ya Yesu inasema  viongozi wa dini ni manabii katika jamii.

Mwaka huu 2015 ni mwaka wa pekee sana katika nchi yetu kwa sababu ya matukio muhimu hasa ya uchaguzi mkuu na upitishwaji wa katiba inayopendekezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ninayoiita katiba haramu ya CCM.

Kutokana na masuala hayo na makando kando yake kama umuhimu wa kuunda tume huru ya uchaguzi, uandikishwaji na uboreshwaji wa daftari la wapiga kura, viongozi wa dini wanamezewa mate mengi sana na wanaccm kuona kama watakuwa upande wao au wa wapinzani, au watabaki katikati kutafuta maslahi ya jamii.

Kama alivyosema Mwadhama Cardinali Pengo katika sikukuu ya kusherehekea miaka 70 ya uhai wake kwamba tulipofikia kama nchi sasa tunahitaji mabadiliko. Alikwenda mbali zaidi nakusema kwamba mabadiliko haya yataletwa kwa kuunganisha nguvu za watu maskini ili kuwaondoa viongozi matajiri waliopo madarakani.

Friday, January 2, 2015

BREAKING NEWS: MBINGA WATOTO WANUSURIKA KIFO BAADA YA KUTOKEA MLIPUKO WA KITU CHENYE NYAYA NYINGI

Hapa ni Jalalani karibu na shamba la mahindi mtaa wa Kiwandani Mbinga mjini mkoani Ruvuma, ambako watoto sita waliokota kifaa chenye nyaya nyingi, ambacho baadae kiliwalipukia na kuwajeruhi.

Mtoto Emmanuel Mwingira (7) akiwa amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, baada ya kulipukiwa na kitu kilichokuwa kimetengenezwa na nyaya nyingi wakati alipokuwa akicheza na wenzake na kusababisha kuumia mkono wake wa kulia, na sehemu mbalimbali za mwili wake.
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

WATOTO wanne kati ya sita wamenusurika kifo, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma baada ya kuwalipukia kitu ambacho kimeunganishwa na nyaya nyingi na kuwajeruhi vibaya, wakati mwenzao mmoja akiwa amekishika anaunganisha nyaya hizo walipokuwa wanacheza pamoja. 

Taarifa za awali ambazo zilisambaa mjini hapa, ilielezwa kuwa mlipuko huo ulitokana na kitu ambacho kilizaniwa kuwa ni bomu ambalo limetengenezwa kienyeji, jambo ambalo sio kweli.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela, ambaye alikuwa eneo la tukio alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alithibitisha kuwa, tukio hilo limetokea leo majira ya saa 5:00 asubuhi katika mtaa wa Kiwandani mjini hapa, wakati watoto hao wakiwa wanachezea kitu ambacho kilikuwa kimeunganishwa na nyaya nyingi.

Msikhela alikitaja kitu hicho kuwa ni kilipuzi ambacho hupenda kutumika na watafiti wa madini migodini au walipuaji baruti, huku akieleza kuwa tukio hilo ni la bahati mbaya ambapo liliwakumba watoto hao baada ya kuokota kifaa hicho jalalani.