Sunday, September 27, 2015

BEROYA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA UDANGANYIFU WA MITIHANI

Ofisa elimu Sekondari Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Leo Mapunda kushoto, akimsikiliza mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Beroya, Mary Komba namna ya kupima mvua kwa kutumia vifaa vya kisasa ambavyo vinawasaidia katika masomo yao, kati kati ni Mkurugenzi wa shule hiyo Sebastian Waryuba.
Na Muhidin Amri,
Songea.

WAHITIMU kidato cha nne, shule ya sekondari Beroya iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambao wanatarajia kufanya mitihani yao ya mwisho, Novemba mwaka huu wametakiwa kujiepusha na udanganyifu wa kutafuta majibu ya mitihani hiyo, badala yake watumie muda uliobaki kujisomea ili waweze kufanya vizuri na kufaulu kwa kupata alama za juu.

Aidha wameelezwa kuwa, serikali tayari imejipanga kudhibiti vitendo hivyo ili kuwadhibiti wanafunzi wenye tabia hiyo na kwamba wameshauriwa kutumia muda huu mfupi uliobakia, kujikumbusha yale waliyosoma na kufundishwa na walimu wao ili siku ya mwisho ya mitihani yao waweze kufuzu vigezo husika.

Ofisa elimu sekondari katika Manispaa hiyo, Leo Mapunda alisema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi katika mahafali ya saba kidato cha nne, shule ya sekondari Beroya yaliyofanyika juzi mjini hapa.

Thursday, September 24, 2015

TUNAONDOKA KATIKA ENEO LA MKUTANO

Wahamasishaji wa kampeni za Ukawa mjini Tunduru mkoani Ruvuma, wakiondoka katika eneo la mkutano huo mara baada ya kutangaziwa na Mwenyekiti wao, Said Mwidadi kwamba mgombea Edward Lowassa hatafika katika viwanja hivyo kwa ajili ya kuwahutubia wananchi. (Picha na Steven Augustino)

WANANCHI WATAKA KUJUA SABABU ZILIZOSABABISHA MGOMBEA UKAWA KUTOWASILI TUNDURU

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Said Mwitadi akitangaza kuahirishwa kwa mkutano huo wa kampeni leo mjini hapa, ambao ulitarajiwa kuhutubiwa na mgombea urais kupitia tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa hata hivyo wananchi hao walitangaziwa kwamba watapewa tena taarifa ni lini mkutano huo utaweza kufanyika. Pia Mwenyekiti huyo hakuweza kueleza ni sababu gani  za msingi zilizosababisha mgombea huyo wa urais kutowasili katika viwanja hivyo vya mkutano mjini Tunduru. ( Picha na Steven Augustino )

TUNDURU WATAWANYIKA BAADA YA MGOMBEA UKAWA KUTOWASILI KWENYE VIWANJA VYA MKUTANO

Baadhi ya wananchi ambao walijitokeza leo kumlaki mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa wakitawanyika kutoka eneo la Ofisi za Chama Cha Wananchi CUF mjini Tunduru mkoa wa Ruvuma, baada ya kutangaziwa kuwa mgombea huyo hatafika. ( Picha na Steven Augustino ).

MGONJWA AMSHAMBULIA KWA KIPIGO MUUGUZI WA HOSPITALI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mgonjwa ambaye alikuwa amelazwa Hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Mariam Njaidi amezua jambo baada ya kumshambulia kwa kipigo Muuguzi mmoja wa kitengo cha maabara katika hospitali hiyo, kutokana na kucheleweshewa majibu ya vipimo vyake vya magonjwa ya taifodi na sukari.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Thabit Mwambungu.
Mgonjwa huyo ambaye alikuwa amelazwa wodi namba tatu, aliwashangaza wagonjwa wenzake waliolazwa hospitalini hapo baada ya kuamka kitandani alipokuwa amelala na kwenda kumfuata muuguzi, Hiren Msokwa katika chumba cha maabara na kuanzisha mapigano kati yao ambaye baadaye alimkuta akiwa na majibu yake mikononi mwake.

Hali hiyo inadaiwa ilitokana na Njaidi kucheleweshewa majibu ya vipimo vya magonjwa hayo kwa zaidi ya siku tatu, ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.

Wednesday, September 23, 2015

AKAMATWA KWA KURUSHIA MAWE MSAFARA WA KAMPENI WA CCM

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limesema, limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja kati ya watano ambao walihusika katika tukio la kurushia mawe msafara wa kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kijiji cha Mtua, kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoani humo na kuharibu magari mawili.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu na kuongeza kuwa katika tukio hilo wengine watano, wametokomea kusikojulikana ambapo wanaendelea kuwasaka ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria, kujibu tuhuma inayowakabili.

Malimi alisema usiku wa kuamkia Septemba 22 mwaka huu, askari wake walifanya msako mkali katika kata hiyo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja kati ya hao, aliyemtaja kwa jina la Christopher Mapunda (32) ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.

MADEREVA WA PIKIPIKI MBINGA WAPEWA SOMO

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKUU wa Polisi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Ramia Mganga amewataka madereva wanaoendesha pikipiki wilayani humo, maarufu kwa jina la Yebo yebo kuacha kutumiwa vibaya na wanasiasa, jambo ambalo linahatarisha usalama wao na kusababisha malumbano yasiyokuwa ya lazima.

Aidha alikemea kitendo cha madereva hao baadhi yao kuleta vurugu, kuchoma moto bendera za vyama na kubandua mabango ya wagombea hao katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi, ambayo yamebandikwa katika maeneo mbalimbali jambo ambalo amewasihi kwa kuwaeleza kitendo hicho waachane nacho, kwani husababisha na kuleta mifarakano au mipasuko katika jamii.

Mganga alisema hayo alipokuwa akizungumza na baadhi ya waendesha pikipiki wa wilaya hiyo, katika viwanja vya eneo la stendi kuu ya magari ya abiria mjini hapa.

Tuesday, September 22, 2015

GAMA: NITAHAKIKISHA KINU CHA KUSINDIKA TUMBAKU KINAFANYA KAZI


Leonidas Gama akifurahia jambo na wapiga kura wake, katika moja ya mikutano yake ya kampeni jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma.
Na Muhidin Amri,
Songea.

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Leonidas Gama amesema iwapo wananchi wa jimbo hilo watamchagua kuwa mbunge wao, atahakikisha anarudisha kinu cha kusindika zao la tumbaku kikiwa kinafanya kazi ambacho kimejengwa jimboni humo kwa miaka mingi.

Mbali na hilo, Gama ameahidi kwa wananchi wake kwamba atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wakulima wa zao la mahindi, wanapata soko la uhakika la kuuzia mazao yao ili waweze kunufaika nalo na kuwafanya wasonge mbele kimaendeleo.

Gama ametoa ahadi hiyo juzi, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni katika kata ya Mshangano mjini hapa ambapo pia wanachama 20, wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walirudisha kadi za chama hicho na kujiunga na chama cha mapinduzi.

UVCCM TUNDURU YAWAONDOLEA HOFU WANANCHI SIKU YA KUPIGA KURA

Katibu mkuu Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM), Sixtus Mapunda.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imewataka wanachama wake na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi na kwenda kupiga kura bila uoga wala hofu ya aina yoyote, kwa lengo la kumchagua kiongozi wanayemtaka Oktoba 25 mwaka huu.

Katibu wa UVCCM wilayani humo, Juma Khatibu alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi waliohudhuria kwenye mkutano wa kampeni wa kuwanadi wagombea udiwani, katika kata za Masonya, Majengo na Mlingoti Mashariki mjini hapa.

Alisema kuwa umoja huo umechukua hatua hiyo, kufuatia kuwepo kwa taarifa za vitisho ambavyo husambazwa kwa njia ya vipeperushi wilayani humo, zenye nia ya kuwatia hofu wananchi wasipige kura.

MSAFARA WA KAMPENI CCM WASHAMBULIWA KWA MAWE

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MAGARI mawili yaliyokuwa katika msafara wa kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kijiji cha Mtua, kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma yameharibiwa vibaya baada ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuvamia msafara huo, na kurusha mawe huku watu waliokuwemo ndani ya magari hayo nao wakinusurika kuumia vibaya.

Tukio hilo lilitokea Septemba 19 mwaka huu majira ya jioni, ambapo Katibu wa CCM wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa ndiye aliyekuwa akiongoza msafara wa kampeni wa chama hicho katika kata ya Mpepai na vijiji vyake kwa lengo la kumnadi mgombea wa nafasi ya udiwani kupitia tiketi ya chama hicho, Benedict Ngwenya.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Chinowa alisema kuwa wakati wakiwa barabarani wanarudi wakitokea katika kijiji cha Mtua ghafla waliona magogo makubwa ya miti yakiwa yamewekwa barabarani, ili kuzuia wasiweze kupita na baadaye walipojaribu kuyatoa ndipo kundi la vijana lilijitokeza na kuanza kuwarushia mawe, ambayo yaliweza kuharibu na kuvunja vioo vya magari hayo yaliyokuwa katika msafara  huo.

Monday, September 21, 2015

TUNDURU YAJIVUNIA RASILIMALI ZAKE

Mnara wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Na Muhidin Amri,
Tunduru.

IMEELEZWA kwamba kuwepo kwa rasilimali nyingi, katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, ni moja kati ya sifa zinazoifanya wilaya hiyo kuwa miongoni mwa wilaya zinazofaa kwa shughuli za uwekezaji miradi mbalimbali ya maendeleo na kuifanya wilaya hiyo, iweze kukua kiuchumi.

Tina Sekambo ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu kuhusiana na mkakati uliopo wa kuitoa wilaya, katika umaskini na kuwa wilaya tajiri kwa kutumia rasilimali zake zilizopo.

Kwa mujibu wa Sekambo alisema kwamba, wilaya yake imebarikiwa kuwa na fursa nyingi kama vile ardhi inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali, mabonde na mito inayotiririsha maji mwaka mzima, ambayo kama itaendelezwa vizuri itaweza kusaidia hata katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

Friday, September 18, 2015

MACHANGUDOA SONGEA WATAFUTIWA DAWA

Mji wa Songea uliopo mkoani Ruvuma.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

OPARESHENI kabambe wakati wowote kuanzia sasa, huenda ikafanyika katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kwa lengo la kuwasaka na kuwakamata wasichana wanaofanya biashara ya kuuza miili yao, maarufu kwa jina la Machangudoa ambao huzurura nyakati za usiku kwenye mitaa mbalimbali ya mji huo.

Imeelezwa kuwa hatua hiyo itachukuliwa ikiwa ni lengo la kuunga mkono, mkakati wa serikali juu ya kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema kuwa zoezi hilo litafanywa na askari kanzu huku akiyataja maeneo yaliyoathirika zaidi kuwa ni mtaa wa Delux One, Ikweta, Serengeti, Majengo na maeneo ya Mfaranyaki ambako kuna idadi kubwa ya vijana wanaohusika kufanya vitendo hivyo.

MWAMBUNGU RUVUMA AWAPA SOMO JKT

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

VIJANA wanaomaliza mafunzo katika vikosi  mbalimbali, vya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) wametakiwa kutojihusisha na kuwa sehemu ya mgawanyiko kwa watanzania kwa misingi ya kuendekeza itikadi ya dini, siasa na ukabila jambo ambalo linaweza kusababisha uvunjifu wa amani hapa nchini.

Aidha wameshauriwa kuwapuuza wanasiasa ambao wanalengo la kuwatumia kwa maslahi yao binafsi katika kusaka uongozi, badala yake waweke kipaumbele cha kuisaidia jamii na kudumisha upendo na umoja.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alipokuwa akifunga mafunzo ya miezi mitatu kwa vijana 1,124 katika kikosi cha 842 KJ Mlale wilayani Songea, mkoa humo.

Monday, September 14, 2015

BODI YA KAHAWA YASIKITISHWA WAKULIMA KUTOZINGATIA KANUNI ZA UBORA WA KAHAWA

Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

BODI ya Kahawa Kanda ya Ruvuma ambayo makao makuu ya ofisi yake ipo wilayani Mbinga mkoani humo, imesikitishwa na vitendo vya baadhi ya wakulima wa zao hilo wilayani hapa, kwa kutozingatia kanuni za ubora wa kahawa, jambo ambalo linachangia kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo.

Aidha imekemea na kuwataka wakulima hao, kuacha tabia ya kuanika kahawa chini jambo ambalo nalo huchangia kushuka kwa ubora wake, badala yake wanatakiwa kuanika kwenye vichanja vyenye urefu wa mita moja kutoka ardhini, ili isiweze kupata vumbi na thamani yake isiweze kuporomoka.

Peter Bubelwa ambaye ni Meneja wa kanda hiyo, alisema hayo wakati alipokuwa akijibu maswali ya mwandishi wetu ambaye alitembelea ofisini kwake, kutaka kujua maendeleo ya uzalishaji wa zao la kahawa ya wilaya ya Mbinga ambapo ni wilaya pekee mkoani Ruvuma, inayozalisha zao hilo kwa wingi.

WACHAFUZI WA MAZINGIRA MJI WA MBINGA KUPIGWA FAINI

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Simon Ngaga akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake vya kikazi wilayani humo.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKAZI wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuuweka mji huo katika hali ya usafi wakati wote ili waweze kuepukana na magonjwa yanayoweza kutokea hapo baadaye, kutokana na taka kuzagaa ovyo.

Aidha kwa atakayekamatwa akionekana anachangia kuufanya mji huo uwe katika hali mbaya ya uchafu kwa kutupa taka katika maeneo ambayo sio rasmi, wamepewa onyo kwamba watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini ya shilingi 50,000 pamoja na kufikishwa Mahakamani, ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Ofisa afya wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, Felix Matembo alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusisitiza kuwa halmashauri hiyo, imejiwekea mikakati kabambe ya kuhakikisha kwamba suala hilo linapewa kipaumbele ili kuweza kuepukana na madhara yatakayoweza kuathiri jamii.

Sunday, September 13, 2015

TUNDURU WAISHUKIA UKAWA WAPONDA KUPOKELEWA KWA LOWASSA

Wananchi wakiwa katika mikutano mbalimbali ya kisiasa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.
Na Muhidin Amri,
Tunduru.

WANACHAMA 153 kutoka Chama cha wananchi CUF na CHADEMA katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wamevihama vyama hivyo na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakidai kuwa wamechoshwa na siasa zisizokuwa na malengo kwa Watanzania, pamoja na udikteta unaofanywa na viongozi wa vyama hivyo kufanya maamuzi mbalimbali bila kushirikisha wanachama wao.

Miongoni mwa wanachama hao, 120 ni wa kutoka CUF na 33 CHADEMA walitangaza juzi kuhama katika vyama hivyo, mbele ya katibu wa Chama Cha Mapinduzi wa wilaya hiyo, Mohamed Lawa tukio ambalo liliambatana na kurudisha kadi za vyama hivyo.

Walisema kuwa kwa muda mrefu sasa vyama hivyo vimekosa demokrasia ya kweli, ambapo viongozi wake ni watu ambao wamekuwa wakifanya maamuzi ambayo yamekuwa kinyume na matarajio ya watanzania walio wengi, wanaohitaji maendeleo.

Waliongeza kuwa hata kupokewa kwa Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo na hatimaye kuwa mgombea urais wa Ukawa, ni udhaifu alionao Freeman Mbowe, James Mbatia na Maalim Seif Sharif kwani hapakuwa na sababu ya wao kumpokea Lowassa kwani mgombea wa kiti hicho hajawahi kukanusha wala kuwaeleza wananchi, ukweli juu ya tuhuma za ufisadi zilizomkabili akiwa ndani ya CCM.

TUNDURU WATAKIWA KUTOGAWA ARDHI YAO KWA WAGENI

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WANANCHI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameaswa kujiepusha na vishawishi vinavyosababisha kuuza ardhi yao kwa wageni bila kufuata taratibu za nchi, ikiwa ni lengo la kuwafanya waweze kuepukana na vitendo vya uporaji vinavyofanywa na watu wajanja, hatimaye kuwa maskini na watumwa katika nchi yao.

Badala yake wametakiwa kutumia utajiri wa ardhi waliyonayo, kuzalisha kwa wingi mazao mbalimbali ili wajikwamue na waondokane na umaskini.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mohamed Lawa alisema hayo alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho, katika kijiji cha Nandembo kwenye ziara yake ya kikazi ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika mikutano ya kampeni ya wagombea wa chama hicho, inayoendelea sasa hapa nchini.

Saturday, September 12, 2015

NYASA WAIPONGEZA NMB KWA KUANZISHA HUDUMA ZA KIFEDHA

Ziwa Nyasa lililopo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

BAADHI ya wananchi wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamepongeza jitihada zinazofanywa na Benki ya NMB kwa kuanzisha na kutoa huduma za kifedha wilayani humo, jambo ambalo limekuwa ni mkombozi kwao katika kuendeleza biashara zao.

Walisema kitendo cha benki hiyo kutoa huduma ya kufungua akaunti, kulipa hundi, kuweka na kutoa fedha kwa kutumia mfumo wa Benki jamii (Bank on Wheel) kumeweza kuwapunguzia umbali mrefu wa kufuata huduma hiyo ambapo awali walikuwa wakilazimika kwenda wilaya ya Mbinga, ili waweze kupata mahitaji ya kifedha katika taasisi hiyo ya kifedha.

Aidha walifafanua kuwa wilaya ya Nyasa ni wilaya mpya, ambayo tokea kuanzishwa kwake sasa ni faraja kwa wananchi wa wilaya hiyo, kusogezewa karibu huduma hiyo muhimu kwa faida ya maendeleo yao.

Friday, September 11, 2015

NAMTUMBO WAITAKA SERIKALI KUYADHIBITI MAKAMPUNI YANAYONUNUA TUMBAKU

Mkulima akiwa katika shamba la tumbaku akiboresha zao hilo.
Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.

WAKULIMA wanaozalisha zao la tumbaku wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wameitaka serikali kuhakikisha inadhibiti ipasavyo tabia ya makampuni binafsi yanayonunua zao hilo wilayani humo kwa njia za ujanja ujanja, yanachukuliwa hatua za kisheria kwani utekelezaji huo usipofanyika mapema huchangia kwa kiasi kikubwa, kuwaibia wakulima na kuwaacha wakibaki maskini.

Aidha walieleza kuwa kumekuwa na mtindo unaotumika wakati wa kununua zao hilo kwa kutumia fedha za kigeni, jambo ambalo wakulima wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya kiwango halisi cha thamani ya fedha anayotakiwa kulipwa mkulima husika.

Baadhi yao walisema wanakabiliwa na tatizo hilo, kutokana na wengi wao wanaolima tumbaku kutofahamu mabadiliko ya fedha hizo pale wanapolipwa na makampuni hayo, wakati wa msimu wa mauzo ya zao hilo.

CCM TUNDURU YAIRUSHIA KOMBORA VYAMA VYA UPINZANI

Na Muhidin Amri,
Tunduru.

SIKU chache baada ya Chama cha wananchi (CUF) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kuanza kampeni za wagombea wake wa ubunge katika Jimbo la Tunduru kaskazini na kusini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na kueleza kuwa wagombea waliosimamishwa na chama hicho cha wananchi hawana uwezo na wasitegemee kupata kura za ushindi, badala yake wagombea wa chama cha mapinduzi ndio watakaoweza kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu ujao, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

CCM imedai kwamba wagombea waliowekwa na chama hicho, Dustan Majolo Tunduru kaskazini na Thabiti Bakiri Jimbo la Kusini ni mteremko kwa chama hicho tawala kuelekea kupata ushindi, ambapo kinawafananisha wagombea hao sawa na kumsukuma mtu mlevi ambaye hana uzito wa kujizuia wakati anaposukumwa, kwa kile walichoeleza kuwa hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana vyama hivyo viliangukia pua.

Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa wilaya hiyo, Juma Khatibu alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mjini Tunduru, ambapo alidai kuwa wagombea hao ni dhaifu kisiasa na hawana uwezo wa kukidondosha chama hicho cha mapinduzi.

WAJASIRIAMALI NAMTUMBO WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA

Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.

WAJASIRIAMALI wadogo wilaya ya Namtumbo mkoa wa Ruvuma, wamehimizwa kuchangamkia fursa katika maeneo maalumu yaliyotengwa wilayani humo, kwa ajili ya ujenzi wa vibanda vya biashara na shughuli nyingine za ujasiriamali ili waweze kuepukana na usumbufu wanaoupata, kwa kufanya shughuli zao kwenye maeneo ambayo hayajaruhusiwia.

Halmashauri ya wilaya hiyo, imetenga viwanja zaidi ya 300 ambavyo hivi karibuni baada ya taratibu husika kukamilika vitaanza kugawiwa kwa watu wa makundi yote, kwa ajili ya ujenzi wa vibanda hivyo.

Kwa ujumla ugawaji huo utafanywa karibu na eneo linalotarajiwa kujengwa kituo kipya cha mabasi Namtumbo mjini, huku ikisisitizwa kuwa zoezi hilo litapewa kipaumbele zaidi kwa watu waliojiunga kwenye vikundi ambavyo, hujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Monday, September 7, 2015

NALICHO NAMTUMBO AWATAKA WANASIASA KUTOKUWA CHANZO CHA VURUGU

Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.

WAKATI joto la uchaguzi likiendelea kupanda kwa vyama vya siasa na wagombea wake ndani ya vyama hivyo, imeshauriwa kuwa ni vyema wagombea hao wajenge moyo wa subira na uvumilivu juu ya mambo yanayohusiana na maslahi ya taifa, ikiwemo kutoa nafasi kwa wananchi kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo na sio kuwa chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa dini na wagombea nafasi mbalimbali za uongozi katika vyama vya siasa, wilayani humo.

Nalicho alisema kuwa suala la maslahi ya kitaifa ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele, na wanasiasa kuacha kutanguliza maslahi yao binafasi ili waweze kuwatumikia vyema Watanzania.

WAKULIMA WANAOZALISHA MUHOGO WAASWA

Vichanja bora vya kukaushia mihogo.
Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

IMEELEZWA kuwa kukosekana kwa ubunifu na maeneo ya kufanyia biashara kwa wasindikaji wadogo, bidhaa zitokanazo na zao la muhogo wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma kunasababisha kuongezeka kwa watu maskini kutokana na wakulima husika katika maeneo mengi ya wilaya hiyo, kukosa mbinu na utaalamu wa kilimo cha zao hilo na kujikuta wakipoteza nguvu na muda mwingi wa kufanya kazi hiyo.

Aidha uzalishaji usiozingatia viwango vyenye ubora nayo ni sababu nyingine, ambayo mkulima wa zao hilo anakosa mafanikio, licha ya jitihada na nguvu kubwa anayoitumia wakati anapozalisha zao hilo.

Mbali na hilo usindikaji umekuwa ukifanywa kwa kutumia vifaa duni, tatizo ambalo limekuwa likichangia bidhaa zinazozalishwa kutokana na muhogo kukosa soko la uhakika, na wakulima kuendelea kuwa masikini ikilinganishwa na wakulima wanaozalisha mazao mengine.

TASAF NAMTUMBO YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE KAYA MASKINI ZANUFAIKA NA MPANGO WAKE

Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

SERIKALI imelipa kiasi cha shilingi milioni 257,004,000 kwa kaya maskini 56 ambazo ziliibuliwa wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, kupitia mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) awamu ya tatu ili ziweze kuwasaidia kugharimia mahitaji yao muhimu, ikiwemo matibabu, chakula na kulipa karo za watoto wao shuleni.

Ofisa ushauri na ufuatiliaji kutoka katika mfuko huo wilayani humo, Edson Kagaruki alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, huku akiwataka walengwa walioibuliwa kwenye mpango huo kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na sio kunywea pombe au kuongeza idadi ya wake majumbani kwao.

Kagaruki alisema, baada ya zoezi la uandikishaji na usajili waliweza kuibua kaya hizo kutoka katika vijiji 42, ambavyo viliingizwa kwenye mpango huo wa awamu ya tatu.

Friday, September 4, 2015

GAMA: EPUKENI KUCHAGUA VIONGOZI WATOA RUSHWA

Leonidas Gama.
Na Muhidin Amri,
Songea.

WAKATI kampeni zikiendelea kwa wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa, nafasi ya Rais, mbunge na diwani wito umetolewa kwa wananchi wa Jimbo la Songea mkoani Ruvuma kuepuka kuchagua viongozi watoa rushwa, kwani kufanya hivyo hakutaweza kusaidia kupata kiongozi bora atakayeweza kuwaongoza wananchi.

Mwito huo umetolewa na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Leonidas Gama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mjini hapa.

Gama ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, amewataka wanaccm kuungana pamoja ili kuweza kuleta ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao na sio kuendeleza majungu na makundi ndani ya chama hicho, ambayo yanahatarisha uvunjifu wa amani katika jamii hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.

“Nawaomba wanachama wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi, tuvunje makundi tuungane pamoja ili tuwashinde wagombea wa vyama vingine vya siasa”, alisema Gama.

DED NAMTUMBO AWAONYA WATUMISHI WAKE KUTOJIINGIZA KWENYE SIASA

Na Mwandishi wetu,
Ruvuma.

SERIKALI wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, imewaonya watumishi wake na kuwataka kutojiingiza katika vitendo vya kushabikia na kuzungumzia mambo siasa wakiwa ofisini, kwani kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu na maadili mahali pa kazi.

Imeelezwa kuwa kufanya hivyo kunapunguza muda wa kuwatumikia wananchi, badala yake waongeze juhudi kutekeleza majukumu yao waliyopewa na serikali ili kuweza kuleta tija katika jamii, ikiwemo upatikanaji wa huduma muhimu kwa faida ya maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya hiyo, Ally Mpenye alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya taratibu za maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika, oktoba 25 mwaka huu kwa nafasi ya Rais, diwani na mbunge ambapo kwa mamlaka aliyonayo yeye ndiye msimamizi mkuu wa uchaguzi huo ndani ya wilaya.

NGONYANI: WALIOSHINDWA KWENYE MCHAKATO KURA ZA MAONI CCM TUACHE KUPAKANA MATOPE

Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyefanikiwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kura za maoni, kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya ubunge kupitia tiketi ya chama hicho Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, Edwin Ngonyani amewasihi wanachama wenzake walioshindwa kwenye mchakato huo kuacha kupakana matope au kufikiria kukihama chama hicho, bali waungane pamoja ili kukipa nguvu na hatimaye kiweze kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Tabia na mawazo ya namna hiyo alieleza kuwa hayana mantiki yoyote ile, kwa kile alichodai kuwa hata kama watakimbilia kwenye vyama vingine vya siasa kwa lengo la kutafuta uongozi, bado nafsi zao zitawasuta.

Ngonyani aliyasema hayo muda mfupi mara baada ya msimamizi wa uchaguzi kura za maoni wilayani humo, Oscar Msigwa kumtangaza kuwa ndiye aliyeshinda kugombea nafasi hiyo ya ubunge katika jimbo hilo.

BABA ASHIKILIWA NA POLISI KWA KUFANYA MAPENZI NA MWANAE

Na Steven Augustino,
Songea.

MKAZI mmoja anayeishi katika mtaa wa Lizaboni Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Abdalah Bakari (43) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma ya kumwingilia kimapenzi mtoto wake wa kike, mwenye umri wa miaka 11.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 10 mwaka huu majira ya usiku, baada ya binti huyo (Jina tunalo) kwenda kulalamika kwa majirani zake, juu ya unyama huo aliofanyiwa.

Akifafanua juu ya tukio hilo, Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa binti huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi Amani iliyopo mjini hapa, alidai kuanza kufanyiwa kitendo hicho na baba yake huyo mzazi mwanzoni mwa mwezi wa saba mwaka huu.

Msikhela alisema baba huyo ambaye ni mzaliwa wa wilaya ya Tunduru mkoani humo, imebainika kuwa alikuwa na mazoea ya kumfanyia mtoto huyo unyama huo mara kwa mara jambo ambalo mtoto, alishindwa kuendelea kuvumilia juu ya maumivu aliyokuwa akiyapata na kulazimika kwenda kutoboa siri hiyo, kwa majirani aliokuwa akiishi nao hapo mtaani.

WATAKIWA KUFANYA KAMPENI ZA KIUSTAARABU

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

VIONGOZI wa vyama mbalimbali vya siasa hapa Tanzania, wameendelea kushauriwa kufanya mikutano yao ya kampeni za siasa kiustaarabu, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, bila kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu uliopo hapa nchini.

Mkurugenzi wa shirika la maendeleo, mikoa na matawi ya Tanzania Red cross Society, Julius Kejo alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na wadau wa shirika hilo kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo, jinsi ya kukabiliana na majanga wakati wa kampeni hizo.
Aidha aliwakumbusha viongozi wa dini, kuongeza juhudi na kutoa mahubiri yanayolenga kusisitiza amani na utulivu katika nchi yetu, ili isiweze kujitokeza machafuko yanayoweza kuliangamiza taifa hili.

Kejo alisema endapo kampeni hizo zitafanyika bila kuathiri ubinadamu au utu wa mtu, upo uwezekano wa kutotokea matendo ambayo yanaweza kusababisha madhara katika jamii.

Thursday, September 3, 2015

LOWASSA: NITAKAPOINGIA MADARAKANI WALIOHUSIKA KUPANDA KWA DENI LA TAIFA NITAWAFIKISHA MAHAKAMANI

Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

EDWARD Lowassa ambaye ni mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hapa nchini, ambaye pia anawakilisha vyama vyote vya siasa vinavyounda umoja wa katiba wa wananchi (Ukawa) amesema atakapoingia madarakani atahakikisha analifanyia kazi suala la kupanda kwa deni la taifa na endapo atabaini kwamba kuna makosa yalifanyika juu ya kupanda kwa deni hilo, wale wote waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria.

“Nitawafikisha Mahakamani wale wote waliohusika katika jambo hili, ili waweze kulipa fedha walizotumia vibaya kinyume na taratibu za nchi, haiwezekani mzigo huu watishwe watanzania ambao ni maskini na wenye kipato cha chini”, alisema Lowassa.

Mgombea huyo wa Ukawa alisema hayo alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika jana kwenye uwanja wa shule ya msingi Kiwanjani uliopo mjini hapa.

Aidha alisema kuwa endapo ataingia Ikulu ataondoa ushuru wote wa mazao ambao wananchi wamekuwa wakitozwa, kwa kile alichoeleza kuwa nchi ya Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo zikitumika vizuri hakuna haja ya kuwasumbua wakulima kwa kuwakopa mazao yao na kuwatoza ushuru mdogo mdogo.

ACHOMWA KISU UBAVUNI KUTOKANA NA WIVU WA KIMAPENZI

Hiki ni kisu ambacho kinadaiwa kutumika katika tukio hilo.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

ATHUMAN Namamba (22) mkazi wa kijiji cha Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amenusurika kupoteza maisha baada kuchomwa kisu katika ubavu wake wa kushoto katika tukio linalodaiwa chanzo chake, ni wivu wa kimapenzi.

Majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya wilaya hiyo na hali yake ni mbaya, ambapo kisu hicho alichomwa na Halid Sinda mkazi wa kijiji hicho Agosti 16 mwaka huu, majira ya usiku baada ya kutokea mabishano kati yao ambapo mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu majeruhi huyo kwamba ana mahusiano ya kimapenzi na mchumba wake, Mwajuma Ndeka.

Taarifa zinaeleza kuwa mtuhumiwa, Sinda aliendeleza jazba na akafikia hatua ya kuchomoa kisu na kumchoma nacho, Athuman hali ambayo ilisababisha kutoka damu nyingi na kumsababishia maumivu makali.

Tuesday, September 1, 2015

ZIARA YA KAMPENI ZA CCM DOKTA MAGUFULI AENDELEA KUFUNIKA RUVUMA


Dokta John Magufuli akimkabidhi mgombea ubunge Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda Ilani ya Uchaguzi ya CCM wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika mjini hapa.

Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dokta John Mgufuli akionesha Ilani ya uchaguzi ya CCM, kabla ya kumkabidhi mgombea ubunge Jimbo la Mbinga vijijini, Martin Msuha wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika mjini hapa.

Dokta Magufuli akimsalimia mlemavu ambaye naye alijitokeza kwenye mkutano huo wa kampeni Mbinga mjini mkoani Ruvuma. 

Dokta John Magufuli akijinadi kwenye mkutano wa kampeni, Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma.

Mgombea ubunge Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, Jenista Mhagama akipokea Ilani ya uchaguzi ya CCM kutoka kwa mgombea Urais kupitia tiketi ya chama hicho, Dokta John Magufuli wakati wa mkutano huo wa kampeni. 


Mgombea Urais wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dokta Magufuli akiwapungia mkono wananchi, ikiwa ni ishara ya kuwaaga mara baada ya kujinadi katika Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma.

MATUKIO MBALIMBALI YA ZIARA YA KAMPENI YA DOKTA MAGUFULI RUVUMA

Dokta John Magufuli akisalimiana na Dada ya wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi wilayani Nyasa, kupitia CCM na Mhamasishaji mkuu Marehemu Kapten John Komba alipokwenda kuweka shada la maua kwenye kaburi la Komba katika kijiji cha Lituhi wilayani humo wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kampeni.

Dokta John Magufuli akiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu Kapten John Komba.

Dokta John Magufuli akiomba dua na viongozi wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mbele ya kaburi la marehemu, Kapteni John Komba kijijini Lituhi mkoani Ruvuma ambako alizikwa.

Dokta Magufuli akijinadi kwenye mkutano wa kampeni katika kijiji cha Lituhi wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.

Dokta John Magufuli akimnadi mgombea ubunge CCM Jimbo la Nyasa, Stella Manyanya katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Lituhi wilayani Nyasa.

DOKTA MAGUFULI AENDELEA KUPOKELEWA RUVUMA KWA KISHINDO

Mgombea Urais wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) John Magufuli, akiwapungia mikono wananchi waliowasili kwenye mkutano wa kampeni Mbinga mjini mkoani Ruvuma, ambapo aliahidi kuboresha kiwanda cha serikali cha kukoboa kahawa (MCCCO) na ujenzi wa barabara kiwango cha lami kutoka Mbinga mjini hadi Mbamba bay wilayani Nyasa.

Dokta John Magufuli akizungumza na wananchi wa Songea mjini mkoani Ruvuma, kwenye uwanja wa Majimaji ambapo aliwaeleza wananchi hao kuwa serikali yake itafanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

Mgombea Urais kupitia tiketi ya CCM, Dokta John Magufuli akiwa na watoto ambao aliwapatia zawadi alipokuwa akiondoka baada ya kujinadi katika Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma.