Wednesday, October 28, 2015

BREAKING NEWS: UCHAGUZI ZANZIBAR WAFUTWA KUTOKANA NA VIKWAZO MBALIMBALI

Na Mwandishi wetu,

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha ametangaza kufutwa kwa uchaguzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mpaka hapo itakapotangazwa tena.

Taarifa kamili hii hapa; 




MEYA MANISPAA YA SONGEA ASHINDWA KUTETEA KITI CHAKE



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

ALIYEKUWA Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Charles Mhagama katika kipindi kilichopita ameshindwa kutetea kiti chake cha udiwani kata ya Matogoro kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Manispaa hiyo, baada ya mgombea udiwani wa kata hiyo kutoka Chama cha Wananchi (CUF) Alawi Kawelea, kuibuka mshindi.

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Songea, Raphael Kimari alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake alisema CCM kimefanikiwa kushinda kata 16, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeshinda kata 4 na CUF kimeshinda kata 1 ambapo jimbo hilo lina jumla ya kata 21.

Charles Mhagama.
Kimari aliwataja washindi wa Chama Cha Mapinduzi na kata zao kwenye mabano, kuwa ni Oddo Mbunda (Mjimwema), Festo Mlelwa (Seedfarm), Mshawej Hassan (Subira), Maurus Lungu (Mletele), Yobo Mapunda (Lilambo), Lotari Mbawala (Mshangano), Cresensia Kapinga (Ndilimalitembo) na Osmund Kapinga wa kutoka kata ya Mwengemshindo.

Aliwataja wengine kuwa ni Wilbart Mahundi (Ruhuwiko), Ismail Aziz (Misufini), Shaib Kitete (Mjini), Hussein Abukadi (Majengo), George Oddo (Lizaboni), Golden Sanga (Bombambili), Izack Lutengano (Msamala) na Mussa Mwakaja kata ya Mateka.

Tuesday, October 27, 2015

TUNDURU SONGEA CCM YAZIDI KUNG'ANG'ANIA MAJIMBO YAKE



Na Steven Augustino,
Ruvuma.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya ya Tunduru na Songea mkoani Ruvuma, kimeendelea kung’ang’ania majimbo yake na kata kwa ujumla baada ya wagombea wake kwa nafasi ya diwani, ubunge na rais kuongoza kwa kura nyingi.

Wakitangaza kwa nyakati tofauti wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo ya Tunduru Kusini, Kaskazini na Songea walisema kuwa wagombea wa chama hicho ndio walioibuka kidedea katika matokeo ya uchaguzi huo, uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Wilayani Tunduru msimamizi wa uchaguzi, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tinna Sekambo aliwatangaza Daimu Mpakate kupitia Chama Cha Mapinduzi kuwa mshindi wa nafasi ya ubunge, jimbo la Tunduru Kusini baada ya kupata kura 27,486.

Monday, October 26, 2015

MANYANYA AIBUKA KIDEDEA JIMBO LA NYASA

Injinia Stella Manyanya

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

TAARIFA zilizotufikia hivi punde Jimbo la Nyasa lililopo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kuongoza na kupeperusha bendera yake kwa nafasi ya kiti cha udiwani, ubunge na rais dhidi ya vyama vya upinzani.

Mkurugenzi msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Jabir Shekimweri amezungumza na mwandishi wa habari hizi na kueleza kwamba kwa nafasi ya udiwani, mpaka sasa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeweza kuchukua kata mbili kati ya 18 zilizopo wilayani humo na matokeo kwa ngazi hiyo ya udiwani, bado yanapokelewa kutoka katika kata mbalimbali.

Alisema jimbo la Nyasa lina idadi ya wapiga kura 70,766 na kwamba waliojitokeza kupiga kura walikuwa 45,838.

CCM MBINGA YAIBUKA KIDEDEA MATOKEO YA UCHAGUZI YATANGAZWA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kimeibuka kidedea baada ya wagombea wake kwa nafasi ya diwani, ubunge na rais kuongoza kwa kura nyingi katika vituo vyake vya kupigia kura.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa Jimbo la Mbinga mjini na vijijini uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu, huku wananchi ambao ni wapiga kura wakijitokeza kwa wingi kupiga kura katika vituo husika.

Matokeo yametangazwa leo majira ya mchana, katika kituo cha utafiti wa zao la kahawa TaCRI – Ugano kilichopo Mbinga mjini ambako Wakurugenzi wa Tume ya uchaguzi katika majimbo hayo, waliweka kambi huko wakifanya kazi ya kujumlisha matokeo ya wagombea.

Akitangaza matokeo kwa jimbo la Mbinga mjini, Mkurugenzi msimamizi wa uchaguzi Oscar Yapesa alisema kuwa jimbo hilo lina idadi ya wapiga kura 61,833 likiwa na kata 19 na vituo vya kupigia kura 165 na kwamba waliojitokeza kupiga kura walikuwa 42,706, kura halali 41,442.

UCHAGUZI JIMBO LA MBINGA MJINI NA VIJIJINI WAENDESHWA KWA AMANI NA UTULIVU MATOKEO KUTANGAZWA LEO



Na Kassian Nyandindi,

Ruvuma.

HALI ya uchaguzi katika Jimbo la Mbinga mjini na vijijini mkoani Ruvuma, limeendeshwa kwa amani na utulivu, huku wananchi ambao ni wapiga kura wakijitokeza kwa wingi kupiga kura.

Mwandishi wetu ambaye ametembelea katika maeneo mbalimbali ya vituo vya kupigia kura, ameshuhudia hali ikiwa shwari licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo wakati zoezi hilo linaendeshwa.

Changamoto hizo ni kwamba baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa, ambao wanadaiwa kutoka vyama vya upinzani, walikuwa wakionekana katika vituo wakifanya kampeni na kupiga kelele.

Hali hiyo imeshuhudiwa katika kata ya Mpepai na Mbangamao jimbo la Mbinga mjini, ambapo askari wa kikosi cha kutuliza ghasia, walikwenda huko na kufanikiwa kuzima kelele hizo.

Saturday, October 24, 2015

ASKARI MAGEREZA WAFARIKI BAADA YA KUPATA AJALI



Na Kassian Nandindi,
Songea.

ASKARI wawili wa Jeshi la magereza, gereza la mifugo la Majimaji lililopo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa wanasafiria kuacha njia na kupinduka.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela aliwataja askari hao waliopoteza maisha kuwa ni B 7303(Wader) Oscar Henry (29) na B 5361 CPL Geofrey Mwambigija (26) wote ni askari wa gereza hilo.

Alisema siku hiyo ya tukio, kwenye barabara inayotoka Tunduru kwenda Masasi pikipiki isiyofahamika namba za usajili ambayo ilikuwa ikiendeshwa na B 7303(Wader) Oscar Henry ikiwa kwenye mwendo kasi ilianguka na kusababisha vifo vyao.

WATAWANYWA KWA MABOMU YA MACHOZI BAADA YA KULETA VURUGU



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

KUNDI la watu linalodaiwa kuwa ni la wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limevamia eneo la soko la wakulima lililopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, na kung’oa kisha kuchana bendera 50 za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye thamani ya shilingi 200,000 kutokana na chuki za kisiasa zilizopo wilayani humo.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya asubuhi huko wilayani Mbinga.

Alifafanua kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio, kundi hilo lilikwenda kwenye eneo hilo na kufanya vurugu kisha kungo’a milingoti iliyowekwa bendera na kuzichana jambo ambalo lilisababisha kuwepo kwa vurugu kubwa kati ya wafuasi wa CHADEMA na wa CCM.

Friday, October 23, 2015

MWAMBUNGU: PIGENI KURA NA KURUDI NYUMBANI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

YAKIWA yamebaki masaa machache Watanzania kushiriki katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu, Serikali mkoani Ruvuma imewataka wananchi wake mkoani humo, Oktoba 25 mwaka huu kushiriki kikamilifu kupiga kura katika kituo husika walichojiandikisha na mara baada ya kukamilisha zoezi hilo, waondoke na kurudi nyumbani.

Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu alisema hayo leo alipokuwa akizungumza na madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la Yeboyebo, katika ukumbi wa Songea Club uliopo mjini hapa.

“Nawasihi sana, mkisha piga kura ondokeni katika eneo la kituo na kuwaacha mawakala wa vyama husika wakilinda kura zenu”, alisema Mwambungu.

TUNDURU KASKAZINI KUMCHAGUA MANJOLO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Tunduru Kaskazini wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameanzisha utaratibu wa kupita nyumba kwa nyumba ili kumsaidia kufanya kampeni mgombea ubunge, kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Manjolo Kambili ambaye anaungwa mkono na UKAWA.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutotajwa majina yao walisema, walisema kuwa maamuzi hayo wameyachukua baada ya kubaini kuwa mgombea ubunge aliyeteuliwa kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi, Mhandisi Ramo Makani  kuwa hawamtaki.

Walisema wamelazimika kuingia katika mapambano hayo, ili kuhakikisha kuwa mgombea huyo wa CCM, anang'olewa kupitia Sanduku la kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Wednesday, October 21, 2015

AMTWANGA NA MCHI KICHWANI NA KUSABABISHA MAUAJI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kitongoji cha Makombe kijiji cha Milonde kata ya Matemanga wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Mohamed Mawazo (43) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma ya mauaji.

Taarifa za tukio hilo, zinasema kuwa  mtuhumiwa huyo anashikiliwa akidaiwa kumuua Zuberi Issa kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa mtuhumiwa huyo ambaye alimpiga kwa kutumia mchi wa kutwangia, kutokana na wivu wa kimapenzi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mtuhumiwa huyo alifanya kosa hilo kwa kumtwanga nao kichwani kitendo ambacho kilimsababishia kufikwa na mauti.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 16 mwaka huu.

Alisema baada ya mtuhumiwa huyo kufanya shambulizi hilo, alikwenda kuripoti kwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Makombe, Said Mussa huku akitamba kuwa tayari amekwisha mpiga mtu aliyekuwa anamtuhumu kwamba anatembea na mke wake, ambaye ni miongoni mwa wake zake watatu.

ASKARI WAASWA KUTOTUMIA NGUVU WAKATI WA UCHAGUZI

Na Steven Augustino,

Tunduru.

ASKARI ambao watashiriki katika jukumu la kulinda amani na utulivu, siku utakapofanyika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu, wametakiwa kupunguza matumizi ya nguvu zisizokuwa za lazima katika uchaguzi huo.

Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Nicolaus Mwakasanga alisema hayo alipokuwa akifungua juzi mafunzo elekezi yaliyoshirikisha askari polisi, magereza, uhamiaji na mgambo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Hospitali ya wilaya hiyo mjini hapa.

Mwakasanga alisema kuwa lengo la mafunzo hayo, ni kuweza kufanikisha na kuhakikisha kwamba uchaguzi huo unakwenda salama.

Tuesday, October 20, 2015

WAUGUZI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YAO



Na Muhidin Amri,
Songea.

MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma, Sixbert Kaijage amewataka Wauguzi wanaofanya kazi ndani ya halmashauri hiyo kujituma na  kutekeleza majukumu ya kazi zao ipasavyo, ili waweze kuboresha huduma husika kwa jamii, jambo ambalo litawafanya waweze kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia wilaya hiyo, kusonga mbele kimaendeleo kwa haraka zaidi, na wananchi kufanya shughuli zao wakiwa na afya nzuri.

Kaijage alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa katika kijiji cha Lundusi, mji mdogo wa Peramiho, wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Maposeni wilayani humo kuhusiana na  serikali ilivyojipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali,  za kiutendaji kwa watumishi wa halmashauri hiyo.

Saturday, October 17, 2015

MAMIA WAMUAGA MBUNGE DEO FILIKUNJOMBE NYUMBANI KWAKE KIJICHI DAR ES SALAAM

 Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, Deogratias Filikunjombe wakati wa ibada ya kuuaga iliyofanyika nyumbani kwake Kijichi Dar es Salaam leo mchana.
 
 Majeneza yenye miili ya aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, Deogratias Filikunjombe na ndugu zake, Plasdus Ngabuma na Casablanga Haule yakiwa yamewekwa mbele wakati wa ibada ya kuiombea iliyofanyika nyumbani kwa mbunge huyo Kijichi Dar es Salaam leo, kabla ya kusafirishwa kwenda Ludewa kwa mazishi.
 
 Mjane wa Deo Filikunjombe, Sarah (katikati) akisaidiwa na jamaa zake wakati wa ibada hiyo.
 
 Waombolezaji wakiwa kwenye ibada hiyo.
 
 Padri Maxmillian Wambura, kutoka Parokia ya Mtakatifu Wote Kiluvya akiyamwagia mafuta ya baraka majeneza hayo.
 
 Waombolezaji wakiwa katika ibada hiyo.
 
 Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza la Plasdus Haule.
 

  Familia ya Filikunjombe ikiwa katika ibada hiyo.
 
 Waombolezaji wakiwa kwenye ibada hiyo.
 
Nyumba ya Filikunjombe ambayo inadaiwa amekaa wiki mbili tangu ahamie baada ya kukamilika ujenzi wake 'Hakika tumuache mungu aitwe mungu"
(Imeandaliwa na mtandao wa habari za jamii.com)

Friday, October 16, 2015

TUNDURU WAISHUKURU SERIKALI AWAMU YA NNE



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANUFAIKA katika mradi wa uhawilishaji fedha, kaya maskini wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ambao unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) awamu ya tatu, wameishukuru serikali ya awamu ya nne kwa kubuni na kuwapelekea mradi huo.

Aidha wanufaika hao, wametaja baadhi ya miradi ambayo wameianzisha na kuanza kuwaletea maendeleo katika maisha yao baada ya kupokea fedha kutoka TASAF kuwa ni ufugaji wa mbuzi, kondoo, kuku, kanga, bata, matibabu pamoja na kununua vifaa vya ujenzi wa nyumba zao.

Wananchi hao walitoa shukrani hizo, walipokuwa kwenye mahojiano maalum na mwandishi wetu ambaye alitembelea vijiji vya Mbesa, Nalasi, Mchoteka, Tunduru mjini  na Namasakata wilayani humo.

BREAKING NEWS: MGOMBEA UBUNGE DEO FILIKUNJOMBE AFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA CHOPA

Mbunge wa Ludewa mkoani Njombe, Deo Filikunjombe aliyevaa shati la kijani enzi ya uhai wake akishiriki na wananchi wake katika shughuli mbalimbali za maendeleo Jimbo la Ludewa.
HABARI ZILIZOTUFIKIA HIVI PUNDE:

ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Ludewa mkoani Njombe na mgombea wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Deo Filikunjombe (Pichani) amefariki dunia wakati akielekea kwenye jimbo lake akitokea jijini Dar es Salaam, akiwa kwenye Chopa iliyoanguka jana katika hifadhi ya wanyama ya Selous iliyopo mkoani Morogoro. 

Jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, na kwamba hakuna mtu aliyepona katika ajali hiyo.

Thursday, October 15, 2015

WATAKIWA KUTUNZA SHAHADA ZAO ZA KUPIGIA KURA

Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

MGOMBEA nafasi ya ubunge Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhandisi Edwin Ngonyani, amewakumbusha wananchi wa jimbo hilo, kutunza shahada zao za kupigia kura na kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.

Aidha amewataka kuwakataa wagombea wanaotumia kiasi kikubwa cha fedha kuwahonga wapiga kura, ili waweze kuwachagua katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Ngonyani alisema kitendo hicho ni cha aibu na fedheha, hivyo kiongozi anayepatikana kwa mfumo huo akishachaguliwa hushindwa kutimiza ahadi alizotoa kwa wananchi wake, badala yake hutumia nafasi yake aliyonayo kuliingiza Taifa kwenye matatizo makubwa na kuwafanya wananchi anaowaongoza kuwa maskini.

UWT RUVUMA YA WAASA WANACHAMA WAKE

Na Muhidin Amri,
Songea.

KATIBU wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani Ruvuma, Chiku Masanja amewataka wanawake wa mkoa huo, kuwaunga mkono  wanawake wenzao waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho.

Alisema wanawake wakipata nafasi za uongozi, itakuwa rahisi kwao kuwatetea wanawake wenzao katika vikao mbalimbali vya maamuzi hasa vile vya baraza la madiwani, ubunge na kupata fursa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli ambazo  zitawawezesha wajikwamue kiuchumi.

Chiku aliyasema hayo jana, wakati  alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya wanawake, kata ya Misufini Manispaa ya Songea mkoani humo kwenye ukumbi wa CCM tawi la mjini, kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya umoja wao sambamba na kuwakumbusha juu ya wajibu wa kila mwanamke kushiriki kikamilifu kupiga kura katika uchaguzi mkuu, Oktoba 25 mwaka huu katika eneo lake analoishi.

Tuesday, October 13, 2015

MARTIN MSUHA CHAGUO LA WANAMBINGA VIJIJINI APANIA KUWALETEA MAENDELEO WANANCHI WAKE

Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dokta John Magufuli akionesha ilani ya uchaguzi ya CCM, kabla ya kumkabidhi mgombea ubunge Jimbo la Mbinga vijijini, Martin Msuha wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika hivi karibuni mjini hapa.
 Na Kassian Nyandindi,

OKTOBA 25 mwaka huu, ni siku maalum ambayo Watanzania wataweka historia kubwa ya kuwachagua viongozi wao watakaoweza kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ambao ni diwani, mbunge na rais kwa kuvihusisha vyama mbalimbali vya siasa ambavyo vimesajiliwa kisheria hapa nchini.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni chama ambacho kimeendelea kuiongoza nchi hii, baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2010, ambapo uchaguzi huo ulivishirikisha vyama vya upinzani au vyama rafiki kama inavyoelezwa na baadhi ya makada wa chama.

Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini, Julai 2 mwaka 1992, CCM ni chama ambacho Watanzania wengi wanakiamini na kukichagua kiendelee kushika dola kwa miaka mingi sasa.

Watanzania hao katika vipindi vyote vya chaguzi zilizopita, waliamua kwa dhati kuwachagua wagombea waliotokana na chama hicho baada ya kuridhishwa na sera zake, ambazo zinalenga kuwaletea maendeleo.

Katika makala haya Mwandishi wetu, anapenda kuelezea juu ya nafasi ya Ubunge ni moja kati ya nafasi nyeti ambayo wananchi watakuwa na haki ya kuchagua kama vile katiba ya nchi yetu inavyotaka, ambapo wakati ukifika upigaji wa kura utafanyika katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi na kupatikana kiongozi ambaye atawaongoza wananchi wake katika eneo husika.

CUF TUNDURU YALAANI KUCHANWA MABANGO YA MGOMBEA WAKE

Na Steven Augustino,
Tunduru.

CHAMA cha Wananchi  (CUF) wilaya ya  Tunduru mkoani Ruvuma, kimelaani vikali kitendo  cha kuchanwa mabango  ya mgombea wake wa udiwani kata ya Mlingoti Mashariki, Mohamed Nyoni.

Kwa mujibu wa taarifa za tukio hilo, zinaeleza kuwa zaidi ya mabango 300 yamechanwa na vijana wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba mabango hayo, yalikuwa yamebandikwa katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.

Sambamba na kuchanwa kwa mabango hayo, pia taarifa hizo zinasema kuwa watu hao walichana mabango ya mgombea  wao wa ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini, anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) Manjolo Kambili.

MGOMBEA UBUNGE TUNDURU KUSINI AFANANISHWA NA JEMBE


Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAPENZI na wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Tunduru Kusini mkoani Ruvuma, wamemfananisha mgombea ubunge wa jimbo hilo, Daimu Mpakate  kuwa ni sawa na jembe na pembejeo za kilimo, ambavyo wamekuwa wakivitabikia kwa muda mrefu jimboni mwao.

Wananchi wenye  bendera za chama hicho, walikuwa na mabango yenye kubeba ujumbe  wa aina mbalimbali ambao ulikuwa ukimuunga mkono mgombea huyo, huku  wakiimba  nyimbo za kumpongeza kuchaguliwa kwake, kuwa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya chama hicho.

Hayo yalibainishwa kwa vitendo kutokana na wananchi hao, pale walipojitokeza kwa wingi huku wakiwa wameinua mabango hayo ambayo yalikuwa na ujumbe wakumpa moyo mgombea, kwamba watamchagua kwa kumpatia kura zaidi ya asilimia zaidi ya 80.

NALICHO: JENGENI UWEZO KWA WATUMISHI WAJIENDELEZE KIMASOMO

Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

SERIKALI wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, imeziagiza idara na taasisi za serikali wilayani humo, kuhakikisha zinawajengea uwezo watumishi wao   kwa kuwapatia nafasi ya kwenda kujiendeleza kimasomo, ili kupunguza tatizo sugu la wataalamu wa kada mbalimbali ikiwa ni lengo la kuongeza ufanisi mahali pa kazi.

Mbali na hilo, wakuu wa idara husika wametakiwa kuwasimamia na kufuatilia kwa karibu watumishi wazembe ambao wanafanya kazi zao kwa mazoea, kitendo ambacho kinasababisha  kutokea malalamiko ya hapa na pale kutoka kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho alipokuwa akizungumza na wakuu wake wa idara katika Halmashauri hiyo na kukemea tabia ya baadhi ya watumishi, kukwamisha kwa makusudi mipango mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kwa manufaa ya jamii.

TASAF NAMTUMBO YASEMA BAADHI YA WANASIASA WANAPOTOSHA WANANCHI

Na Muhidin Amri,
Ruvuma.

OFISA ushauri na ufuatiliaji, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) hapa nchini wilaya ya  Namtumbo   mkoani Ruvuma,  Edson  Kagaruki  amekanusha  taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wilayani humo, kwamba mfuko huo unafanya kazi ya kuhawilisha fedha kwenda kaya maskini, kwa lengo la kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kiweze kushinda katika uchaguzi mkuu utakaofanyika, Oktoba 25 mwaka huu.

Kufuatia maneno hayo, Ofisa huyo wa TASAF  wilayani humo amewataka wanasiasa hao kuacha porojo  hizo na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali, katika kupambana na umaskini hapa nchini.

Aidha amewakumbusha kutumia majukwaa ya kisiasa, kueleza sera zao na sio kuwapotosha wananchi kwa mambo ambayo hayana msingi, jambo ambalo linaweza kuchochea uhasama katika jamii.

Monday, October 12, 2015

VITUO 216 JIMBO LA PERAMIHO KUTUMIKA KUPIGIA KURA

Mlemavu asiyeeona akisoma mfano wa karatasi ya kupigia kura, wakati wa mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Watu wenye ulemavu.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JUMLA ya vituo 216 vimetengwa katika jimbo la Peramiho, lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kwa ajili ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba, 25 mwaka huu.

Akizungumza na mwandishi wetu, kwa niaba ya msimamizi mkuu wa uchaguzi wa jimbo hilo Sixbert Valentine, Ofisa uchaguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Furaha Mwangakala, alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo yamekamilika.

Mwangakala alifafanua kuwa katika kila kituo ndani ya Jimbo hilo, kutakuwa na wapiga kura 450 kwa lengo la kupunguza msongamano na kutoa fursa kwa wananchi wote ambao wamejiandikisha, waweze kupiga kura bila kupata usumbufu wa aina yoyote ile.

Alisema kuwa, kufuatia zoezi hilo jumla ya watu 67,334 kwa Jimbo la Peramiho wenye sifa ya kupiga kura wamejiandikisha, miongoni mwao yakiwemo makundi mbalimbali ya wazee, vijana, wanawake kwa wanaume ili waweze kutumia haki yao ya msingi kuwachagua viongozi wao.

MANJORO KUMBWAGA RAMO TUNDURU KASKAZINI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAKATI kampeni za Uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika  Oktoba 25 mwaka huu zikiendelea kushika kasi sehemu mbalimbali hapa nchini, mgombea ubunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) na Umoja wa Katiba ya Wananchi  (UKAWA) Manjoro Kambili, amesema ataendelea kujiwekea mikakati ya kuhakikisha kwamba anajipatia ushindi mnono na kujinyakulia jimbo hilo, ili aweze kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Jimbo hilo kwa sasa mgombea huyo, anapambana na Mhandisi Ramo Makani ambaye anapeperusha bendera kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hayo yamebainika kufuatia uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, ambapo taarifa zinaonesha kuwa Kambili amechukua maamuzi hayo kutokana na kuwepo kwa mgogoro mkubwa miongoni mwa wanachama wa CCM ambao unafukuta chini kwa chini, huku kukiwa na kundi kubwa lililoanza kujitokeza na kumuunga mkono mgombea huyo wa UKAWA.

AUAWA NA TEMBO AKIWA SHAMBANI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja ambaye ni wa kijiji cha Kalulu, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Said Athuman (42) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na Tembo, wakati akiwa shambani kwake.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 29 mwaka huu, majira ya jioni baada ya kundi la Tembo kujitokeza na kumvamia.

Alifa Abdalah Said ambaye ni Kaka wa marehemu huyo, alisema chanzo cha tukio hilo kilitokana na maafisa wa idara ya wanyama pori ambao wanalinda wanyama katika kituo cha hifadhi Kalulu kilichopo kwenye hifadhi ya taifa ya Selous, walikuwa wakiwafukuza Tembo hao katika maeneo waliyokuwepo, ndipo walikimbilia shambani huko na kusababisha mauaji.

MAMBO MAZURI TUNDURU WAIBUKA KIDEDEA

Na Steven  Augustino,
Tunduru.

TIMU ya soka, Mambo Mazuri FC ya Tunduru mjini mkoani Ruvuma, imeibuka kidedea kupitia ligi ya Polisi Jamii, baada ya kuwafunga  mahasimu wao, Vampire FC magoli manne kwa matatu katika mchezo mkali, uliorindima kwenye uwanja wa Chama Cha Mapinduzi mjini hapa.

Kutokana na matokeo hayo, Vampire FC imeambulia nafasi ya pili na mshindi wa tatu katika mashindano hayo ikachukuliwa na Jobe FC.

Kulingana na maelekezo yaliyotolewa na Mratibu wa mashindano hayo,  Inspector Songelael Jwagu mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atazawadiwa kikombe, seti moja ya jezi na mpira mmoja wa miguu.

Friday, October 9, 2015

DED TUNDURU ACHUKIZWA WANANCHI KUUZIWA MAENEO YA MAKABURI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imewataka wananchi wake kuzingatia taratibu husika, hasa pale wanapohitaji kununua maeneo ya viwanja kwa ajili ya kujenga nyumba au kuweka makazi yao ya kudumu.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Tinna Sekambo alitoa rai hiyo Ofisini kwake alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu, na akatumia nafasi hiyo kuwataka kutoa ushirikiano pale wanapoona wanatapeliwa na wajanja wachache ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Sekambo alifafanu kuwa, tahadhali hiyo ameitoa kufuatia kuwepo kwa taarifa za kuibuka kwa kundi la matapeli wilayani humo, ambao wamekuwa wakiwauzia watu viwanja na kuwapatia hati bandia.

Alisema kufutia hali hiyo, Ofisi yake inafanya uchunguzi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuweza kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria haraka iwezekanavyo, kabla ya wananchi hawajapata hasara kubwa.

POLISI WATOA ONYO SIKU YA UCHAGUZI MKUU

Na Muhidin Amri,
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limesema kwamba, halitakuwa tayari kuona amani na utulivu vikivurugwa hasa katika kipindi hiki cha kampeni na kuelekea siku ya kupiga kura, kutokana na sababu za itikadi za kisiasa.

Kauli  hiyo  imetolewa jana na Kaimu Kamanda wa  Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na hali ya usalama ya wananchi, kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 25 mwaka huu.

Malimi alisema Jeshi hilo limejiandaa vya kutosha kuhakikisha kwamba, uchaguzi wa mwaka huu unaendeshwa kwa amani na utulivu, katika maeneo mbalimbali mkoani humo mpaka siku ya mwisho ya upigaji  kura.

Tuesday, October 6, 2015

PICHA YA WIKI: MKUU WA WILAYA MBINGA AKIFURAHIA TEKINOLOJIA YA MAJIKO SANIFU YA KUPIKIA

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga akijaribu kupika chakula kwa kutumia jiko sanifu lililotengenezwa na kampuni ya RTE IMPROVED STOVED TANZANIA LIMITED, ambayo hutumia kiasi kidogo cha kuni na kuelezwa kuwa kama jamii itahamasishwa kuyatumia itasaidia kupunguza matumizi ya mkaa na kuni. Katikati ni mkurugenzi wa kampuni hiyo, David Nzimba.

POLISI NA JWTZ WAFANIKIWA KUHARIBU MABOMU MAWILI

Na Mwandishi wetu,
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wamefanikiwa kuharibu mabomu  mawili, yaliyokutwa katika Kijiji cha Ngwinde kata ya Litola, wilayani Namtumbo mkoani humo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocutus Malimi alisema kuwa mabomu hayo yaliharibiwa ili yasiweze kuleta madhara katika jamii, ambapo moja liliharibiwa majira ya saa nne asubuhi na la pili saa sita mchana.

Alisema kuwa katika mabomu hayo, moja lilikuwa aina ya Motor lenye ukubwa wa mm. 82 ambalo lilikutwa chini ya mti na la pili ni  la kurusha kwa Roketi (RPG) lenye ukubwa wa mm. 122 ambalo lilichimbiwa chini ya ardhi.

WASHIKILIWA KWA KOSA LA KUJIANDIKISHA MARA MBILI KATIKA BVR

Revocatus Malimi, kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma. 
Na Muhidin Amri,
Ruvuma.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linawashikilia watu 18 kwa  kosa la kujiandikisha zaidi ya mara mbili katika daftari la kudumu la wapiga kura,  kwa njia ya kielektroniki (BVR).

Kukamatwa kwa watu hao, kumetokana na ushirikiano kati ya Jeshi hilo na taasisi nyingine zinazohusika na uandikishaji huo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocutus Malimi alisema kwamba watu hao wamekamatwa kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo, hata hivyo bado wanaendelea kuwatafuta wengine ambao wanadaiwa nao kujiandikisha zaidi ya mara moja katika daftari hilo.

Sunday, October 4, 2015

WANAFUNZI SEKONDARI AGUSTIVO MBINGA WAFUNDWA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANAFUNZI wanaohitimu masomo ya kidato cha nne wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa kutojiingiza kwenye masuala ya anasa kama vile vitendo vya kimapenzi, ambavyo husababisha kukatisha ndoto ya kujiendeleza kimasomo katika maisha yao.

Aidha wakati wote wametakiwa kuonesha dhamira ya kusonga mbele, kwa kujikita zaidi kwenye malengo ya kuongeza elimu kwa faida ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Ushauri huo ulitolewa jana na Khalid Kingi, ambaye ni Katibu msaidizi wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) katika mahafali ya kidato cha nne shule ya sekondari Agustivo iliyopo mjini hapa, ambapo katika sherehe hizo alikuwa akimwakilisha mgeni rasmi Katibu Mkuu UVCCM Taifa, Sixtus Mapunda.

“Ndugu zangu mnahitimu masomo yenu katika kipindi ambacho kina changamoto nyingi, natoa wito kwenu na kwa wengine hapa wilayani ambao wanahitimu kidato cha nne kama ninyi, huko muendako mkapambane na changamoto za ulimwengu huu kwa kuweka malengo ya kuongeza elimu, na kuacha tabia ya kufikiria maisha ya mtaani ambayo yatawafanya mwisho wa siku mjiingize kwenye makundi mabaya”, alisema Kingi.

MGOMBEA URAIS ACT ASEMA MAENDELEO YALIYOPO YANATOKANA NA JITIHADA ZA VYAMA VYA UPINZANI

Anna Mghwira mgombea urais kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, akiwa katika moja ya mikutano yake ya kampeni hapa nchini. 
Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANANCHI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa kufanya mabadiliko kwa kuchagua wagombea kutoka vyama vya upinzani ifikapo Oktoba 25 mwaka huu, ili waweze kuwaletea maendeleo yenye kasi ya ajabu kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Mgombea urais, Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, Anna Mghwira alisema hayo alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi ambao walijitokeza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Baraza la Idd mjini hapa.

Aidha mgombea huyo alipokuwa akizungumza na wananchi hao, aliahidi kuunda serikali ya umoja wa kitaifa akidai kwamba lengo lake kuondoa chokochoko zilizopo, na mitafaruku ambayo baadaye inaweza kuleta mapigano (Vita) miongoni mwa jamii.

UHAMIAJI RUVUMA WATOA ONYO

Na Mwandishi wetu,
Songea.

IDARA ya uhamiaji   mkoa wa Ruvuma, imewaonya watu wasiokuwa raia wa Tanzania kutojihusisha kwa namna yoyote ile katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, na endapo watafanya hivyo watakuwa wamekiuka sheria za nchi.

Mbali na hilo imeelezwa kuwa kushiriki katika uchaguzi huo kwa mtu asiyekuwa raia wa Tanzania, kunaweza kusababisha taifa kupata viongozi wabovu wasiokuwa na uchungu wa kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Ofisa uhamiaji wa mkoa huo, Hilgaty Shauri alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari mjini songea.

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA SEKTA YA AFYA

Na Muhidin Amri,
Namatumbo.

SERIKALI imesema, itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa  nyumba za wauguzi, madaktari na kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuwavutia  watumishi wa idara  ya afya, kupenda kufanya kazi wakiwa katika mazingira mazuri na waweze kutekeleza majukumu ya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa uchaguzi kwa viongozi wa chama cha wauguzi mkoani humo, uliofanyika kwenye ukumbi wa Faraja uliopo mjini hapa.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho.
Alifafanua kuwa serikali inatambua matatizo yanayowakabili wafanyakazi wa idara hiyo, ambapo itaendelea kuboresha mazingira yao ikiwemo pia mishahara na maeneo ya kufanyia kazi zao.

Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa bado serikali inaendelea kuajiri watumishi wengi mwaka hadi mwaka, sambamba na ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na hospitali ili kukidhi mahitaji husika ya watanzania kwa kila  mkoa, wilaya, kata na vijiji ikiwa ni lengo kwamba wananchi wake waweze kupata huduma ya matibabu kwa urahisi.

NGAGA: MWALIMU ATAKAYEKUWA MTOVU WA NIDHAMU ATACHUKULIWA HATUA

Na Muhidin Amri,
Ruvuma.

WALIMU  nchini wametakiwa kukataa kugeuzwa wapiga debe na kuwa madalali wa  vyama vya  siasa, badala yake wazingatie majukumu yao ya kazi kwa kuongeza juhudi ya ufundishaji watoto darasani, hatua ambayo itasaidia kuwaongezea uelewa wanafunzi na kukuza taaluma hapa nchini.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi ngaga alisema hayo, mwishoni mwa wiki alipokuwa akifungua kikao cha siku tatu kwa wakuu wa shule za sekondari kutoka mikoa mitatu ya nyanda za juu kusini Ruvuma, Njombe na Iringa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa katoliki uliopo mjini hapa.

Mbali na hilo, pia amewaonya walimu hao kutotumia maeneo ya shule kufanyia kampeni wanasiasa kwa sababu maeneo hayo, sio rasmi kwa ajili ya shughuli hizo huku akisisitiza kwamba tabia hiyo inawanyima fursa watoto, kupata haki yao ya msingi.

HII NI KERO NA AIBU KWA MANISPAA YA SONGEA

Uchafu ukiwa umefurika na kusambaa kwenye ghuba karibu na Soko kuu la Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na kusababisha kero kubwa kwa wapita njia, kutokana na taka hizo kutoa harufu mbaya. Kwa ujumla Manispaa hiyo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu sasa na wananchi wake, kwa kushindwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya mji huo. (Picha na Muhidin Amri)

Friday, October 2, 2015

MWANAFUNZI SHULE YA MSINGI MAHELA MBINGA AOMBA MSAADA AKATIBIWE INDIA

MAELEZO YA PICHA HII:

Huyu ni mtoto Yasin Ngonyani mwenye umri wa miaka 13, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Mahela wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, anaomba msaada wa kuweza kufanikiwa kwenda nchini India kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya oparesheni ya mguu wake ambao unamsumbua kwa muda mrefu sasa.

Kwa mujibu wa Madaktari ambao wamemfanyia uchunguzi wa awali, gharama za matibabu yake ni shilingi milioni 17, hivyo yeyote atakayeguswa na tatizo hilo ambaye yupo tayari kumsaidia kuweza kufanikisha matibabu ya mguu huo, anaweza kuwasiliana na mzazi wake kwa simu namba; 0763 - 770387 au 07 - 12345831.

Hata hivyo kwa mawasiliano zaidi unaweza kupiga simu namba; 0754 - 236443 kwa Ofisa ustawi jamii, Davina Maketa hapa wilayani Mbinga ambaye ndiye anafuatilia kwa karibu na kushughulikia matibabu ya mtoto huyo.

KUTOA NI MOYO SIO UTAJIRI !!