Tuesday, February 28, 2017

GOMBO SAMANDITO AWAKEMEA WALIMU WATORO KAZINI ASISITIZA ATAKAYEKAMATWA ATAMFUKUZA KAZI

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

WALIMU wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi zao ikiwemo kuacha vitendo vya ulevi na utoro kazini.

Aidha wamesisitizwa kuwahi na kuwa katika mazingira ya kazi wakati wote na kufuata taratibu za kazi zao kwa mujibu wa nafasi walizonazo kazini.

Gombo Samandito.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Gombo Samandito wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha tathimini ya maendeleo ya elimu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga mjini hapa.

“Walimu mnatabia ya kuwa watoro kazini natambua mnajua kwamba zikipita siku tano haupo kazini nakufukuza kazi, wakati wa kazi fanyeni kazi zenu kwa kutekeleza ipasavyo majukumu mliyopewa mkayasimamie haya vizuri msiwe sehemu ya matatizo”, alisisitiza Samandito.


Samandito alisisitiza pia kwa atakayepuuza maagizo yake hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufukuzwa kazi huku akiongeza kuwa adui mkubwa wa maendeleo katika maisha ya kila siku ya binadamu ni tabia ya mtu husika hivyo walimu hao wanapaswa kujiangalia kwanza wenyewe na kubadilika mara moja kuwa na tabia nzuri kazini.

Monday, February 27, 2017

MAGHEMBE ASHANGAZWA NA UTAJIRI WA VIVUTIO VYA UTALII ZIWA NYASA

Wageni mbalimbali wakiwa katika eneo la viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Vita vya Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameshangazwa na utajiri wa vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa wa Ruvuma, wakiwemo aina ya samaki wa mapambo zaidi ya 400 katika ziwa Nyasa mkoani humo na viumbe wengine adimu waliopo katika ziwa hilo.

Kwa ujumla viumbe hao licha ya kuwa ni adimu pia wamekuwa hawapatikani sehemu yoyote ile hapa duniani.

Profesa Maghembe alishangazwa na hayo wakati alipokuwa akizungumza katika sherehe za kumbukizi ya miaka 110 ya Vita vya Majimaji, zilizofanyika kwenye viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea mkoani hapa.

Alisisitiza kuwa ni fursa pekee sasa, kuendelea kutangaza vivutio hivyo ili viweze kuleta tija kwa Taifa hili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho wakiwemo Wananyasa na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

MANISPAA SONGEA YAGAWA MICHE YA MATUNDA BURE KWA WATUMISHI WAKE

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

KATIKA kuhakikisha kwamba mazingira yanaendelea kuboreshwa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, idara ya kilimo katika Manispaa hiyo imegawa bure miche bora ya matunda kwa watumishi wake wa idara mbalimbali.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa uongozi wa Manispaa umefanya hivyo kwa lengo la kuwajenga watumishi wake, kuwa na tabia ya mara kwa mara kupenda kupanda miti ya matunda na miti mingine ya aina mbalimbali ili kusaidia kuhifadhi mazingira na watu kuweza kupata matunda.

Midelo alifafanua kuwa Manispaa ya Songea, imenunua miche bora ya matunda 2000 yenye thamani ya shilingi milioni 5,000,000 kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA).

VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA WATAKIWA KUJENGA USHIRIKIANO

Na Dustan Ndunguru,     
Mbinga.

MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Ambrose Nchimbi  amewataka viongozi wa kisiasa na watendaji katika maeneo mbalimbali wilayani humo, kujenga ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao na kuacha kuendekeza malumbano badala yake wasimamie vyema ujenzi wa miradi ya wananchi ili iweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.

Akizungumza na mwandishi wetu, Nchimbi alisema kuwa baadhi ya maeneo wilayani humo miradi ya wananchi ya maendeleo imekwama haijakamilika kwa wakati uliopangwa kutokana na tabia ya viongozi kuendekeza malumbano hasa yanayochochewa na viongozi wa vyama vya siasa.

Alivinyoshea kidole vyama vya upinzani kutokana na tabia ya viongozi wake kuwakatisha tamaa wananchi kwa kuwadanganya kuwa serikali imewasahau kitu ambacho sio cha kweli.

Sunday, February 26, 2017

MWALIMU SHULE YA SEKONDARI KIAMILI MBINGA ATAFUTWA NA POLISI KWA KUMSHAMBULIA MWANDISHI WA HABARI

Na Mwandishi wetu,      
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamtafuta Mwalimu wa shule ya sekondari Kiamili wilaya ya Mbinga mkoani humo, Victor John Kayombo ambaye amekimbia hajulikani wapi alipo kwa kosa la kumshambulia mwandishi wa habari, kumpiga na kutaka kumjeruhi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizomfikia mwandishi wa habari hizi zinaeleza kwamba tukio hilo lilitokea Februari 24 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni katika mtaa wa Soko kuu Mbinga mjini.

Imefafanuliwa kuwa Kayombo alimshambulia mwandishi wa habari Kassian Nyandindi wa gazeti la Majira mkoani hapa, baada ya kumhoji masuala ya utoro kazini ambapo amekuwa akilalamikiwa kwa muda mrefu na Walimu wenzake wa sekondari hiyo kwamba, haudhurii ipasavyo vipindi vyake vya masomo darasani pale anapotakiwa kufundisha wanafunzi wa shule hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji.

Aidha imeelezwa kuwa tokea mwalimu huyo ahamie shuleni hapo Januari 11 mwaka 2016 akitokea shule ya sekondari Dokta Shein, iliyopo katika kata ya Mpepai halmashauri ya mji wa Mbinga amekuwa na tabia hiyo ya kutozingatia vipindi vya kufundisha watoto darasani.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mwalimu Kayombo amefunguliwa shauri hilo katika Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga, Jalada la uchunguzi lenye namba MBI/IR/286/2017 na baadaye aweze kufikishwa Mahakamani kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.

Awali kwa upande wake Nyandindi alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya hali hiyo alikiri kushambuliwa na mwalimu huyo ambapo alieleza kuwa ilitokana na kumhoji kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa Walimu wenzake shule ya sekondari Kiamili kwamba, haudhurii ipasavyo darasani hivyo walimu wenzake hulazimika kujitolea kufundisha masomo ambayo alipaswa yeye kuyafundisha shuleni hapo.

WANANCHI WAHAKIKISHIWA UJENZI WA DARAJA MTO KITURA

Na Dustan Ndunguru,     
Mbinga.

MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma Ambrose Nchimbi amewahakikishia wananchi wa kata ya Kitura wilayani humo kwamba halmashauri hiyo itajenga daraja la mto Kitura ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi wa kata hiyo, sambamba na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto zingine ambazo zimekuwa zikikwamisha shughuli za maendeleo ndani ya kata hiyo.

Mkurugenzi mtendaji Halmashauri wilaya Mbinga, Gombo Samandito.
Nchimbi alisema hayo juzi wakati wa majumuisho ya ziara yake ya Kamati ya uongozi na mipango ya halmashauri hiyo, ilipotembelea kata hiyo kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo ya wananchi ambapo Wajumbe waliweza kupata fursa ya kutembelea daraja la mto Kitura, zahanati, nyumba ya mganga, ofisi ya kata na kukagua ujenzi wa nyumba za walimu katika sekondari ya Kitura.

Alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi hiyo ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa nyakati tofauti wilayani humo, sambamba na kubaini changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba wananchi amewaasa kutoa ushirikiano wa karibu kwa kueleza ukweli hasa pale wanapobaini mradi unatekelezwa chini ya kiwango.

SONGEA WAPONGEZWA KWA KUKUZA TAALUMA ELIMU YA MSINGI NA SEKONDARI

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

POLOLET Kamando Mgema, ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma amewapongeza walimu wa shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Songea mkoani humo, kwa kufanya kazi nzuri ambayo imeleta mafanikio mazuri ya kukuza taaluma katika matokeo ya mitihani darasa la saba na kidato cha nne.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa pongezi hizo kwenye kikao cha tathimini ya elimu kwa mwaka wa 2015/2016 ambacho kiliwakutanisha Wadau mbalimbali wa elimu Waratibu elimu kata, Walimu wakuu wa shule za msingi, Wakuu wa shule za sekondari, Madiwani na Maofisa elimu ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana Songea.       

Pamoja na kuwapatia pongezi hizo, Mgema alikemea pia tabia zinazofanywa na baadhi ya walimu kuwa na utoro kazini ambapo amewataka waache mara moja vinginevyo kwa yule atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kufukuzwa kazi.

KITURA SEKONDARI HAINA MWALIMU WA HESABU NA FIZIKIA


Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

SHULE ya Sekondari Kitura iliyopo katika kata ya Kitura wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, haina mwalimu wa somo la Hisabati na Fizikia tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 jambo ambalo limekuwa likisababisha wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kutosoma kabisa masomo hayo muhimu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye.
Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Stanslaus Mapunda alisema hayo juzi wakati wa ziara ya Madiwani ambao ni Wajumbe wa Kamati ya uongozi na mipango ya halmashauri ya wilaya hiyo, iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake Ambrose Nchimbi.

Mapunda alisema kuwa licha ya kulifikisha tatizo hilo katika mamlaka husika kwa muda mrefu hakuna utekelezaji uliofanyika na kwamba mpaka sasa pia hakuna ufumbuzi uliofikiwa juu ya utatuzi wa tatizo hilo hivyo wanalazimika kufundisha masomo mengine tu jambo ambalo limekuwa likisababisha watoto hao kutopata fursa nzuri ya kujisomea.

Thursday, February 23, 2017

SERIKALI YATOA UFAFANUZI JUU YA KUWAFUNGIA VIBANDA WAFANYABIASHARA SOKO KUU SONGEA



Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

SERIKALI kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imetoa ufafanuzi juu ya hatua iliyochukua ya kuwafungia vibanda Wafanyabiashara wa Soko kuu Songea lililopo katika Manispaa hiyo kwamba, walifanya hivyo kutokana na wafanyabiashara hao kudaiwa shilingi milioni 150 za pango la vibanda vya biashara ambavyo wamepanga.

Ufafanuzi huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Songea, Pololet Kamando Mgema alipokuwa akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake katika ukumbi wa mikutano wa wilaya hiyo.

Mgema alifafanua kuwa soko hilo lilianzishwa mwaka 1938 na kwamba ulipofika mwaka 1996 halmashauri hiyo ililazimika kuwaruhusu wafanyabiashara kukarabati vibanda hivyo vya soko ambavyo walikuwa wakifanyia biashara zao.

Alisema kuwa kila mfanyabiashara kwa wakati huo alikuwa akilipa pango la shilingi 8,000 kwa mwezi ambapo kiasi hicho kilikuwa kikiendelea kulipwa mpaka Agosti 20 mwaka 2002 wakati soko hilo lilipoungua na kuteketea kwa moto.

Sunday, February 19, 2017

KAMATI YA UONGOZI NA MIPANGO YARIDHISHWA NA UJENZI NYUMBA ZA WALIMU KITURA SEKONDARI

Na Dustan Ndunguru,   
Mbinga.

WAJUMBE Kamati ya uongozi na mipango katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imepongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Kampuni ya Sinani Building Contactors katika kukamilisha ujenzi wa nyumba za walimu shule ya sekondari Kitura iliyopo wilayani humo, mradi ambao hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi milioni 168.7.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Ambrose Nchimbi alitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi huo iliyofanyika mwishoni mwa wiki ambapo alisema kwamba mradi huo hadi kukamilika kwake utasaidia kuondoa tatizo la walimu kukosa nyumba za kuishi na kuondokana na adha ya kupanga uraiani.

Nchimbi alisema kuwa mradi huo unagharimu fedha nyingi hivyo ni vyema ujenzi wake unapaswa kuwa wa viwango vinavyokubalika na kwamba kamwe halmashauri hiyo, haitawavumiliwa makandarasi ambao wamekuwa na tabia ya kuhujumu miradi ya maendeleo ya wananchi na kusababisha kuzua malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

WAJUMBE WA BODI MBINGA WALIMU SACCOS WASWEKWA RUMANDE WAKITUHUMIWA KUIBA MILIONI 540,704,572

Askari Polisi wa Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, akimuongoza mmoja kati ya watuhumiwa wa fedha za Mbinga Walimu SACCOS iliyopo wilayani humo, Edmund Hyera baada ya kuamriwa na Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani hapa, Biezel Malila wakamatwe jana kwenye mkutano maalumu wa Wanachama wa SACCOS hiyo uliofanyika mjini hapa ambapo inadaiwa kuwa yeye na watuhumiwa wenzake walishiriki kuiba shilingi milioni 540,704,572. (Picha na Muhidin Amri)
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

WAJUMBE wa bodi ya Kamati ya usimamizi Chama cha ushirika Mbinga Walimu SACCOS iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamekamatwa na kuwekwa mahabusu wakituhumiwa kuiba shilingi milioni 540,704,572 za wanachama wa chama hicho cha ushirika na kusababisha hasara kubwa kwa chama kushindwa kujiendesha kwa manufaa ya wanachama.

Aidha hatua hiyo ya kukamatwa kwa Wajumbe hao ilitolewa na Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo, Biezel Malila baada ya kusomwa taarifa ya ukaguzi juu ya mwenendo wa chama hicho cha ushirika ambayo ilibainisha wizi wa fedha hizo katika mkutano mkuu maalumu wa wanachama, uliofanyika Februari 18 mwaka huu kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

“Kwa masikitiko makubwa ndugu zangu wanachama mliohudhuria mkutano huu naomba niwaeleze kwamba mwenendo wa chama hiki sio mzuri unatia kichefuchefu, chama kina hali mbaya kina hati chafu ya ukaguzi kwa kuwa Wajumbe wa bodi hii wameshiriki kwa namna moja au nyingine kukiuka taratibu za uendeshaji wa chama hiki, hivyo wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria na taratibu husika za vifungu vya uendeshaji wa vyama vya ushirika”, alisema Malila.

Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma alifafanua kuwa fedha hizo ambazo Wajumbe hao wanadaiwa kuiba na kujinufaisha kwa matakwa yao binafsi zilitokana na baki ya mikopo shilingi milioni 174,915,794 hisa, akiba na amana shilingi milioni 363,873,778 na mikopo ambayo waliitengeneza bila kufuata taratibu husika walichota shilingi milioni 1,915,000.

WILAYA YA MBINGA MKOANI RUVUMA YAONGOZA KWA KILIMO CHA BANGI

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa katika mkoa wa Ruvuma wilaya ya Mbinga mkoani humo imekuwa ikiongoza kwa kilimo cha bangi, hivyo serikali itaendelea kupambana na watu wanaohusika na uzalishaji wa zao hilo kwa kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha Mahakamani.

Aidha wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano mara kwa mara kwa viongozi wa ngazi ya vijiji, kata hadi wilaya katika utoaji wa taarifa ni wapi kumekuwa na mashamba ambayo yamekuwa yakitumika kuzalisha zao hilo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Madiwani pamoja na wananchi kwenye kikao cha kujadili mapendekezo ya mpango wa bajeti ya maendeleo halmashauri ya mji wa Mbinga kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

Tuesday, February 14, 2017

WALIOCHUKUA MIKATABA SOKO KUU SONGEA WAANZA KUFUNGULIWA VIBANDA VYAO

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,  Abdul Hassan Mshaweji amesema kwamba tayari vibanda vya Soko kuu la Manispaa hiyo vimeanza kufunguliwa na kupewa wafanyabiashara ambao wametimiza masharti yaliyowekwa na Manispaa hiyo.

Pololet Mgema, Mkuu wa wilaya ya Songea.
Kufunguliwa kwa vibanda hivyo alieleza kuwa kunafuatia wafanyabiashara wa Soko hilo ambao baadhi yao wamekubali kuingia mkataba mpya na halmashauri hiyo na kulipia gharama ya pango katika kibanda husika.

Mshaweji alifafanua kuwa hadi mwishoni mwa wiki hii wanatarajia idadi kubwa ya vibanda vitakuwa vimefunguliwa, baada ya wafanyabiashara wengi kuhamasika kuchukua mikataba na kulipia kodi ya vyumba vilivyopo katika soko hilo. 

Alisisitiza kuwa Manispaa inatekeleza kwa vitendo maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kuhakikisha kwamba Soko kuu la Manispaa ya Songea linakuwa chanzo muhimu cha mapato kwa lengo la kukuza uchumi wa Manispaa hiyo.

NAMTUMBO WASAMBAZA MICHE BORA YA KAHAWA KWA WAKULIMA WAKE

Na Yeremias Ngerangera,       
Namtumbo.

HALMASHAURI ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imejiwekea mikakati ya usambazaji wa miche bora ya kahawa kwa wakulima wake ambapo tayari miche 33,333 imegawiwa kwa wakulima wanaoishi katika vijiji vya Litola, Namabengo na Lumecha wilayani humo katika msimu wa kilimo mwaka huu.

Aidha lengo la uzalishaji huo ni kuwafanya wakulima hao waweze kupanda zao hilo katika mashamba yao na baadaye waweze kujikwamua kiuchumi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Kaimu Ofisa kilimo wa wilaya hiyo, Aniceth Ndunguru alisema kwamba yeye ndiye aliyesimamia zoezi la ugawaji wa miche hiyo kwenye vijiji hivyo na kwamba halmashauri hiyo, katika bajeti yake ya mwaka 2016/2017 ilitenga kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kununulia miche hiyo ambayo wakulima hugawiwa bure hatimaye waweze kupanda katika mashamba yao.

Monday, February 13, 2017

AFISA KILIMO HALMASHAURI MJI WA MBINGA ADAIWA KUINGIA MITINI NA MBEGU ZA WAKULIMA WA TANGAWIZI

Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma.
Na Dustan Ndunguru,       
Mbinga.

MALALAMIKO yametolewa na baadhi ya Wananchi waishio katika kata ya Kihungu Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, dhidi ya Kaimu Ofisa kilimo wa halmashauri hiyo, Maganga Ngahy wakimshutumu kutokana na kitendo chake cha kuwapelekea mbegu pungufu za zao la Tangawizi wananchi wa kata hiyo, ambazo walipaswa kuzalisha katika mashamba yao katika msimu wa mwaka huu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti Wanachama wa kikundi cha JITUME waliopo katika kata hiyo walisema kuwa kabla ya kupelekewa mbegu hizo walielezwa kwamba wangepata kilo 500 za zao hilo, lakini cha kushangaza wamepewa kilo 400 tu huku kukiwa na upungufu wa kilo 100 jambo ambalo limewafanya washindwe kutimiza ndoto yao ya kupanda eneo lote walilotarajia kupanda Tangawizi hizo.

Walisema kuwa mbegu hizo za Tangawizi wanachotambua ni kwamba wamekopeshwa ili wakati wa mavuno utakapowadia wanapaswa kurejesha baadhi ya mbegu kwa wakulima wengine, ambapo wasiwasi wao walionao sasa ni kwamba kutokana na kupatiwa mbegu pungufu watashindwa kurejesha kiasi husika ipasavyo ukizingatia kwamba uongozi wa halmashauri hiyo unatambua wao wamepewa kilo zote miatano na sio vinginevyo.

MGOGORO SOKO KUU SONGEA WAFANYABIASHARA WAFUNGA SAFARI DODOMA KUMUONA WAZIRI MKUU

Na Mwandishi wetu,    
Songea.

WAFANYABIASHARA wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wametuma ujumbe wa wafanyabiashara wenzao watano na wazee watano kwenda Dodoma kumuona Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa lengo la kupeleka kilio chao baada ya Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema kudaiwa kuwafungia vibanda vyao vya biashara, tangu Februari 11 mwaka huu kwa madai kwamba wanadaiwa shilingi milioni 100 na halmashauri hiyo jambo ambalo wamekana na kueleza kuwa sio la kweli.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Masoko katika Manispaa ya Songea (UWABIMASO) Leonard Chiunga alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa dharura na wafanyabiashara hao, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Chama cha walimu Songea uliopo mjini hapa ambao ulihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania mkoa wa Ruvuma, Issaya Mwilamba.

Chiunga alisema kuwa tokea maduka hayo yalipofungwa wateja ambao wamekuwa wakienda kwa ajili ya kupata mahitaji kwenye maduka hayo wanashindwa kupata mahitaji husika, jambo ambalo limeonekana kuwa ni kero kubwa kwao hivyo wanaziomba mamlaka za juu zione umuhimu wa kuchukua hatua haraka kuyafungua ili hata wafanyabiashara hao nao wasiweze kupata hasara kutokana na kuyafunga huko.

WATANZANIA WASHAURIWA KUSHIRIKIANA NA MALAWI

Na Kassian Nyandindi,       
Songea.

WANANCHI wanaoishi katika mikoa inayopakana na nchi ya Malawi wamehimizwa kuona umuhimu wa kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini humo, ikiwemo kufanya biashara kwa njia ambazo ni halali ili waweze kuinua uchumi wao.

Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Hassan Bendeyeko alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alisisitiza kuwa wananchi wanaoishi katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Ruvuma wanayo fursa kubwa ya kuweza kufanya hivyo ili waweze kuondokana na umaskini.

Bendeyeko alisema kuwa hivi sasa ni wakati pekee wa kuchangamkia fursa hizo kwa kujenga ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na Malawi, jambo ambalo litaweza kuleta tija katika shughuli zao za kukuza uchumi wa kila siku.

Sunday, February 12, 2017

WANAFUNZI AMBAO HAWAJARIPOTI SHULE KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MAOFISA elimu katika Halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata wametakiwa kuhakikisha kwamba watoto wote waliochaguliwa kwenda shule kwa ajili ya kuanza kidato cha kwanza wanaripoti haraka katika shule husika, kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

Agizo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alipokuwa akizungumza na Madiwani, Maofisa elimu na Watendaji wa halmashauri hizo mjini hapa huku akieleza kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari mwaka huu mpaka sasa kwa shule hizo za sekondari jumla ya wanafunzi 120 hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa kwenda kusoma wilayani humo, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua ili kuweza kudhibiti hali hiyo isiweze kuendelea kuwepo na kujenga mazoea katika jamii.

“Naendelea kusisitiza kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanapaswa kwenda shuleni kusoma, nawataka maofisa elimu na watendaji wa vijiji na kata mshirikiane kumaliza tatizo hili mapema na ofisi yangu ipate taarifa haraka kwamba watoto hawa wapo shuleni wanasoma”, alisisitiza.

DC AWAPONGEZA MADIWANI MBINGA

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amewapongeza wajumbe wa kikao cha maridhiano ya kugawana mali kati ya pande mbili za halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga kwa kumaliza kikao hicho katika hali ya amani, utulivu na maelewano bila ya kuwepo kwa mgogoro, mvutano na malumbano.

Cosmas Nshenye.
Nshenye ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alitoa pongezi hizo juzi wakati alipokuwa akizungumza na Madiwani wa halmashauri hizo katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

Alisema kuwa kitendo hicho kimeonyesha utashi na ukomavu wa kifikra kwa kile alichoeleza kuwa kuna baadhi ya maeneo mengine wanapokuwa kwenye vikao kama hivyo, imekuwa ikizuka migogoro na malumbano ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi huku akisisitiza kuwa uhamisho wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga utafanyika mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa ofisi zao.

Akichangia hoja kwenye kikao hicho, Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbinga Kipwele Ndunguru alisema kuwa mapendekezo yaliyoridhiwa na kikao cha kamati ya ushauri ni kuhamisha bajeti ya shilingi bilioni 2.1 ambayo ilikuwa inatakiwa kujenga boma la halmashauri hiyo na kuzihamishia halmashauri ya wilaya ya Mbinga ambapo mpaka sasa kwa kuanzia kimetolewa kiasi cha shilingi milioni 500.

ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA YA KUMUUA MDOGO WAKE

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Omary Likande (32) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Msechela wilayani Tunduru mkoani humo, kwa tuhuma ya kumuua mdogo wake Unda Likande (23) kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali shingoni.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 7 mwaka huu majira ya mchana katika kitongoji cha Mkalala kilichopo katika kijiji cha Msechela tarafa ya Namasakata wilayani humo.

Mwombeji alisema kuwa siku hiyo ya tukio inadaiwa kuwa Unda aliuawa kwa kukatwa shingoni na kaka yake, Omary Likande wakati baba yao alipokuwa ametoka kwenda kutafuta chakula.

SITA WAJERUHIWA VIBAYA NA MMOJA AFARIKI DUNIA BAADA YA KUPIGWA NA RADI

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

WATU sita wanaoishi katika kitongoji cha Kifaguro kijiji cha Lituta wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wamejeruhiwa vibaya na mtu mmoja kufariki dunia baada ya kupigwa na radi kufuatia mvua kubwa ambayo iliambatana na upepo mkali, kuezua nyumba zenye kaya 37 na kusababisha kuharibika kwa mali mbalimbali zilizokuwemo ndani ya nyumba hizo.

Katika tukio hilo wakazi 79 wa kitongoji hicho pia wamekosa mahali pa kuishi ambapo habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 4 mwaka huu majira ya saa 9 alasiri.

Mwombeji alifafanua kuwa siku ya tukio hilo mvua hiyo iliambatana na upepo mkali na kusababisha kuezuliwa kwa nyumba hizo na vitu mbalimbali vilivyokuwemo ndani yake viliharibika ikiwemo vyakula ambapo thamani yake halisi bado haijajulikana.

Saturday, February 11, 2017

DC: VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA YA AFYA MBINGA KUMEKUWA NA TATIZO LA UKOSEFU WA DAWA

Sehemu ya watumishi wa halmashauri ya wilaya Mbinga, wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Cosmas Nshenye.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amesema kuwa katika wilaya hiyo kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ambayo amekuwa akiyapokea kwa nyakati tofauti kwamba katika vituo vya kutolea huduma za afya wilayani humo, kumekuwa na tatizo la ukosefu wa dawa jambo ambalo limekuwa ni kero kubwa kwa wananchi.

Aidha kufuatia hali hiyo amewataka watendaji waliopewa dhamana kusimamia kikamilifu majukumu yao ya kazi ikiwemo kujipanga ipasavyo katika kuhudumia wagonjwa wanaokwenda kutibiwa ili kuweza kuondoa malalamiko hayo yasiyokuwa ya lazima.

Nshenye alisema kuwa tatizo hilo linaanzia hospitali ya wilaya ambapo malalamiko juu ya ukosefu wa dawa yamekuwa yakitolewa na wananchi kwa muda mrefu na kwamba wamekuwa wakilazimika wakati mwingine kwenda kununua dawa hizo kwenye maduka ya dawa muhimu badala ya kupewa hospitalini hapo.

BARAZA LA MADIWANI MBINGA LAWAFUKUZA KAZI WATUMISHI WAKE

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma limewafukuza kazi baadhi ya watumishi wake, kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya utoro kazini na kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya shilingi milioni 46,680,000.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ambrose Nchimbi akitangaza jana kufukuzwa kazi kwa watumishi hao katika baraza hilo alisema kuwa wamefikia maamuzi hayo baada ya baraza hilo kuketi kama kamati kwa muda wa masaa matatu kujadili suala hilo na kufikia maamuzi hayo, ambayo alieleza kuwa yatakuwa fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia kama hiyo.

Nchimbi alisema kuwa waliofukuzwa kazi ni Mosta Ndunguru ambaye ni Afisa tabibu na Bapara Mwang'ombe Mhudumu wa afya ambapo wote kwa pamoja wamefukuzwa kwa makosa ya utoro kazini.

Wednesday, February 8, 2017

SAMANDITO: MPANGO WA BAJETI MBINGA UNALENGA KUBORESHA HUDUMA ZA KIJAMII NA KUKUZA UCHUMI KWA KUZINGATIA DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA KUWA NA VIWANDA VYA KATI

Aliyesimama ni Mkurugenzi mtendaji Halmashauri wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito akitoa ufafanuzi juu ya mambo mbalimbali katika kikao cha Bajeti baraza la Madiwani wilayani humo kilichoketi leo mjini hapa. Katikati ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ambrose Nchimbi na Makamu mwenyekiti Benward Komba.

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa malengo makuu ya mpango wa bajeti kwa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ni kuimarisha amani na utawala bora, kuboresha huduma za kijamii, kukuza uchumi wa wilaya hiyo kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wake, sambamba na dira ya maendeleo ya taifa inayolenga Tanzania kuwa nchi ya viwanda vya kati.

Aidha halmashauri hiyo inaendelea na jitihada za kuongeza vyanzo vipya vya mapato ya ndani badala ya kutegemea zao la kahawa pekee ambalo hivi sasa halikidhi mahitaji husika, ambapo jitihada zinafanyika za kutafuta wawekezaji watakaoweza kutumia rasilimali zilizopo wilayani humo kama vile madini, ardhi na misitu viweze kuingiza mapato zaidi.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito wakati alipokuwa akitoa maelezo mafupi juu ya rasimu ya mpango wa bajeti kwa Baraza maalum la Madiwani wa halmashauri hiyo, mwaka wa fedha 2017 hadi 2018 lililoketi leo kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

Samandito alisema kuwa kuongezeka kwa fedha hizo za mapato kutatokana pia na fedha za upimaji wa mashamba ya kahawa ambapo ekari moja hupimwa kwa shilingi 100,000 na kwamba tayari mashamba 70,000 ya wananchi wilayani humo yamepimwa na wahusika kupewa hati za kimila huku halmashauri ikiweza kupata shilingi bilioni 7,000,000,000.

Tuesday, February 7, 2017

ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA YA KUMNYWESHA SUMU MWANAYE NA KUMSABABISHIA KIFO

Na Mwandishi wetu,     
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Suzana Mgaya (19) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Wino tarafa ya Madaba wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, kwa tuhuma ya kumnywesha sumu mwanaye mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu aliyejulikana kwa jina la Gerlad Kabelege na kusababisha afariki dunia huku yeye mwenyewe pia akinywa sumu hiyo kwa lengo la kutaka kujiua.

Taarifa zilizopatikana jana mjini Songea na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Februari 5 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni katika kijiji hicho cha Wino.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa Suzana Mgaya siku hiyo alikutwa akitoka povu mdomoni na puani jambo ambalo lilisababisha hofu kwa mashuhuda kuwa huenda amekunywa sumu.

MASHINDANO KUMTAFUTA BALOZI WA UTALII RUVUMA YAFANYIKA MAJIMAJI SONGEA

Samson Kahabuka, Mratibu wa kituo cha habari za utalii mkoa wa Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

MASHINDANO ya kumtafuta Balozi wa utalii mkoa wa Ruvuma, ambayo yanaratibiwa na Kituo cha habari za utalii mkoani humo yameanza kufanyika kwenye hoteli ya Majimaji iliyopo mjini Songea.

Mratibu wa kituo hicho, Samson Kahabuka alisema kuwa warembo 15 kutoka wilaya ya Songea wameanza mazoezi kwenye ukumbi wa hoteli hiyo ambapo lengo kuu la kufanya hivyo ni kuwapata warembo watakaotoka wilaya zote za mkoa huo.

Kahabuka alisema lengo kuu la shindano hilo ni kutangaza vivutio vyote vya mkoa wa Ruvuma, ambapo Februari 10 mwaka huu warembo 15 kutoka wilaya ya Songea watatembelea wilaya ya Nyasa ili kuweza kuona baadhi ya vivutio vya wilaya hiyo.

SONGEA WAPITISHA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 26.5

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma limepitisha bajeti ya shilingi bilioni 26,531,667,816 katika mwaka wa fedha wa 2017 hadi 2018 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi wilayani humo.

Bajeti hiyo ilipitishwa juzi kwenye kikao maalumu cha Baraza hilo ambacho kilikuwa kikiongozwa Mwenyekiti wake, Rajab Mtiula katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo ambacho kilihudhuriwa na wakuu wa idara pamoja na watendaji wa kata wa wilaya hiyo.

Akiwasilisha bajeti ya mpango wa maendeleo kwa mwaka huo wa fedha mbele ya baraza la madiwani hao, Afisa mipango wa halmashauri hiyo Shaban Millao alisema kuwa bajeti hiyo imezingatia makubaliano waliyoketi katika vikao vya kamati mbalimbali.

MADIWANI MBINGA WATAKIWA KUSIMAMIA KIKAMILIFU MIRADI YA WANANCHI

Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amewataka Madiwani wa wilaya hiyo kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi ambayo inatekelezwa katika kata zao, ili iweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyokubalika.

Pia amewaasa wazingatie masuala ya kitaalamu pindi watendaji wanapotoa ushauri wakati huo wa utekelezaji wa miradi jambo ambalo litasaidia kuepusha migongano baina yao.

Nshenye aliyasema hayo juzi wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kwa Madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga juu ya sheria, kanuni na miongozo katika usimamizi na uendeshaji wa halmashauri yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

Sunday, February 5, 2017

WATUMISHI SABA WA HALMASHAURI AMBAO NI WAJUMBE BODI YA KURUGENZI SACCOS MBINGA WABURUTWA MAHAKAMANI WAKIDAIWA KULA NJAMA NA KUJIPATIA MILIONI 500

Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

HATIMAYE Watumishi saba wanaotoka katika Halmashauri ya mji wa Mbinga, wilaya ya Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma ambao pia ni Wajumbe wa bodi ya Chama cha ushirika Mbinga Kurugenzi SACCOS, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi mkoani humo wakituhumiwa kula njama na kutenda kosa la kujipatia mkopo wa shilingi milioni 500 kutoka benki ya CRDB kinyume na taratibu husika.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa Mahakamani hapo na Mwendesha mashtaka ambaye ni Wakili wa serikali mkoani hapa, Shaban Mwegole mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama hiyo Simon Kobero alidai kuwa washtakiwa hao pia wanakabiliwa na makosa kumi, wakidaiwa kughushi nyaraka mbalimbali na kufanikiwa kufanya wizi katika sehemu ya fedha hizo jambo ambalo limesababisha hasara kubwa kwa chama hicho kushindwa kujiendesha kwa manufaa ya wanachama.

Mwendesha mashtaka huyo aliwataja washtakiwa wanaokabiliwa kufanya makosa hayo na kufunguliwa kesi Jinai namba 1 ya mwaka 2017 kuwa ni, Emmanuel Mwasaga, Alex Kalilo na Zackaria Lingowe ambao ni watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa, Jamima Challe na Stella Mhagama wanatoka halmashauri ya mji wa Mbinga, Lucas Nchimbi na Mhadisa Meshack nao ni watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga.

MPANGO WA KUUZA KAHAWA KWA JINA LA EX MBINGA WANUFAISHA WAKULIMA

Upande wa kushoto ni mtaalamu wa mimea na udongo Kaminyoge Mhamerd akiwa katika eneo la shamba darasa la kilimo cha kahawa, kikundi cha Unango kata ya Ngima wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma akiwaelimisha wakulima wa zao hilo wazingatie kanuni bora za kilimo cha zao hilo.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

KATIKA kuhakikisha kwamba wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wanaendelea kunufaika na uzalishaji wa zao la kahawa wilayani humo, wilaya inaendelea kutekeleza mpango wa kuhifadhi na kuuza kahawa ikiwa na jina la Ex Mbinga, badala ya Miji ya Makambako mkoani Njombe kama ilivyokuwa hapo awali.

Aidha mpango huo wa kuuza kahawa kwa majina ya Ex Makambako ulikuwa ukisababisha kupunguza faida ya mauzo ya kahawa kwa mkulima na kuhamasisha wafanyabiashara kutorosha kahawa ya Mbinga na kumfanya mkulima aendelee kupata hasara.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye ambapo alifafanua kuwa gharama hizo kwa mkulima hivi sasa zimepungua ikiwemo na suala la utoroshaji wa kahawa, hali ambayo inavutia hata kuwepo kwa wawekezaji wa zao hilo wilayani humo.

MBINGA WAENDELEA KUFANIKIWA ZOEZI LA UPIMAJI ARDHI

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa hadi kufikia Disemba mwaka jana, mashamba yenye ukubwa wa ekari 78,149.065 sawa na hekta 31,259.626 yameingizwa na kupimwa katika mpango wa upimaji ardhi, ambapo halmashauri ya wilaya ya Mbinga katika kipindi hicho imefanikiwa kupima ekari 70,491.165 na ekari 7,657.9 zimepimwa kutoka halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma.

Kwa mujibu wa takwimu hizo na taarifa zilizomfikia mwandishi wetu kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vimethibitisha kuwa, halmashauri hizo zinaendelea kutekeleza sheria za ardhi pamoja na kutimiza agizo la serikali la kupima kila kipande cha ardhi na kukimilikisha kwa walengwa husika.

Aidha halmashauri zimekuwa zikiendelea kuhamasisha wamiliki wa viwanja na mashamba kulipia kodi za ardhi pamoja na kuviendeleza viwanja vyao kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kusambaza hati za madai ya kodi kwa wadaiwa sugu na kwamba wale wanaoshindwa kulipa hufikishwa Mahakamani.

ATIWA MBARONI KWA TUHUMA YA KUMBAKA MWANAFUNZI

Na Kassian Nyandindi,       
Songea.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Luhimba kata ya Mtyangimbole wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Allan Kihwili (48) ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka sita, ambaye anasoma shule ya msingi Ngembambili na kumsababishia maumivu makali katika sehemu zake za siri.

Zubery Mwombeji.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 24 mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika kijiji hicho wilayani hapa.

Mwombeji alifafanua kuwa inadaiwa siku ya tukio hilo mwanafunzi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa akiwa anapita jirani na nyumba ya mtuhumiwa huyo ghafla alimkamata na kumwingiza kwenye nyumba anayoishi kisha kumfanyia unyama huo.

Friday, February 3, 2017

DC MBINGA AWATAKA WADAU WA SHERIA KUTENDA HAKI NA KUTEKELEZA WAJIBU WAO IPASAVYO

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa ucheleweshaji wa utoaji haki kwa wakati unasababisha kupoteza rasilimali muda na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, hivyo wito umetolewa kwa wadau wote washeria kuhakikisha kwamba wanatenda haki na kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Aidha vitendo vya rushwa na kuweka vikwazo visivyokuwa na sababu ya msingi Mahakamani, ambavyo vinazuia utoaji wa dhamana kwa watuhumiwa vinachangia kuleta msongamano wa mahabusu gerezani.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Mahakama ya wilaya hiyo mjini hapa.

“Nasisitiza kwamba zile kesi ambazo zinauwezekano wa kutolewa dhamana zitolewe dhamana kwa wakati, tuache tabia ya kuwaweka mahabusu gerezani tupunguze wasiwepo wengi wanaokaa huko bila sababu yoyote ile ya msingi”, alisema Nshenye.

WAFUASI WATATU CHADEMA WAPANDISHWA KIZIMBANI WAKIDAIWA KUHARIBU GARI LA CCM

Na Mwandishi wetu,       
Songea.

WAFUASI watatu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi mkoani humo, kwa tuhuma ya kula njama na kuharibu gari la Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kulipiga mawe.

Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali kanda ya Songea Tumaini Ngiruka aliwataja Mahakamani hapo washitakiwa hao kuwa ni Joseph Fuime (52) mkazi wa Songea mjini aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani humo, Emmanuel Kalisinjesi (37) mkazi wa mtaa wa Ruvuma na Sedrick Komba (51) mkazi wa Bombambili mjini hapa.

Mwendesha mashtaka ambaye ni Mwanasheria huyo wa Serikali kanda ya Songea, Ngiruka alidai mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya mkoa wa Ruvuma, Issa Magori kuwa mnamo Januari 20 mwaka huu majira ya usiku katika eneo la mtaa wa Pambazuko uliopo nje kidogo ya Manispaa ya Songea washtakiwa hao waliharibu gari la CCM aina ya Landcruiser lenye namba za usajili T 640 BEU kwa kulipiga mawe na kusababisha kuvunjika kioo cha mbele ya gari hilo na upande wa dereva.

WASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA YA KUJERUHI

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia wakazi wawili wanaoishi katika mtaa wa Pambazuko uliopo katika kata ya shule ya Tanga Manispaa ya Songea mkoani humo, kwa tuhuma ya kumjeruhi Abethi Ponera (25) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kwenye paja lake la mguu upande wa kulia na kumsababishia jeraha na maumivu makali.

Zubery Mwombeji.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Bernad Mng`ong`o (39) na Boniface Mbecha (27) wote wakazi wa mtaa huo.

Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 21 mwaka huu majira ya saa tano usiku, katika mtaa huo.

Alifafanua kwamba siku ya tukio hilo Ponera akiwa anarudi nyumbani kwake akitokea kunywa pombe kwenye kilabu cha pombe za kienyeji, ghafla alivamiwa na watu asiowafahamu na kuanza kumpiga kisha kumjeruhi paja lake la mguu wa kulia na kuathiri sehemu zake za siri.

Alisema kuwa Ponera kabla ya kukutwa na tukio hilo akiwa katika kilabu hicho ambacho kinamilikiwa na Mg’ong’o kulikuwa na malumbano kati yake na watu wengine aliokuwa anakunywa nao pombe hizo za kienyeji, ambao walikuwa wakimtaka ifikapo Januari 22 mwaka huu aende kwenye uchaguzi mdogo akamchague mgombea udiwani wanayemtaka wao (chama ambacho jina lake linahifadhiwa) jambo ambalo Ponera alipingana nalo kisha baadaye aliamua kuondoka kuelekea nyumbani.