Wakulima wa kahawa Mbinga wakipeana mawazo namna ya kuzingatia kanuni bora za uendeshaji wa vyama vyao vya ushirika. |
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
VIONGOZI waliopo katika Vyama vya
ushirika wa kahawa Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wamesisitizwa kujenga
mahusiano mazuri na viongozi wa Serikali ambao wamepewa dhamana ya kusimamia
maendeleo ya vyama hivyo Wilayani humo, ili kuweza kuvifanya viweze kusonga
mbele kimaendeleo.
Aidha imeelezwa kuwa ushirika wa zao
hilo katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya hiyo ulifikia hatua ya kufa,
kutokana na utendaji mbaya na kutokuwepo kwa ushirikiano mzuri kati ya wakulima
na viongozi hao.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas
Nshenye alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa vyama vya
ushirika katika mafunzo elekezi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mbicu hotel
uliopo mjini hapa.
“Ndugu zangu ushirika ni sehemu ya
Serikali hivyo nasisitiza juu ya uwepo wa mahusiano mazuri katika utendaji wenu
wa kazi, ninyi viongozi mkiona wakulima wanadhulumiwa mnapaswa kuvaa ile sura
ya uadilifu na kutenda haki kwa hiyo suala hili la uadilifu nawataka huko
muendako mkalizingatie”, alisisitiza Nshenye.
Nshenye amewataka pia wabadilike na
kuachana na vitendo vya wizi na kwamba ameapa kuwa pale atakaposikia kiongozi
yeyote yule wa chama cha ushirika Wilayani hapa amehusika kumuibia mkulima
Serikali itachukua hatua kali za kisheria ikiwemo kumfikisha Mahakamani.
Alifafanua kuwa viongozi hao wa vyama
vya ushirika wanapaswa kuweka wazi utendaji wao wa kazi ikiwemo bei na taarifa
za mauzo ya kahawa zao na sio kutengeneza mbinu za kificho.
Naye Benigna Haulle ambaye ni Mratibu
wa mafunzo hayo kutoka chuo kikuu cha ushirika Moshi Ofisi ya Mkoa wa Ruvuma,
alisema kuwa mpango uliowekwa na Serikali hivi sasa ni kutaka kuona mkulima
anayezalisha kahawa ananufaika na zao lake na sio vinginevyo.
Haulle alibainisha kuwa Halmashauri
za Wilaya zinapaswa kudhibiti ubora wa kahawa kwa kushirikiana na wakulima
wenyewe na kwamba hivi sasa Makampuni yatanunua kahawa mnadani lakini vyama
vyote vya ushirika vinapaswa kuomba kibali cha kununua zao hili katika
halmashauri husika.
“Kila mmoja wetu achukue nafasi hii kuwajibika
ipasavyo hebu sasa tuvae kikamilifu sura ya mkulima, tuachane na vitendo vya
hujuma ambavyo hurudisha nyuma maendeleo ya mkulima”, alisema Haulle.
Kwa upande wake Leo Kumburu ambaye ni
Afisa kilimo wa Wilaya ya Mbinga kitengo cha ukaguzi na ubora wa kahawa
aliwataka wakulima wa zao hilo kuachana na vitendo vya kuanika kahawa mbivu
chini badala yake wanapaswa kuanika kwenye meza maalum ili kuweza kulinda ubora
wake.
Vilevile alipiga marufuku biashara za
magoma ya kahawa huku akitaka kahawa yote inayopokelewa kwenye chama husika cha
ushirika ipokelewe kwa stakabadhi maalum.
No comments:
Post a Comment