Monday, December 15, 2014

ILE NYOTA ILIYONG'ARA MBINGA KIMAENDELEO IMEZIMIKA, KATIBU MKUU UMOJA WA VIJANA TAIFA ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI


Menas Mbunda Andoya wakati wa uhai wake akiwa na mkewe na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa mradi wake wa kuzalisha umeme, maporomoko ya maji katika kijiji cha Lifakara, kata ya Mbangamao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.



Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma. 

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Sixtus Mapunda, ametoa salamu za pole kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla, kwa kuondokewa na mwanaharakati ambaye ni mpiganaji katika mchango wa kukuza maendeleo wilayani humo, Marahemu Menas Mbunda Andoya.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Katibu huyo alisema kuwa amepokea taarifa ya kifo cha mwanaharakati huyo, kwa masikitiko makubwa na kuwataka wananchi wa wilaya hiyo, kuungana pamoja katika kipindi hiki cha majonzi.

Mapunda alifafanua kuwa katika kipindi hiki kigumu, wananchi hawana budi kumuombea kwa Mungu Marahemu huyo, kwani sote tupo safarini na hapa duniani tunapita.

Marahemu Andoya alikuwa mpiganaji hasa katika shughuli nyingi za kimaendeleo wilayani Mbinga, ambapo ameacha kazi muhimu ambayo alikuwa akiitekeleza na yenye kufikia hatua ya mwisho juu ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa maporomoko ya maji ambao unafahamika kwa jina maarufu, Andoya Hydro Electric Power (AHEPO) uliopo katika kijiji cha Lifakara kata ya Mbangamao wilayani humo. 

Lengo la mradi huo ukishakamilika taratibu husika, utaunganishwa katika mfumo wa gridi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tawi la Mbinga. 


Kwa ujumla mradi huo, tayari mfumo wa umeme na nguzo zimekwisha jengwa na kusambazwa katika maeneo husika, na kilichobakia ni taratibu za kufunga na kuwasha mitambo husika ili nishati hiyo muhimu ianze kusambazwa kwa wateja. 

Historia fupi ya mradi:

Menas Mbunda Andoya, ni mzalendo wa Tanzania ambaye alibuni mradi huo wa umeme wa maji takribani miaka 13 iliyopita ambapo wazo lake la kuanzisha mradi huo, lilimfanya akumbane na vikwazo vingi ikiwamo kufukuzwa kama kuku na watu katika ofisi zao huku akipigwa vita kila kona.

Andoya ambaye ni Mkurugenzi wa AHEPO hakuchoka wala kukata tamaa ambapo aliendelea kuwa jasiri, hatimaye mradi mkubwa wa umeme wa maporomoko ya maji alioubuni mwaka 2000 umezaa matunda baada ya kufanikiwa kuwasha umeme kwa majaribio.

Kadhalika Andoya (57) anafahamika na watu wengi na ni mzaliwa wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, akiwa ni mtoto wa tatu kati ya saba katika familia yao ambapo marahemu huyo ameacha watoto watatu wa kiume. Kitabia ni mcheshi, mwenye busara na mtu ambaye alikuwa akijiamini kwa kila alichokuwa akikifanya.

Andoya ambaye alikuwa rafiki yangu wa karibu, wakati wa uhai wake siku zote alikuwa akiniambia kwamba, alikuwa na hamu kubwa ya kuona anafanikiwa na kuhakikisha anatimiza ndoto yake na Watanzania wenzake hususani wanambinga, wanapata huduma ya umeme na atakapokufa akiwa na faraja ya kutimiza lengo lake.

Madhumuni ya kuzalisha umeme katika mradi huo ni Megawati 1 na kuunganishwa kwa wateja wa awali 922 kati ya 3,835 katika vijiji vya Lifakara, Kilimani na Mbangamao wilayani hapa na ziada kuuzwa TANESCO ukilenga kupata umeme kwa njia endelevu na nafuu.

Hivi sasa tayari ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme kutoka Mbinga mjini, hadi kituo kikuu cha uzalishaji na usambazaji katika vijiji hivyo umekwisha kamilika.

Mwaka 2005 kampuni hiyo ya Andoya Hydro Electric Power ilisajiliwa na upembuzi yakinifu wa mradi ulikamilika, hatimaye taarifa na mchanganuo wa mradi ulipitiwa na wataalamu mbalimbali wa taasisi za serikali ikiwamo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), NEMC na Wataalamu kutoka Benki ya Dunia nao wote waliafiki kuwa kiasi cha Megawati 1 kinaweza kupatikana katika maporomoko hayo ya mto Mtandasi. 

Kufikia Novemba 2012 mradi ulifanikiwa kupata kibali na fedha za kutekeleza, ukiwa katika hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa njia ya usafirishaji wa umeme yenye urefu wa kilometa 14 kwa kiwango cha HT kutoka kituo cha umeme cha Mbangamao hadi makao makuu ya wilaya ya Mbinga, ili kuunganisha na gridi ya TANESCO pamoja na vijiji vya Lifakara kilmometa 2, Kilimani kilomoeta 4 na Mbangamao kilometa 4.

Awamu ya pili ilikuwa ni ujenzi wa njia za kusambaza nishati hiyo muhimu kwa wateja, ambapo gharama za ujenzi wa mradi huo ni shilingi bilioni 4.5 na kwamba asilimia 30 zilichangwa kutoka mtaji wa kampuni ya Andoya Hydro electric power, asilimia 70 ni mkopo kutoka benki ya CRDB, mkopo wa benki ya dunia kupitia serikali na taasisi zake ikiwamo (REA) chini ya mpango wa Tanzania Energy Development and Access Project (TEDAP) ambapo pia UNIDO wameahidi kuchangia dola 250,000 za Marekani. 

Menas Mbunda Andoya, alifariki dunia, Desemba 14 mwaka huu majira ya asubuhi katika hospitali ya serikali wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, baada ya kuugua ghafla, na mazishi yatafanyika Desemba 16 mwaka huu yakianzia na misa takatifu majira ya saa 5:00 asubuhi, katika kanisa katoliki la Jimboni lililopo mjini hapa.

Mungu alitupatia na ametwaa, ailaze roho ya Marahemu mahali pema peponi, kazi ya Mola haina makosa, Amen.