Na Mwandishi wetu,
Iringa.
SERIKALI
imeziagiza Mamlaka za usafiri wa majini na nchi kavu
(SUMATRA ) nchini, kuanza mchakato wa kukaa na
wamiliki wa vyombo hivyo ili kuanza uagizaji wa
vyombo vya usafiri yakiwemo mabasi ambayo ni rafiki na walemavu
nchini, huku ikipiga marufuku majengo ya serikali kujengwa
bila kuwepo kwa mchoro unaoonyesha mazingira yanayozingatia
makundi yote ya jamii likiwemo la walemavu wa viungo.
Agizo
hilo limetolewa na Waziri mkuu Mizengo Pinda,
wakati wa maadhimisho ya siku ya walemavu duniani
yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya
kichangani mkoani Iringa.
Akiwahutubia
walemavu hao na wananchi waliofika katika viwanja
hivyo waziri mkuu, aliyewakilishwa na Waziri wa nchi ofisi
ya waziri mkuu (sera na uratibu wa bunge) Wiliam Lukuvi ambaye ni mbunge
wa jimbo la Isimani mkoani Iringa, alisema kimekuwepo kilio
cha muda mrefu kutoka kwa walemavu juu ya kusahulika katika
ujenzi wa majengo mbalimbali, ambayo yamekuwa
yakijengwa bila kuzingatia kundi la watu wenye
ulemavu jambo ambalo ni sawa na kuwabagua watu hao.
Aidha alisema
katika kuona kilio hicho cha walemavu kinafanyiwa
kazi kuanzia sasa, majengo yote ya serikali
zikiwemo shule na taasisi nyingine kabla ya kuanza
ujenzi wake lazima wasimamizi wa ujenzi huo
kujiridhisha kwa mchoro ambao utaonyesha mazingira
yatakayomuwezesha mlemavu, kutumia jengo husika bila
usumbufu wowote tofauti na ilivyo sasa ambapo idadi kubwa ya
majengo mazingira yake si rafiki kwa mlemavu.
"Ni siku
nyingi watu wenye ulemavu wamekuwa wakilalamika juu ya
mazingira yasiyo rafiki katika majengo mbalimbali............
sasa leo naomba kuagiza kuwa michoro yote inayochorwa katika
majengo ya huduma za kijamii, ni marufuku kupitishwa
ama wasimamizi wa ujenzi husika kuruhusu
ujenzi iwapo mchoro hauonyeshi kama utajali makundi yote
wakiwemo walemavu,
“Wasimamizi wote
msikubali kusimamia wala kutangaza tenda ya
ujenzi kama ramani yake si rafiki kwa mlemavu, lakini
pia hata kwenye mabasi hivi unamtegemea mtu mwenye ulemavu wa miguu
ataingia vipi na baiskeli yake katika gari iwapo hakuna
mazingira yanayomwezesha kuingia, hivi sasa
teknlojia imezidi kukua na baadhi ya nchi wameanza muda mrefu
kuwajali walemavu kwa kuwa na mabasi ambayo mlemavu anaingia na baiskeli
yake na kushuka nayo bila usumbufu, ni vyema hata
Sumatra mkaangalia uwezekano wa kuwajali walemavu hawa”, alisema
Lukuvi.
Kuhusu ombi la walemavu
hao hasa kwa wale wasiosikia wameiomba
serikali kuwa na wakalimani katika kituo cha Televisheni ya Taifa
(TBC) na vituo vingine vya luninga, ili
kuwawezesha walemavu hao nao kuweza kufuatilia hotuba
ya Rais mwisho wa mwezi na mambo mengine badala ya kutengwa.
Lukuvi alisema
kuwa suala hilo ni wajibu wa serikali
kuwajali watu wake hivyo tayari imeuagiza
uongozi wa TBC, na mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA)
kulitafutia ufumbuzi suala hilo la mkalimani hasa
katika TBC .
Katika hatua
nyingine Lukuvi aliwataka walemavu hao ili ombi
lao la kutazamwa katika nafasi za uongozi liweze
kuzingatiwa, ni vyema wao wenyewe kujitokeza kwa
wingi kuipigia kura katiba iliyopendekezwa pindi
itakapokuja kwa wananchi kwa madai kuwa katika
katiba hiyo imezingatia mambo mengi ya kijamii, likiwemo
la kuwajali watu wenye ulemavu kwa kuwatengea nafasi
nyingi zaidi na iwapo katiba hiyo
itapitishwa kazi ya msuguano wa rushwa unaweza kuhamia kwa
walemavu kwa kila mmoja kutaka kupewa nafasi.
"Hadi
hivi sasa ni chama cha mapinduzi (CCM) pekee ambacho kina wabunge
wa viti maalum wa kuteuliwa kutoka kundi la walemavu
huku vyama vingine vyote havijawakumbuka kabisa
watu wenye ulemavu ukiacha mbunge wa jimbo la Lindi mjini
pekee ambae hakupendelewa katika ubunge wake bali alishindwa
kihalali kwa kuchaguliwa na wananchi wake..nafikiri
tushirikiane kuhakikisha katiba hii iliyopendekezwa
inapita ili tuungane pamoja katika kujenga nchi yetu”,
alisema.
Katika salaam
za walemavu kote nchini, Waziri wa Afya na ustawi wa
jamii Dokta Seil Rashid zilizotolewa kwa niaba yake
na mwenyekiti wa baraza la watu wenye ulemavu nchini na
Dunford Makala, alisema kuwa wizara
inaendelea kuimarisha ushirikiano na vyama vya
watu wenye ulemavu, na shirikiasho la vyama vya
watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) katika kuhakikisha
utekelezaji wa uwekaji wa fursa na haki sawa kwa
watu wenye ulemavu nchini.
Alisema
katika kuhakikisha ushirikiano unakuwepo wizara yake
imezindua baraza la ushauri la Taifa la
watu wenye ulemavu, toka mnamo 1 Novemba 2014 na
katika hilo kamwe hawataacha kumpongeza Rais Dokta
Jakaya Kikwete kwa kumteua mwenyekiti wa baraza
hilo.
Alifafanua kuwa ni
ukweli usiopingika kuwa nchi hii chini ya Rais Dkt
Kikwete imefanya mambo mengi zaidi ya kuwajali
watu wenye ulemavu katika Nyanja za kiuchumi, kiutamaduni
na kisiasa ambavyo vyote hivyo kumwezesha mlemavu
kujikwamua kimaisha.
Hata
hivyo alisema ushahidi wa yote hayo ni pamoja na kuridhia
mikataba ya kimataifa juu ya haki za watu wenye ulemavu,
kutungwa kwa sheria Na.9 ya mwaka 2010 ya watu wenye ulemavu na
kanuni zake, kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika tume ya
mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
kuteuliwa kwa wajumbe 20 wenye ulemavu katika bunge
maalumu la mabadiliko ya katiba la mwaka 2014.
Awali walemavu
hao katika risala yao iliyosomwa na makamu mwenyekiti
wa SHIVYAWATA Amina Mollel, pamoja na kuishukuru serikali kwa
jinsi kwa kuendelea kuwa karibu zaidi na
watu wenye ulemavu kwa kushiriki shughuli mbali mbali za walemavu, bado
waliweza kuishukuru serikali kwa kuandaa sera ya maendeleo ya
watu wenye ulemavu ya mwaka 2004, kutambuliwa kwa watu wenye
ulemavu katika MKUKUTA, kuwezesha kuongezeka kwa idadi ya watu wenye
ulemavu wanaopata elimu kuanzia shule za msingi hadi elimu ya juu
na mambo mengine mengi ambayo wao kama walemavu
wamekuwa wakiona serikali yao ipo pamoja nao.
Sanjari na mema
hayo bado waliiomba serikali kuzingatia kuwapatia walemavu mambo
muhimu katika maisha ya kila siku ikiwa ni pamoja na kuwa na vyombo
vya usafiri rafiki kama magari moshi.vyombo vya usafiri majini
,angani ,miundo mbinu katika majengo na viwanja vya
ndege ambavyo vitamwezesha mlemavu pia kuwa huru.
Mkuu wa mkoa wa
Iringa Amina Masenza alisema kuwa maadhimisho hayo
yaliyofanyika chini ya kauli mbiu isemayo, "Maendeleo
endelevu ahadi ya Teknolojia, huku mkoa wa Iringa
ukiendelea kuwa bega kwa bega na walemavu ikiwa
ni pamoja na kufanya kazi karibu na vyama hivyo
vya watu wenye ulemavu na kuwa mkoa huo
kwa sasa, una jumla ya walemavu zaidi ya 179,000 na
wote serikali imeendelea kuwalinda na kuwa nao pamoja.
No comments:
Post a Comment