Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAJUMBE wa bodi ya Kamati ya usimamizi Chama cha ushirika
Mbinga Walimu SACCOS iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamekamatwa na
kuwekwa mahabusu wakituhumiwa kuiba shilingi milioni 540,704,572 za wanachama
wa chama hicho cha ushirika na kusababisha hasara kubwa kwa chama kushindwa
kujiendesha kwa manufaa ya wanachama.
Aidha hatua hiyo ya kukamatwa kwa Wajumbe hao ilitolewa na
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo, Biezel Malila baada ya
kusomwa taarifa ya ukaguzi juu ya mwenendo wa chama hicho cha ushirika ambayo
ilibainisha wizi wa fedha hizo katika mkutano mkuu maalumu wa wanachama,
uliofanyika Februari 18 mwaka huu kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini
hapa.
“Kwa masikitiko makubwa ndugu zangu wanachama mliohudhuria
mkutano huu naomba niwaeleze kwamba mwenendo wa chama hiki sio mzuri unatia
kichefuchefu, chama kina hali mbaya kina hati chafu ya ukaguzi kwa kuwa Wajumbe
wa bodi hii wameshiriki kwa namna moja au nyingine kukiuka taratibu za
uendeshaji wa chama hiki, hivyo wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria na
taratibu husika za vifungu vya uendeshaji wa vyama vya ushirika”, alisema
Malila.
Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma alifafanua
kuwa fedha hizo ambazo Wajumbe hao wanadaiwa kuiba na kujinufaisha kwa matakwa
yao binafsi zilitokana na baki ya mikopo shilingi milioni 174,915,794 hisa,
akiba na amana shilingi milioni 363,873,778 na mikopo ambayo waliitengeneza
bila kufuata taratibu husika walichota shilingi milioni 1,915,000.
Alieleza kuwa mpaka sasa ni Wajumbe kumi na nne ndio
waliohusika kuiba fedha hizo ambazo ni za wanachama wa Mbinga Walimu SACCOS
ambapo kati ya hao waliokamatwa na kuwekwa mahabusu ni wanne tu ambao ni
Sostenes Ndunguru ambaye ni Meneja, Prosper Mbepera ni Mhasibu, Stephen Komba
mjumbe kamati ya usimamizi na Edmund Hyera ambaye ni mjumbe wa bodi.
Alifafanua kuwa Wajumbe kumi wamekimbia hawajulikani walipo
ambapo taarifa zao zimeripotiwa Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga na
kwamba wanatafutwa ili waweze kujibu tuhuma hizo zinazowakabili ambao ni
Emmanuel Kapinga Mwenyekiti, Kenneth Ndunguru, John Komba, Peter Challe, Batson
Mpogolo, Osmund Komba, Wille Mkwene, Marion Nchillas, Materinus Ndunguru na
Tabu Mshani ambao wote nao walikuwa ni Wajumbe wa bodi katika SACCOS hiyo.
“Hawa waliotoroka kufuatia kuwepo kwa kesi hii ya ubadhirifu
wa fedha hizi, madai yao yamefunguliwa Kituo kikuu cha Polisi Mbinga, tunawatafuta
popote pale walipo ili waweze kukamatwa na kujibu tuhuma hizi zinazowakabili mbele
yao na kila mtu atabeba mzigo wake”, alisisitiza Malila.
Malila aliongeza kuwa fedha hizo ambazo zililenga kuwanufaisha
wanachama kwa mtindo wa kukopeshana cha kushangaza Wajumbe hao wamejinufaisha
kwa matakwa yao binafsi, hivyo wanatakiwa kuzilipa kwa mujibu wa kifungu namba
55 cha sheria ndogo namba 13 ya ushirika namba 6 ya mwaka 2013.
Kadhalika kufuatia kuwepo kwa tukio hilo Mrajisi huyo ametoa
wito kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma, akiwaonya
kuacha vitendo vya wizi wa fedha na mali za ushirika na kwamba ofisi yake itaendelea
kuchukua hatua za kuwafungulia mashtaka wale wote watakaobainika kushiriki
katika upotevu wa mali za ushirika.
Vilevile Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amethibitisha
kuwepo kwa tukio hilo ikiwemo kukamatwa kwa watuhumiwa hao wanne, huku
akifafanua kuwa wanaendelea kuhojiwa kutokana na tuhuma zinazowakabili na hao
wengine kumi waliobakia ambao wamekimbia hawajulikani walipo Jeshi hilo linaendelea
kuwasaka popote pale ili waweze kuwakamata na kujibu tuhuma hizo zinazowakabili.
Awali wakichangia hoja kwa nyakati tofauti katika mkutano huo
wanachama wa SACCOS hiyo waliunga mkono jitihada hizo zilizochukuliwa na
Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoani hapa, huku wengine wakidai kuwa
wamesikitishwa kwa taarifa hizo ambazo ni utovu mkubwa wa nidhamu uliofanyika
ndani ya chama chao juu ya matumizi mabaya ya fedha za wanachama.
Percy Komba ambaye ni mmoja kati ya wanachama wa ushirika huo
alisema kuwa taarifa hiyo ya mkaguzi ambayo imesomwa mbele yao inaonesha kuwa
na madudu mengi ya ubadhirifu wa fedha na dosari za kiutendaji, hivyo kwa
uchungu walionao wanachama kuna kila sababu kwa viongozi wao kuchukuliwa hatua
za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Naye Renatus Nambombe ambaye ni mwananchama wa ushirika huo
aliongeza kwa kusema kuwa tukio hilo wanalilinganisha na msiba mkubwa ambao
umewapata na hawakutegemea kama yangeweza kutokea mambo hayo.
“Kwa kilio hiki kilichotupata hawa watuhumiwa wanastahili kabisa
kukamatwa na kutiwa pingu mikononi ili
wafikishwe Mahakamani, kwani inasikitisha sana na kutuongezea uchungu mkubwa
katika maisha yetu”, alisema Nambombe.
Pamoja na mambo mengine chama hicho cha ushirika kinaundwa na
wanachama ambao ni watumishi wa serikali kutoka katika halmashauri ya mji wa
Mbinga, wilaya ya Mbinga na Nyasa ambapo makao makuu ya ofisi zake yapo Mbinga
mjini.
Katika mkutano huo hatua iliyofuata ilikuwa ni ya kuvunja
bodi ya Chama hicho cha ushirika Mbinga Walimu SACCOS kufuatia kuwepo kwa
matatizo hayo ya wizi wa fedha za wanachama na kwamba, waliteuliwa Wajumbe watano
wa bodi ya mpito mpaka utakapofanyika uchaguzi mkuu wa kuwachagua Wajumbe wengine
watakaoweza kuongoza ushirika huo.
Wajumbe hao walioteliwa kuongoza watadumu kwa muda usiozidi
mwaka mmoja ambao ni Vitalis Mapunda ambaye ni Mwenyekiti, Judith Komba, Sota
Ndunguru, Michael Simbo na Silvester Msuha ambao wote ni wajumbe wa mpito kamati
ya usimamizi.
Awali hivi karibuni nao Watumishi saba wanaotoka katika halmashauri hizo
wilayani humo ambao pia ni Wajumbe wa bodi ya Chama cha ushirika Mbinga
Kurugenzi SACCOS iliyopo mkoani hapa, walikamatwa Januari 21 mwaka huu waliwekwa
mahabusu na kufikishwa Mahakamani wakituhumiwa kuiba shilingi milioni 500 za
wanachama wa chama hicho cha ushirika.
Kukamatwa kwao na kufikishwa katika mkono wa sheria
kulitokana pia na Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma kueleza kwamba
fedha hizo ambazo Wajumbe hao wanadaiwa kujinufaisha kwa matakwa yao binafsi
zilitokana na mkopo wa shilingi milioni 500 uliotolewa na benki ya CRDB kwa
ajili ya kukopeshwa wanachama lakini cha kushangaza waliamua kuzitumia kinyume
na taratibu husika.
Hata hivyo watuhumiwa hao saba ni Zackaria Lingowe,
Emmanuel Mwasaga, Alex Kalilo, Jamima Challe, Stella Mhagama, Lucas Nchimbi,
Mhadisa Meshack na kwamba mpaka sasa shtaka lao limefikishwa katika Mahakama ya
Hakimu mkazi Mfawidhi mkoa wa Ruvuma ambapo litatajwa tena Marchi 7 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment