Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SHULE ya Sekondari Kitura
iliyopo katika kata ya Kitura wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, haina mwalimu wa somo
la Hisabati na Fizikia tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 jambo ambalo limekuwa
likisababisha wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kutosoma kabisa masomo hayo
muhimu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye. |
Kaimu Mkuu wa shule hiyo,
Stanslaus Mapunda alisema hayo juzi wakati wa ziara ya Madiwani ambao ni
Wajumbe wa Kamati ya uongozi na mipango ya halmashauri ya wilaya hiyo, iliyokuwa
ikiongozwa na Mwenyekiti wake Ambrose Nchimbi.
Mapunda alisema kuwa licha ya
kulifikisha tatizo hilo katika mamlaka husika kwa muda mrefu hakuna utekelezaji
uliofanyika na kwamba mpaka sasa pia hakuna ufumbuzi uliofikiwa juu ya utatuzi
wa tatizo hilo hivyo wanalazimika kufundisha masomo mengine tu jambo ambalo
limekuwa likisababisha watoto hao kutopata fursa nzuri ya kujisomea.
Kwa upande wake Mratibu elimu
kata, Nikodem Hyera alisema kuwa bado wataendelea kufuatilia walimu hususani
hao wa masomo hayo mawili ambayo hayana walimu ili kuepukana na tatizo hilo
ambalo limedumu kwa miaka kumi sasa bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Mbinga, Nchimbi alisema kuwa ipo changamoto kubwa ya upungufu wa walimu
wa masomo ya hesabu na sayansi hivyo serikali wilayani humo itahakikisha inawasiliana
na mamlaka husika ili kuweza kuona ni namna gani tatizo hilo linapatiwa
ufumbuzi kwa kuwapelekea walimu wa masomo hayo.
“Tatizo la walimu wa masomo
haya halipo huku kwetu pekee bali ni la nchi nzima hivyo pamoja na tatizo hili
kuwepo hapa kwetu, lazima tuhakikishe tunalimaliza hata kama tutapata mwalimu
mmoja atakayeweza kufundisha masomo haya mawili”, alisema Nchimbi.
Hata hivyo Nchimbi alisema kuwa
kuwepo kwa changamoto hiyo kunawafanya hata wazazi kushindwa kuwahamasisha
watoto wao wapende kusoma masomo ya sayansi na kwamba licha ya tatizo hilo, kwa
wale ambao wamebahatika shule zao kuwa na walimu wanaofundisha masomo hayo wanapaswa
kuhakikisha kuwa wanasoma kwa bidii ili hatimaye wataalamu wanaotokana na masomo
hayo waweze kupatikana kwa urahisi kama vile waganga na wataalamu wa afya.
No comments:
Post a Comment