Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
HALMASHAURI ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imejiwekea
mikakati ya usambazaji wa miche bora ya kahawa kwa wakulima wake ambapo tayari
miche 33,333 imegawiwa kwa wakulima wanaoishi katika vijiji vya Litola,
Namabengo na Lumecha wilayani humo katika msimu wa kilimo mwaka huu.
Aidha lengo la uzalishaji huo ni kuwafanya wakulima hao
waweze kupanda zao hilo katika mashamba yao na baadaye waweze kujikwamua
kiuchumi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Kaimu Ofisa kilimo wa wilaya hiyo, Aniceth Ndunguru alisema
kwamba yeye ndiye aliyesimamia zoezi la ugawaji wa miche hiyo kwenye vijiji
hivyo na kwamba halmashauri hiyo, katika bajeti yake ya mwaka 2016/2017
ilitenga kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kununulia miche hiyo ambayo
wakulima hugawiwa bure hatimaye waweze kupanda katika mashamba yao.
Ndunguru alisema kuwa ugawaji wa miche hiyo umekamilika na
kwamba licha ya uwepo wa changamoto ya ongezeko la mahitaji ya zao hilo, halmashauri
ya wilaya ya Namtumbo itaendelea kuisambaza kulingana na taratibu husika.
Kadhalika Stevene Mtunguja ambaye ni Ofisa kilimo wa kata ya
Namabengo alisema kuwa idadi ya wananchi wanaojitokeza kuhitaji miche hiyo hivi
sasa ni kubwa, tofauti na msimu uliopita waliweza kusambaza miche 1,500 tu na
wananchi walionesha kusuasua kutohitaji kwa wingi.
Pamoja na mambo mengine, halmashauri hiyo pia imeweza
kusambaza mbegu za korosho kilo 660 zenye thamani ya shilingi milioni 1,980,000
na miche ya mikorosho 10,020 iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 10,020,000
katika vijiji vya Lingusanguse, Magazini, Amani, Msisima na Matepwende.
Wakati wa usambazaji huo pia kulikuwa na zoezi la usambazaji
wa mbegu aina ya choroko kilo 1,000 zenye thamani ya shilingi 1,500,000 mbaazi
kilo 1,000 zenye thamani ya shilingi 4,000,000 na ufuta kilo 400 wenye thamani
ya shilingi 4,000,000.
Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina jumla ya vijiji 71
ambapo ugawaji wa miche na mbegu za mazao hayo yamekuwa yakizingatia hali ya
hewa katika eneo husika na uhalisia wa kuweza kustawi zao hilo.
No comments:
Post a Comment