Na Steven
Augustino,
Tunduru.
MHUDUMU wa kuuza vinjwaji katika baa ya Tunduru Pub
mjini hapa, aliyefahamika kwa majina ya Mary Baby Obodo amefariki dunia wakati
akijaribu kutoa mimba kwa njia za kienyeji.
Binti huyo ambaye alianza kufanya kazi hiyo mwanzoni
mwa mwezi Desemba mwaka jana katika baa hiyo, inadaiwa kuwa alifanya jaribio hilo la kutoa mimba
wakati akiwa katika nyumba ya kulala wageni ya iitwayo New Sety View ambako
alikuwa akiishi tangu afike mjini hapa.
Wakizungumzia tukio hilo
miongoni mwa mashuhuda wa tukio hilo walisema
kuwa baada ya kufanya jaribio hilo,
na kufanikiwa kuua kiumbe hicho marehemu alianza kuishiwa nguvu na kuzidiwa ghafla
hali ambayo iliwafanya wasamaria wema kumkimbiza hospitali ya serikali ya wilaya
ya Tunduru kwa matibabu zaidi.
Walisema binti huyo ambaye alionekana kuweka siri
alifichua siri hiyo akiwa katika hatua za mwisho za kukata roho, hali ambayo pia
iliwafanya madaktari kumuongezea kwa haraka chupa mbili za damu, iliyotolewa na
msamaria aliyefahamika kwa jina moja la Kaimu, ikiwa ni juhudi za kujaribu
kuokoa maisha yake.
Walisema baada ya tukio la kifo hicho ndipo yakafichuka
mengi kuwa majina hayo aliyokuwa akiyatumia marehemu yalikuwa ni ya uongo
ambapo baada ya kumpigia simu baba yake mzazi aliyejitambulisha kwa jina la
Gerodi Msemwa, alieleza kuwa kama kweli aliyefariki dunia ni binti yake jina lake ni
Tumaini na sio hayo.
Mzazi huyo ambaye ilimchukua muda mrefu kuyaelewa
maelekezo ya kifo cha binti yake alisema kuwa yeye siyo mchaga na wala siyo
mkazi wa mkoa wa Mbeya, bali ni mkazi wa mkoa wa Njombe na akaendelea
kubainisha kuwa marehemu alitoweka nyumbani miaka mitatu iliyopita na hakuwa na
mawasiliano naye.
Taarifa zilizotolewa na rafiki wa marehemu zinaeleza
kuwa kabla ya kwenda kufanya kazi katika baa hiyo, alikuwa nafanya kazi katika
miji ya Mbeya, Iringa, Songea na Tunduma ambako inadaiwa kuwa ndiko
alikoipatia ujauzito aliokuwa nao hivyo baada ya kuahidiwa kuolewa na mtu aliyefahamika
kwa jina moja la Jaki.
Taarifa zilizotolewa na maafisa tabibu katika hospitali
ya Tunduru ambako alilazwa, kabla ya kupatwa na mauti zinaeleza kuwa chanzo cha
kifo hicho kilisababishwa na kutokwa na damu nyingi, pamoja na kiumbe hicho
kilicho kuwa na umri wa miezi sita kushindwa kutoka.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Msemwa, mwili wa
marehemu utazikwa katika makaburi yaliyopo mtaa wa Nakayaya mjini Tunduru.
No comments:
Post a Comment