Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKATI serikali ikiendelea kumaliza
mgogoro wa kupinga kusafirishwa kwa gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, hali
hiyo imehamia hapa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambapo juzi kundi la wakazi
wa kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani humo, nalo lilikuja juu na
kutaka kuandamana kwa muda wa masaa kadhaa kupinga kusafirishwa kwa makaa ya mawe ambayo yanachimbwa kijijini humo.
Lengo la kutaka kufanya hivyo
lilitokana na wakazi hao kudai nyongeza ya fidia zao katika eneo ambalo
walihamishwa, kwa ajili ya kupisha kazi ya uchimbaji wa makaa hayo na kupinga
juu ya uchafuzi wa maji katika mto Nyamabeva ambao unafanywa na wachimbaji wa
madini hayo.
Maji ya mto huo yamekuwa yakitumika
na wananchi hao kwa shughuli mbalimbali majumbani mwao, lakini hivi sasa
wanashindwa kuyatumia kutokana na wachimbaji wa makaa hayo kutiririsha maji
yenye mkaa wa mawe kuelekea kwenye mto huo, na kusababisha baadhi ya viumbe
kama vile samaki kupoteza maisha ambapo serikali ya wilaya ya Mbinga baada ya
kupata taarifa hizo, ilichukua jukumu la kwenda huko na kuamuru wachimbaji hao
kuzuia maji hayo yasielekezwe katika mto huo.
Aidha kundi hilo lilikuwa likilalamika
kwamba vumbi kali la mkaa wa mawe limekuwa likienea katika vijiji vilivyokuwa
jirani na mgodi huo pale unaposafirishwa, ambapo walimtaka mwekezaji husika
aangalie namna ya kulidhibiti ili wananchi wasiweze kuathirika afya zao.
Hali ilikuwa tete ambapo kamati ya
ulinzi na usalama ngazi ya wilaya ikiongozwa na Mwenyekiti wake mkuu wa wilaya
hiyo Senyi Ngaga, ililazimika kwenda huko kumaliza mgogoro huo ambao ulionekana
kutaka kuhatarisha amani kati ya kampuni inayochimba mkaa huo, Tancoal Energy
katika mgodi wa Ngaka, uliopo kijijini humo na wananchi kwa ujumla.
Ngaga na kamati yake baada ya kwenda
huko Januari 29 mwaka huu, alifanya kikao na wananchi wa kijiji cha Ntunduaro katika eneo la ofisi ya
serikali ya kijiji hicho, na kuzungumza nao kwa kuwatuliza waache jazba wawe
watulivu wakati serikali, inaendelea na mchakato wa kuyashughulikia madai yao.
Pamoja na hayo licha ya mkuu huyo wa
wilaya ya Mbinga, kuwataka wananchi hao wafanye hivyo, bado wengine walionekana
kulalamika kwamba kilio chao kimedumu kwa muda mrefu, wakidai kwamba
wamechoshwa na ahadi ambazo hazizai matunda na utekelezaji wake unaonesha
ukifanywa taratibu.
Vilevile Ofisa mtendaji wa kata ya
Ruanda Matilda Nchimbi alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alisema mgogoro
huo wa wakazi kijiji cha Ntunduaro, unatokana pia na kampuni hiyo ya Tancoal
Energy kutokamilisha kwa muda mrefu kazi waliyoahidi ya ukarabati wa zahanati
ya kijiji hicho, ujenzi wa visima vya maji na shule, jambo ambalo limekuwa
likizua malalamiko miongoni mwa jamii.
Nchimbi alieleza kuwa tatizo lingine
ni kwamba madai ya wakazi hao wanataka majibu yatolewe haraka juu ya uchafuzi
wa maji ya mto Nyamabeva, ambao maji yake baada ya kuchafuliwa na mkaa wa mawe
wataalamu wa mazingira kutoka wilayani humo walikwenda na kuchukua kiasi kidogo
kwa ajili ya kuyafanyia uchunguzi wa kina, ili waweze kubaini madhara yake na
kwamba hadi sasa ni muda mrefu umepita hakuna majibu yaliyotolewa.
Hata hivyo alipoulizwa msimamizi wa
uchimbaji wa mkaa wa mawe katika mgodi huo wa Ngaka, aliyejitambulisha kwa jina
moja la Hemedi alisema yeye akiwa kama mwakilishi wa kampuni, amepewa jukumu la
kusimamia uchimbaji wa mkaa huo tu na hawezi kuzungumzia lolote juu ya
malalamiko hayo.
No comments:
Post a Comment