Wednesday, February 13, 2013

WAKULIMA WA KAHAWA WASHAURIWA KUZINGATIA KANUNI ZA KILIMO BORA







Meneja wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kanda ya Ruvuma, Edmond Zani. (Picha na Kassian Nyandindi).











Na Kassian Nyandindi,
  
MOJA kati ya zao kuu la biashara linalozalishwa hapa nchini na kuuzwa nje ya nchi ni kahawa, ambapo zao hili huwasilisha kiasi cha asilimia tano ya bidhaa zinazouzwa nje na kuchangia kiasi cha asilimia 24 ya mapato ya nchi yanayotokana na kilimo.

Kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita zao la kahawa limekuwa linaingiza kiasi cha zaidi ya dola milioni miamoja za kimarekani na kwamba ni chanzo cha kipato kwa familia zipatazo 450,000 na limekuwa likinufaisha maisha ya watanzania wapatao milioni 2.5.

Katika nchi yetu ya Tanzania asilimia 90 ya zao hili huzalishwa na wakulima wadogo, ambapo kwa ujumla wastani wa uzalishaji kwa mwaka tani za kahawa safi ni 50,000 ukiambatana na kupanda na kushuka kila baada ya mwaka mmoja kati ya tani 68,000 na 33,000.


Akizungumza na mwandishi wa makala haya Meneja wa bodi ya kahawa Tanzania (TCB) kanda ya Ruvuma, Edmond Zani anasema ili kuweza kuongeza uzalishaji na kuhakikisha ubora wa zao hilo unaimarika zaidi wakulima hawana budi kufuata kanuni za kilimo bora, zinazotolewa na wataalamu wa ugani.

Zani anasema, wamejiwekea mikakati ya kuhakikisha kwamba katika mkoa huo, mkulima wa kahawa anatunza shamba lake kwa kulifanyia usafi wakati wote ili kudhibiti wadudu waharibifu, magugu yanayo ota shambani na matumizi sahihi ya virutubisho kwenye udongo ili mche wa kahawa uweze kustawi vizuri.

“Magugu husababisha maficho mbadala kwa wadudu na magonjwa, ni muhimu kwa shamba la kahawa kuyang’oa kwa jembe au kutumia dawa za kuulia magugu”, anasema.

Anasema mche wa kahawa unachukua kiasi kikubwa cha virutubisho kutoka kwenye udongo, hivyo mbuni huo unahitaji virutubisho kwa ajili ya ukuaji na uzaaji ambapo kutokana na hilo wakulima wanaelimishwa kutumia matandazo ya nyasi ambayo yakioza yanaongeza rutuba kwenye udongo, kuzuia mmomonyoko na kutunza unyevu.

Vilevile anaeleza kwamba kanuni za kilimo bora cha kahawa ni pamoja na ukataji wa matawi mara baada ya mavuno kufanyika na kabla ya mvua kuanza.

Faida ya kufanya hivyo ni kuupa mbuni umbo linalotakiwa (Capping) ambalo huruhusu kupenyeza kwa mwanga, hewa ambavyo hupunguza uwezekano wa kujenga mazingira ya kukua kwa visababishi vya magonjwa na wadudu waharibifu.

“Katika mfumo huu wa kukata matawi katika shamba la kahawa, kunafanya kuwepo kwa uwiano sawa kati ya matunda na majani”, anasema Zani.

Zani anashauri wakulima kuondoa pia mashina yaliyozeeka shambani kwa kutumia mtindo wa kurengeta, ambao husaidia ukuaji wa maotea mapya yanayokuwa na mashina mapya.  

Anongeza kuwa ili kuweza kufikia malengo ya uzalishaji bora wa kahawa, serikali imekuwa ikiiwezesha taasisi ya utafiti wa zao la kahawa (TaCRI) ambayo inahusika na uzalishaji wa miche bora ya zao hilo, ambayo haishambuliwi na wadudu kwa urahisi.

Miche hiyo ambayo ni ya kisasa hujulikana kwa jina la Vikonyo, wakati wa mavuno imekuwa ikizalisha kilo 2 hadi 5 kwa mti mmoja wa kahawa ambao umetunzwa vizuri, tofauti na miche ya asili ambayo huzalisha chini ya nusu kilo au gramu 300.

Hivyo anasisitiza kwamba wakulima katika kanda ya Ruvuma wamekuwa wakihamasishwa mara kwa mara kutumia miche hiyo, ikiwa ni pamoja na kuboresha utunzaji wa kahawa, uchumaji, ukoboaji, uoshaji na uanikaji kwa kutumia vichanja.

Akizungumzia suala la uaandaji wa kahawa bora ngazi ya mkulima Zani anafafanua kwa kuanzia hatua ya uchumaji akisema, mkulima anatakiwa kuchuma matunda yaliyoiva ambayo ni mekundu.

Anasema mkulima hatakiwi kuchuma tunda lenye rangi nusu nyekundu, nusu njano au mchanganyiko wa kijani kibichi ambapo yakiwa yamechumwa kwa bahati mbaya, inashauriwa yatengwe kabla ya kuanza kumenywa katika mashine ili kuepusha kuharibu ladha na sura ya kahawa baadaye.

Hatua ya pili ni ya kumenya, ambayo mkulima anasisitizwa tunda la kahawa limenywe siku ile ile linapochumwa, ili kuzuia sukari iliyo kwenye ganda la nje haipenyezi ndani hadi kwenye punje, kwa kuwa itaharibu uonjo na kwamba katika zoezi hili  hushauriwa kutumia maji mengi na safi ili kuepukana na kuharibu punje ya zao hilo.

Kadhalika hatua ya tatu ni uvundikaji, hivyo husaidia kuondoa ute unaozunguka kila punje, ambapo kahawa iliyomenywa huvundikwa katika matanki yaliyo safi ambayo yametengenezwa kwa saruji na vifaa vya aluminiamu, chuma kama vile masufuria pia vinafaa na sio yaliyotengenezwa kwa mbao.

Mkulima vilevile anapofikia hatua ya nne ya kusafisha, hushauriwa kuendelea kutumia maji safi kwa kuhakikisha ute wote unaonatanata unaondolewa kwenye punje, na kuipanga kahawa iliyosafishwa katika madaraja huku akiondoa punje nyepesi na masalia ya maganda.

Meneja huyo wa kanda ya Ruvuma anaeleza kuwa kinachofuata  ni kuanika katika chekecheke zilizoinuliwa kiasi cha meta moja kutoka usawa wa ardhi, ambapo kahawa husambazwa katika chekecheke hizo kina cha inchi moja ili unyevu uweze kunyauka na baada ya hapo ikisha kauka vizuri, huhifadhiwa katika magunia yaliyosafi ili kuzuia isipate vumbi na kuhifadhiwa katika ghala ambalo lina nafasi ya kutosha kuruhusu mwanga na mzunguko wa hewa.

Pamoja na mambo mengine anasema kwenye ghala magunia ya kahawa hupangwa juu ya mbao zilizoinuliwa, ili yasigusane na ardhi na kuhakikisha ghala hilo halivuji maji na halina hali ya unyevu, ambao utaweza kuathiri punje za kahawa kavu zilizohifdhiwa katika magunia tayari kwa kupelekwa kwenye kituo cha mauzo.

“Mkulima anayezingatia kanuni hizi kwa umakini atakuwa amezalisha kahawa bora na kuitunza vizuri hivyo hujihakikishia bei nzuri, na kwa kuwa uzalishaji wa zao hili duniani huendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, njia pekee ya kuboresha mapato yetu ni kuongeza uzalishaji na kuendelea na jitihada za kuimarisha na kulinda ubora wa kahawa yetu”, anasisitiza Zani.

Binafsi nashauri kwamba ni vyema sasa wataalamu wa ugani hapa nchini, twende kwa mkulima na kumuelimisha juu ya utunzani na uzalishaji bora wa kahawa, ili tuweze kukuza uchumi wetu na pato la taifa kwa ujumla.

Itakuwa ni suala la kushangaza kuona tunaishia utaalamu wetu kuufanyia kazi katika mafaili yetu maofisini, wakati mkulima kijijini anateseka kwa kukosa utaalamu wa kilimo bora ambao ndio tegemeo la kuleta maendeleo katika nyanja hii ya kilimo.

No comments: