Na Steven Augustino,
Tunduru.
VIONGOZI na Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Kata Mpya ya
Majengo wilayani Tunduru Ruvuma, wamempongeza diwani wa kata hiyo Athumani
Nkinde, kwa kuwafungulia miradi zaidi ya shilingi milioni 1.2 iikiwa ni juhudi
za kuiendeleza kata yao.
Mwasisi wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilayani humo Neema
Chiwinga na Mwenyekiti wa kamati wa kikundi hicho Alus Chibwana ni miongoni mwa
viongozi waliotoa pongezi hizo, wakati wakitoa ushuhuda wa maendeleo ya kata
yao katika mkutano wa maadhimisho ya CCM kutimiza miaka 36 toka kizaliwe yaliyofanyika
kiwilaya katika kata hiyo.
Katika taarifa hiyo viongozi hao walimwelezea diwani
Nkinde kuwa ni miongoni mwa madiwani wanaotakiwa kuigwa mfano, wilayani humo
kutokana na upendo wake kwa wanachama na wakazi wote wa kata hiyo.
Alusi aliitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa kuuza kuni
na mkaa uliogharimu shilingi 750,000 na sasa wameongezewa mradi wa kilimo cha mpunga
utakaogharimu zaidi ya shilingi 400,000/ hadi kukamilika kwake na kwamba,
miradi yote inaendelea vizuri na wanaouhakika kuwa itawasaidia kuwaletea
maendeleo.
Upande wa vikundi vya Napasa na Cheleweni mjini hapa
wakimpongeza kwa njia ya nyimbo walidai kuwa diwani huyo, ambaye amewahi kuwa
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, kwa kipindi cha miaka mitatu aliweza
kuisaidia wilaya yao kwa moyo wa dhati ingawa kulikuwa na makundi ya watu
wachache wasioitakia mema wilaya yao walimpiga vita na kumuangusha katika
wadhifa huo.
Pongezi hizo ambazo pia ziliungwa mkono na Mwenyekiti
wa CCM wilaya ya Tunduru Hamisi Kaesa na mjumbe wake wa halmashauri kuu ya CCM
Taifa Ajiri Kalolo walimwelezea diwani Nkinde kuwa pamoja na wilaya
hiyo kushamiri sera za ubaguzi hasa kwa viongozi wasio kuwa wazawa wa wilaya
hiyo, lakini diwani huyo ni hazina na mfano wa kuigwa ndani ya chama hicho kwa
madai hata miradi aliyoianzisha na kuibuni kwa wanachama wake wa CCM haina hata
sababu ya kuendelea kulumbana.
Pamoja na viongozi hao kusisitiza mshikamano ndani ya chama
walikemea vikali tabia za ubaguzi kuwa zikiendelea ipo hatari ya kuiua wilaya
yao na chama hicho kwa ujumla, kwa madai kuwa hakuna mji ambao unaweza kujengwa
na kabila au wazawa peke yao na wakawataka watu wenye tabia hizo kujifunza
kutoka katika miji mingine yenye maendeleo kwa asilimia kubwa imejengwa na
wageni.
Katika mkutano huo diwani Athumani Nkinde alisema, pamoja
na kuwapongeza wanakikundi hao kwa kumpa moyo katika uendelezaji wa miradi hiyo
aliwahimiza kuitunza na kuienzi ili iweze kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Nkinde aliendelea kueleza kuwa lengo la kuwapatia
miradi hiyo ni kuonesha njia na mfano kuwa chama katika ngazi zote kinatakiwa
kuwa na miradi na kwamba ili kutimiza hayo chama katika ngazi zote kinahitaji
viongozi wabunifu na wenye uwezo wa kujituma ili kuonesha njia ya mafanikio kwa
wananchi wake.
No comments:
Post a Comment