Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WANANCHI wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameshtushwa na
kuwepo kwa wimbi la wasichana kutoka nje ya wilaya hiyo, wanaofika na kufanya
vitendo vya ukahaba katika mitaa mbalimbali nyakati za usiku huku wengine wakicheza muziki wakiwa nusu uchi kwenye nyumba za starehe maarufu kwa jina la Kangamoko, jambo
linalohofiwa kuongezeka kwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.
Ilielezwa kuwa kundi hilo la makahaba linadaiwa kutoka mikoa
ya Mbeya, Tanga, Dar es Salaam na miji mingine mikubwa wamekuja Songea kwa
ajili ya kufanya biashara hiyo ya ukahaba, ambapo ikifika majira ya saa tatu
usiku wamekuwa wakijipanga katika mitaa mbalimbali kutafuta wanaume.
Makahaba hao ambao wanalalamikiwa wanakadiriwa kuwa na umri
kati ya miaka 18 hadi 30 ambao wamekuwa wakifanya shughuli hiyo isiyo rasmi
hasa katika mitaa maarufu ya Delux, Serengeti, Majimaji na barabara ya Sokoine,
huvaa nguo fupi na nyingine zinazoonesha maumbile ya miili yao kwa lengo la
kutaka kuwavutia wanaume, ambao hujikuta wakiingia mtegoni bila kutarajia
kutokana na ushawishi unaofanywa na wasichana hao.
Wananchi hao walisema kuwa tabia inayofanywa na wasichana hao
haipaswi kufumbiwa macho, kwani licha ya kumdhahalilisha mwanamke lakini pia
inachangia maambukizi mapya ya ukimwi wakati serikali na wadau wengine wapo
katika mapambano ya kuzuia maambukizi mapya ambapo jamii imekuwa ikiaswa kuunga
mkono jitihada hizo kwa kuepuka vishawishi mbalimbali.
Aidha wameliomba Jeshi la polisi wilaya ya Songea, kuangalia
uwezekano wa kufanya msako mkali wa kushitukiza mara kwa mara katika mitaa hiyo
ili kuwakamata watu hao, kwani iwapo wataachwa kuendelea vitendo hivyo viovu, kuna
uwezekano mkubwa wa kuhatarisha jamii kuingia katika majanga ambayo
yatasababisha hata kudumaza shghuli za kimaendeleo.
Naye Siwajibu Athuman (34) mkazi wa Mjimwema alisema,
mwanamke kucheza muziki au ngoma yoyote akiwa nusu uchi ni fedheha na uzalilishaji, sio kwa yule tu anayeendekeza vitendo
hivyo bali ni kwa wanawake wote na kwamba aliitaka jamii kuungana katika kukomesha tabia hiyo ambayo imeshanza
kuota mizizi katika Manispaa ya Songea.
Hata hivyo msichana mmoja aliyefahamika kwa jina la Paulina
mkazi wa Majengo mjini hapa, aliiomba jamii kuacha
kushabikia na kufurahia vitendo hivyo, kwani licha ya kumdhalilisha mwanamke pia ni kwenda kinyume na
maagizo ya Mungu ambayo yanakataza tabia na matendo machafu.
No comments:
Post a Comment