Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
ULE mpango wa kutaka kuvunjwa kwa Kamati ya mipango na fedha katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, mapya yameendelea kuibuka ambapo
imeelezwa kwamba, ni mpango ambao umesukwa na vigogo wachache wa wilaya hiyo huku Madiwani wake wakiendelea kulalamika kutoshirikishwa juu ya suala hilo. Mtandao
huu unaripoti.
Taarifa za uhakika zilizotufikia leo zinaarifu kuwa, mkakati
huo wa kuvunja kamati hiyo huenda ukagonga mwamba kufuatia baadhi ya Madiwani kuja
juu na kueleza kwamba Katibu wao wa baraza la madiwani, Adolph Mandele ambaye
naye ni diwani wa kata ya Mpapa, ndiye anayewachanganya na kuwauza wenzake, akidaiwa
kutumiwa na vigogo hao (majina tunayo) kusuka mipango mibaya kwa lengo la kuhakikisha
vigogo hao wanafanikisha jambo hilo.
Mandele analalamikiwa kutengeneza muhtasari hewa ambao unaonyesha
kwamba wajumbe wa baraza hilo kwa maana ya madiwani wenzake, walikutana pamoja na
kuketi kupitia kikao cha dharula (CCM) na kukubaliana kufanya hivyo jambo
ambalo, madiwani wenzake wanamshangaa na kuanza kumjia juu wakisema sio kweli
anadanganya.
Wengi wanapinga vikali kuhusika katika kufanya kikao hicho,
ambapo Mandele alipofanya mahojiano na mwandishi wetu alithibitisha kwa kauli
yake akisema kikao hicho kilifanyika Desemba Mosi mwaka huu, katika ofisi za
makao makuu ya CCM wilayani Mbinga na madiwani hao walikubaliana juu ya
kuvunjwa kwa kamati hiyo.
“Jambo hili madiwani tulikwisha kaa kikao cha dharula na
mahudhurio niliyonayo pale ofisini tulikuwa madiwani 28, na mimi nimekwisha
andika muhtasari nimepeleka kwa mkurugenzi wetu kwa hatua zaidi”, alisema
Mandele.
Madiwani hao walisema baada ya kubaini hilo hata viongozi wa
chama hicho wilayani humo, wanaelezwa kumuuliza ni nani aliyemtuma kufanya
hivyo badala yake alishindwa kuweka bayana jambo hilo, na kuishia akisema kuwa
yeye alitumwa afanye hivyo na kuonekana dhahiri kuwa suala hilo linapikwa bila
kufuata taratibu kitendo ambacho kimefafanuliwa kuwa, kiongozi anayetumika kwa
mtindo huu kwa lengo la kuwasaliti au kuwavuruga wenzake ni hatari katika
jamii.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, umebaini kwamba
mchezo huo mchafu ni mpango ambao umesukwa na baadhi ya vigogo wa wilaya hiyo
(majina tunayo) ambao mnamo Januari 15 mwaka huu, walikutana pamoja nyumbani
kwa kigogo mwenzao (jina tunalo) na kuweka mikakati hiyo namna ya kuvunja
kamati hiyo kwa lengo la matakwa yao binafsi.
“Sisi tunamshangaa sana huyu Katibu wetu kufikia hatua ya
kutaka kutusaliti wanachama wenzake wa CCM (madiwani), anafikia hatua ya
kutengeneza taarifa hewa na kupeleka kwa mkurugenzi mtendaji kwamba tumekubaliana
kuvunja Kamati ya mipango na fedha wakati jambo hili halina ukweli, hafai kuwa
kiongozi huyu ni muuaji”, walisema.
Awali Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Mbinga, Hussein Ngaga
alishutumiwa na madiwani wake kwamba, mpango huo wa kutaka kuvunja kamati hiyo
amekuwa akiufanya chini kwa chini na tayari suala hilo, limefikishwa mezani
kwake kwa utekelezaji, katika kikao cha baraza la madiwani kinachotarajiwa
kuketi Januari 23 mwaka huu, wilayani humo kama alivyothibitisha Katibu huyo wa
madiwani.
Jambo hilo limethibitishwa pale mkurugenzi huyo alipovunja
ratiba za vikao vya kamati husika, ambapo hata baraza hilo ilibidi liketi
mwishoni mwa mwezi huu na sio tarehe hiyo, ambapo madiwani wake wameshangazwa kupangiwa
tarehe hiyo kufanya kikao cha baraza kinyume na ratiba husika inavyotaka.
Malalamiko hayo yametolewa na kufafanuliwa kuwa hakuna kikao
ambacho madiwani hao walikaa na kukubaliana kuvunjwa kwa kamati hiyo, ambayo
ndio mhimili wa kamati zote za baraza la madiwani.
Walisema kitendo hicho kinachofanywa, ni mpango mchafu ambao haupaswi
kuigwa katika jamii, na hili mkurugenzi huyo analifanya akidaiwa kutokana na wajumbe wachache waliomo ndani ya kamati hiyo
ya mipango na fedha, kuwa mwiba kwake na kutotaka kuburuzwa wakati wa kupitisha
mambo mbalimbali ya kimaendeleo ya wilaya hiyo, kinyume na taratibu husika.
“Leo anapotaka kuvunja
kamati hii maana yake ikishavunjwa, kamati zote tulizonazo ndani ya baraza hili
itabidi ziundwe nyingine upya, sisi tunashangaa sana hatuja kaa kikao chochote
kama madiwani na kukubaliana kupitisha maamuzi haya”, walisema.
Kadhalika waliongeza kuwa kuvunjwa kwa kamati hiyo, huenda
kanuni husika za baraza la madiwani hazitaruhusu kufanya hivyo kutokana na kile
walichoeleza kuwa baraza hilo linaelekea mwishoni kuvunjwa, tayari kuelekea
uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu wa kumchagua Rais, Wabunge
na Madiwani.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Mbinga, Ngaga wamemtaka kuwa makini
katika hili na azingatie kanuni husika, na endapo kama zinamruhusu kufanya
hivyo kabla ya yote ni muhimu akashirikisha kwanza madiwani wake, kupitia vikao
halali kabla ya kuleta maamuzi katika kikao cha baraza la madiwani.
No comments:
Post a Comment