Saturday, January 10, 2015

HALMASHAURI YA MBINGA YAINGIA KATIKA KASHFA MPYA, YALALAMIKIWA KUKUMBATIA FEDHA ZA MRADI WA MAJI KIGONSERA

Waziri wa maji, Profesa Jumanne Maghembe.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKAZI wa kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameutaka uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo  kurejesha haraka iwezekanavyo fedha zao za mradi wa maji wa kijiji hicho, ambazo zimekaa kwa muda mrefu na mradi kushindwa kuendelea kufanyiwa ukarabati.

Shilingi milioni 11.3 ambazo wananchi wa kijiji hicho walichangiana kwa ajili ya kuboresha mradi wao wa maji kijijini hapo, ndizo ambazo wanalalamikia na mradi huo wa wananchi umesimama kufanyiwa ukarabati kutokana na kukosa fedha.

Akitolea ufafanuzi juu ya fedha hizo, Mwenyekiti wa mradi wa maji katika kijiji hicho cha Kigonsera Izack Komba alisema baada ya kukamilisha kazi ya kuchangisha fedha hizo waliambiwa waziingize kwenye moja kati ya akaunti ya halmashauri ya wilaya hiyo, mpaka baadae watakapokamilisha kufungua akaunti yao ya mradi katika benki ya NMB tawi la Mbinga.

Mwenyekiti huyo alisema licha ya kukamilisha taratibu husika za kufungua akaunti katika benki hiyo, ni mwaka mmoja sasa umepita fedha hizo hazijaingizwa kwenye akaunti ambayo wameifungua katika tawi hilo, na wanashindwa kuendelea kufanya ukarabati wa mradi wao wa maji hapo kijijini na hivi sasa upo katika hali mbaya.

Mwandishi wa habari hizi ambaye alitembelea katika kijiji cha Kigonsera hivi karibuni, na kuzungumza na wananchi kwa nyakati tofauti ameshuhudia mradi huo wa maji ulivyo katika hali mbaya kwani chanzo kikuu cha kuleta maji kijijini hapo, ni kichafu na mabomba yamekuwa yakitoa maji machafu yenye tope.

Mradi huo ambao umefadhiliwa na shirika la fedha duniani (Wolrd Bank) na kusambazwa maji yake shuleni na baadhi ya nyumba wanazoishi wakazi wa kijiji hicho, huenda wakahatarisha afya zao kwa kupata magonjwa ya tumbo kama vile kuhara kutokana na kunywa maji machafu.

“Baada ya kuchangiana fedha hizi ambazo zililenga juu ya ufuatiliaji wa mradi huu, tuliona kutokana na mradi kutoa maji machafu basi ni vyema tutafute chanzo kingine mbadala cha maji kilichokuwa kizuri tukijenge kitaalamu ili tuweze kupata maji safi, lakini kila tukifuatilia fedha zetu kule halmashauri tunazungushwa kama watoto wadogo hatupati majibu yanayoeleweka”, walisema.

Mhasibu wa mradi huo Christa Mbelle naye alifafanua kuwa wananchi wanashindwa kuelewa hatma ya fedha zao ambazo walichanga, na kwamba wamekuwa wakiijia juu kamati husika ya mradi huo hapo kijijini ambayo ilihusika kukusanya fedha hizo kutoka mikononi mwa wananchi huku wakisumbuliwa mara kwa mara, itoe majibu sahihi juu ya fedha zao.

Mbelle alisema kuwa hawajui wafanye nini juu ya jambo hilo ambapo hata wanafunzi mashuleni katika Kata hiyo ya Kigonsera, wanapata shida namna ya kuyatumia maji hayo kutokana na kuwa machafu badala yake hulazimika kwenda kuchota katika vijito vidogo ambavyo huzunguka kata hiyo, ili waweze kuondokana na adha ya kunywa maji machafu ambayo yanaweza kuwaletea madhara makubwa baadaye.

“Sisi katika mradi huu wa maji tokea muda mrefu tulikuwa na akaunti yetu benki ya wananchi (MCB) hapa Mbinga, lakini wakati tunachangisha fedha hizi tuliambiwa na uongozi wa halmashauri kwamba hatuwezi kwenda kuweka fedha katika benki hii, tunatakiwa tukafungue NMB,

“Hivyo tulifuata maelekezo yao waliyotuambia na kwenda kufungua akaunti nyingine huko, lakini sasa ni takribani mwaka mmoja umepita hadi leo hii ninavyokuambia fedha za wananchi zimechukuliwa na halmashauri, hazijarejeshwa na kuingizwa kwenye akaunti hiyo mpya ambayo tumeifungua”, alisema Mbelle.  

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Hussein Ngaga hakuweza kupatikana ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo na simu yake ya mkononi, kwa muda mrefu ilikuwa haipatikani.

No comments: