Na Mwandishi wetu,
Songea.
JESHI la polisi mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na vyombo
vingine vya ulinzi na usalama limefanikiwa kukitambua kikundi cha mtandao
wa kigaidi ambacho kinadaiwa kujihusisha na majaribio matatu, ya
kuwashambulia askari polisi wakiwemo wa kikosi cha usalama barabarani
na tayari linawashikilia watuhumiwa kadhaa ambao majina yao
yamehifadhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kamanda
wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela alisema kuwa Jeshi la polisi limefanikiwa
kumtambua mtuhumiwa aliyelipukiwa na bomu hivi karibuni, pamoja na
mtandao wote unaojihusisha na matukio matatu ya kigaidi ya ulipuaji
mabomu, yaliyolenga kuwashambulia askari hao.
Alisema marehemu huyo jina lake limehifadhiwa, ambapo
imebainika kuwa ni mzaliwa wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, ambaye alizikwa
Desemba 31 mwaka jana baada ya Baba yake mzazi kujitokeza na kuchukua
mwili wa mtoto wake na kwenda kuuzika.
Alisema Marehemu huyo alikuwa ni miongoni mwa watuhumiwa
wa kikundi cha kigaidi ambapo tukio la kwanza wanatuhumiwa kuwarushia askari
polisi waliokuwa doria kwa bomu lilotengenezwa kienyeji Septemba 16 mwaka
jana katika eneo la Mabatini mjini hapa.
Tukio la pili lilitokea Oktoba 27 mwaka jana ambapo askari wa
kikosi cha usalama barabarani wakiwa katika eneo la Mshangano, walilopangiwa
kukagua magari walitegeshewa bomu ambalo baadaye liligunduliwa na askari
hao na kufanikiwa kuteguliwa kwa kushirikiana na Jeshi la wananchi, na kwamba
tukio la tatu lilitokea Desemba 25 mwaka jana wakati askari hao wakiwa doria
katika eneo la mtaa wa Majengo.
Alifafanua kuwa, katika matukio mawili yaliyotokea Mabatini
na Majengo askari wanne walijeruhiwa kwa mabomu hayo mpaka sasa
jeshi la polisi linawashikilia watuhumiwa kadhaa, na wengine wanaendelea kusakwa
ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.
“Jeshi la polisi limejipanga vizuri kuhakikisha
linawapata washiriki wote wa mtandao huu wa kigaidi waliokuwa wakishirikiana na
marehemu, ili kuweza kutokomeza wimbi hili la uhalifu katika mkoa
wetu wa Ruvuma na maeneo mengine ya nchi yetu, pia tunawaomba wananchi
waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuweza kuufichua mtandao
huu”, alisema Mihayo.
No comments:
Post a Comment