Humphrey Kisika. |
Mbinga.
KWA vyovyote iwavyo, mapigo ya moyo ya Mbunge wa Jimbo la
Mbinga mkoani Ruvuma, Gaudence Kayombo yataongezeka mara dufu baada ya kijana
msomi ambaye ni Afisa Habari wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Humphrey
Kisika (32) kutangaza nia ya kuwania ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Kisika ambaye ni msomi mwenye shahada ya kwanza ya uandishi
wa habari, pia ni mwanafunzi wa chuo Kikuu cha Iringa, anayesoma shahada ya
pili ya uandishi wa habari na utawala, anataka kuwania nafasi hiyo kupitia
chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na wanahabari kijijini kwake Ukata wilayani
Mbinga, alisema anataka kupokea kijiti toka kwa Mbunge huyo wa sasa, ili atumie
maarifa aliyonayo kusukuma zaidi maendeleo ya jimbo hilo.
Alisema anautambua na kuuthamini mchango wa mbunge wa sasa
katika kusukuma maendeleo ya jimbo hilo, lakini kuna haja akampokea kijiti
hicho ili aongeze kasi yake.
“Kipaumbele changu kitakuwa maendeleo kwanza
yatakayoshirikisha makundi yote ya jamii likiwemo kundi muhimu sana la vijana,
yatakayonufaisha wote,” alisema.
Alisema endapo nia yake hiyo itatimia, atahakikisha anaondoa
pengo linalodumaza maendeleo baina ya wataalamu ambao ni watendaji wa shughuli
mbalimbali za serikali, na wanachi ambao ni wapiga kura.
“Kumekuwepo na manung’uniko toka kwa wananchi, lakini
kimsingi manung’uniko hayo yanachangiwa na baadhi ya watendaji ambao kwa maslahi
yao binafsi au kwasababu ya kufanya kazi kwa mazoea, wanashindwa kuutumikia
vyema umma wa watanzania”, alisema.
Alisema CCM ina sera nzuri, huenda kuliko chama kingine kile
cha siasa ambazo hata hivyo yawezekana katika baadhi ya maeneo zimeshindwa
kutekelezwa ipasavyo, kwasababu ya uzembe wa wataalamu hao.
Akizungumzia muonekano wa kundi kubwa la vijana kuonekana
wakishabikia zaidi vyama vya upinzani kuliko chama chake cha CCM, Kisika
alisema katika mazingira ambayo nchi ina demokrasia ya hali ya juu kama
Tanzania, ni lazima wawepo vijana wanaopenda vyama vya upinzani.
Aidha alisema hiyo haina maana kwamba vijana wote wanavipenda
vyama vya upinzani, kwani chama cha mapinduzi inao vijana wengi na ndio maana
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) upo imara kuanzia ngazi ya tawi hadi Taifa.
“Ombi langu kwa vijana wenzangu, ni muhimu katika kipindi
hiki cha ushindani mkubwa wa kisiasa, tukafanya siasa kwa misingi ya upendo na
amani, tusikubali kutumiwa kwenye harakati za siasa chafu zitakazohatarisha
amani ya nchi hii ili iendelee kuwa kisiwa cha amani,” alisisitiza
Endapo ndoto yake hiyo itatimia, Kisika alisema wanambinga wategemee
maendeleo ya pamoja yatakayoletwa kupitia nguvu ya pamoja.
No comments:
Post a Comment