Padre Baptiste Mapunda. |
Na Padre Baptiste Mapunda,
WATAALAMU siku zote wanasema mwanzo mbaya huashiria mwisho mbaya, hivyo
basi kwa kauli hii mwaka huu 2015
Watanzania waishio Jijini Dar es Salaam
wameuanza vibaya kwa kutikiswa na kikundi cha “Panya Road.”
Siku ya tarehe moja Januari ya kila mwaka duniani husherehekewa
kama siku ya amani duniani, na amani hii tunayoitamka hapa ni ile inayotoka kwa
Mungu na siyo ya bunduki wala mabomu.
Baba Mtakatifu kila mwaka huwa anatoa ujumbe wa amani kwa
watu wote waliowakristo na wasiowakristo, mwaka huu ujumbe wake ulibeba kauli
ya “sasa hakuna mtumwa” kwani sote ni
kaka na dada.
Nilivyomwelewa Baba Mtakatifu Francis anamaanisha kwamba utumwa wa aina yeyote ile ni alama ya kukosekana kwa
amani moyoni, familia, jamii na dunia kwa ujumla wake.
Duniani tumwa ni nyingi mathalani utumwa wa mawazo, wa kukosa uhuru, haki za binadamu, utumwa wa
dhambi, wa kutawaliwa na hata ule wa umaskini. Watu wa jiji la Dar es Salaam mwaka
huu walianza na utumwa wa kukosa amani ya kutembea kwa uhuru na furaha, kwa
sababu ya ujambazi, uhuni na uhalifu wa
kikundi cha Panya Road.
Wakati wananchi wengi
wakilalamikia uhalifu wa panya road na
kuihoji serikali na jeshi la polisi lenye jukumu la kulinda amani ya raia na mali zao, Polisi jijini Dar es
salaam kupitia Kamanda wao Suleiman Kova
amekuwa akitoa majibu yanayokinzana.
Mara ya kwanza alisema kwamba, hiki ni kikundi cha vijana
wasiozidi kumi na tano hivi na wala hakina madhara kwa jamii.
Lakini baada ya siku chache kamanda huyo huyo, alisikika
anaripoti kwamba kulikuwa na vijana zaidi ya 500 wakijihusisha na kikundi hiki cha panya road. Na baadaye
kidogo ripoti ilisema sasa ni vijana
zaidi ya elfu moja wamekamatwa katika uhalifu wa panya road.
Kwanza neno lenyewe “Panya Road” nimekuwa nikijiuliza maswali
mengi maana yake ni nini, na msamiati huu umetungwa na nani, maana yake ni nini katika
jamii ya watanzania labda jeshi la polisi wangetupa asili ya neno hili, linatokana
na nini na lina ashiria nini?
Kitu cha kujiuliza neno panya, hawa ni viumbe wadogo tena
wenye woga mkubwa je, wanawezaje kuwatisha wanadamu wakiwamo polisi wenye ujuzi
na ukakamavu wa kushughulika na kulinda amani ya jamii?
Mbaya zaidi tumesikia pia jeshi la polisi likitoa tafsiri ya
Panya road kwamba ni vijana wavuta bangi, wazurulaji, waosha magari, vibaka,
wezi nakadhalika.
Vijana wazururaji ni wazururaji, na wavuta bangi nao
wanajulikana kwa uvutaji bangi, wezi wanaitwa wezi, waosha magari nao vile vile.
Ifahamike kwamba siyo kila kijana mzurulaji au mwosha magari au mvuta bangi ni mhalifu la hasha!
Polisi mtuambie panya
road ni nani, na mbaya zaidi inaonekana wazi kwamba baada ya kushindwa
kuwapata vijana panya road basi polisi waliamua kuwakamata vijana wa makundi yaliyotajwa hapo juu na
kuwafanya ndiyo wawajibike na uhalifu wa panya road. Je hii ni sahihi
kuunganisha vijana wote katika kundi la panya road?
Hii siyo sahihi, huku ni kutafuta majibu mepesi kwa maswali magumu, huu ni uzugaji na
uendelezaji wa sinema ambazo zimeendela kugonga mwamba kama ile ya mtekaji wa Dokta
Ulimboka, ambaye alisemwa na kamanda
Kova kwamba alikuwa ni Mkenya. Mimi naona kwamba Jeshi la polisi nchini linaendelea kuchezea amani ya Tanzania ambayo ni tunu kwa
taifa letu, iliyotoka kwa mwenyezi Mungu.
Mara nyingi imetokea katika nchi za Afrika kwamba, chama tawala kinapokaribia kupokonywa madaraka kwa sababu ya kuchokwa na
wananchi huwa kinaendekeza vikundi vya kihalifu
ambavyo baadaye vinaweza kutumiwa na watu wenye nia mbaya, kuharibu
shughuli ya uchaguzi mkuu.
Kule nchini Kenya kumekuwa na kikundi cha Mungiki, kikundi
cha vijana walioanza kama kimzaha mzaha kama kilivyo kwa hawa panya road,
wakakiiita kikundi cha vijana wahuni tu. Lakini baadaye kikundi hiki kilitumiwa na wanasiasa ili kudhuru na kuua wapinzani na wakosoaji wa
chama tawala hasa enzi za KANU chini ya Rais Arap Moi.
Leo ninaposikia ubabaishaji wa jeshi la polisi juu ya kikundi hiki maarufu kama panya road, naanza kuwa na wasi wasi mkubwa
juu ya utendaji wa jeshi letu la polisi hasa kuelekea uchaguzi mkuu. Hiki
kikundi mimi nakiona ni kikundi cha wahuni, majambazi na wahalifu ambao huenda wamefadhiliwa na baadhi ya watu wenye pesa ili kuweza kuwatisha wananchi, kuwajeruhi
na hata kuwaua raia. Hayo nayasema na
kuyaandika kutokana na maono
niliyoyadokeza wiki jana katika gazeti la Mwananchi pamoja na kusoma alama za
nyakati.
Sote tunafahamu kwamba mwaka huu mwezi wa Aprili, tutakuwa na
upigajikura wa maoni ya kuikubali au kuikataa katiba pendekezwa ya CCM. Mimi
kama nilivyoandika awali kwamba kura yangu
itakuwa ni ya “hapana, hapana, hapana” kwa sababu katiba pendekezwa hii
na ambayo naiona ni haramu ina kazi moja tu ya kulinda maslahi ya wanaccm hasa
viongozi wake.
Pia mwezi Oktoba watanzania tutakuwa na kazi nzito ya uchaguzi wa madiwani, wabunge pamoja na Rais mpya wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar. Sasa kuibuka kwa kikundi cha “panya
road” katika muda huu wa kuelekea
chaguzi hizi kunatia shaka juu ya usalama wa raia nchini na hasa wapinzani na wasokosoaji wa chama tawala.
Jeshi la polisi wamekuwa wanajigamba kwamba wana inteligensia
kali sana na weledi mkubwa katika utendaji waowa kazi, basi sasa watuambie
ukweli panya road ni nani na wanafadhiliwa na nani na kwa malengo gani?
Kuendelea kutoa majibu mepesi kama ni wahuni tu au ni magaidi au watu wasiojulikana, ni kuonyesha udhaifu mkubwa katika kulinda
amani ya raia na mali zao na hasa katika kipindi cha kampeni za chaguzi husika
ambazo tunakaribia kuzifikia.
Lazima ifahamike wazi kwamba endapo watu watajeruhiwa na kuuawa na amani kutoweka katika chaguzi
zijazo, basi ijulikane wazi kwamba Rais Kikwete na serikali yake ndiyo watakaowajibika
kwa maana ndiyo wenye dhamana ya kuiongoza na kuilinda nchi yetu.
Na ndiyo maana leo naandika na kusema bila hofu kwamba, “Jeshi la polisi acheni kuichezea amani ya Tanzania.”
Mwandishi wa
makala haya anapatikana kwa barua pepe; frmapunda91@gmail.com
No comments:
Post a Comment