Padre Baptiste Mapunda. |
Na Padre Baptiste Mapunda,
SERIKALI iliyopo madarakani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)
bado tumeshuhudia vituko vya hapa na pale, katika ulingo huu wa kisiasa huku ikijigamba
ndiyo inayoendesha mambo yake kwa kutumia demokrasia, na utawala bora.
La hasha, mfano mzuri ni ule katika kipindi cha kampeni,
upigajikura na utangazaji matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambao
umefanyika hivi karibuni Desemba 14 mwaka jana, CCM kilionekana kufanya rafu
kwa wapinzani wao wa kisiasa, ili kujihakikishia kinapata ushindi.
Chama hiki tawala kilionekana kutumia mbinu nyingi, kama vile
kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani katika maeneo mbalimbali hapa nchini,
kwa namna moja au nyingine ikiwemo hata wakati mwingine, kutumia vyombo vya
dola kama polisi ikiwa ni mbinu tu ya kutafuta ushindi.
Aidha baadhi ya matokeo katika vituo vya kupigia malalamiko
yalijitokeza kwamba yalibatilishwa, na sio hilo tu bali hata pale yalipokuwa
wazi kwamba wapinzani wameshinda bado
CCM haikukubali bali ulikuwa ni mwendo tu wa kulazimisha ushindi, kitu ambacho siasa
za namna hii zinaweza kuiingiza jamii katika vurugu au machafuko kama yaliyotokea
kule Kenya na sehemu nyinginezo.
Mbaya zaidi ni kile kitu cha kuwaapisha wagombea wengine ambao walikuwa wameshindwa
kupata kura za kutosha na wananchi wakibaki wanalalamikia, jambo ambalo dhahiri
linaonesha wazi kuwa bado ile dhana ya demokrasia huru ikiendelea kuminywa,
kila kukicha hasa nyakati za chaguzi mbalimbali.
Watanzania wengi hivi sasa walio na akili timamu na wapenda
amani, demokrasia na maendeleo wanachoshwa na vitendo hivi, ambavyo tunaweza
tukaviita ni “uhuni uliopindukia.”
Mimi najiuliza hivi kweli Chama Cha Mapinduzi, ni siku gani kinaweza
kushinda uchaguzi bila ghiliba, fitina, chuki, mizengwe, rushwa ya kura, uchakachuaji
matokeo au utumiaji wa nguvu ya vyombo vya dola?
Wahenga husema; siku za mwizi ni arobaini, maana yake ni siku
hiyo anayoshikwa hata kama itakuwa ya kumi na saba. Sasa naona mwisho wa
kutawala kwa chama hiki unakaribia, kwani ile propaganda yao ya “ushindi wa
kishindo” imeanza kujulikana walikuwa
wana maanisha nini?
Lakini pia kwa upande wangu siwezi kushangaa vituko hivyo vya mwaka, kwa sababu hii yote
ni alama ya kufilisika kimawazo na sera.
Mimi nakumbuka kama mchezaji wa mpira wa mguu mara nyingi timu
yetu tukiona inaelekea kushindwa na muda
unapita, sasa kinachobaki ni kukata mtama kila mpinzani wetu anayekaribia goli
letu. Yaani hapo sasa ni “mchezo wa bora liende” ni upiga juu, piga nje basi
kwa maana sasa hakuna matumaini tena ya kushinda.
Basi naona ndivyo na yalivyo mambo ndani ya CCM kwa sasa, alama
za wananchi kuamka na kujua wanachotaka zimeonekana kupitia uchaguzi wa
serikali za mitaa. “Nyota ya asubuhi imewaangazia wananchi maskini wa
Tanzania.” Mungu naye yupo upande wa maskini na wanyonge, basi ameamua kuwatia
nguvu watu wake akiwatuliza kwamba, “mimi
ni Mungu wenu, msiogope, nitawakomboa tu.”
Wanaccm wenye upeo wameona upepo umebadilika ila wanaogopa
kuwatonya na wenzao kwa sababu walio wengi, bado hawakubali kama watanzania wa
leo wamebadilika. Walio wengi wanaendelea kujidanganya kwamba mtanzania bado
mjinga, mpumbavu, zezeta na waoga wa kudai haki zao, zama za kufikiri haya umepita.
Ndiyo maana nionavyo mimi, wanaona wanaweza tu kuapisha “wagombea wao walioshindwa” na kuendelea kutawala au
kuongoza wakisahau kwamba uchaguzi ndiyo
msingi wa upatikanaji wa viongozi bora katika jamii kidemokrasia. Ni makosa
kuwachagulia wananchi viongozi na mbaya zaidi kuwalazimisha wananchi kuongozwa
na viongozi ambao siyo ridhaa yao.
Lakini kwa upande mwingine, mimi naona ni mojawapo sehemu ya
“mnara wa Babeli” na pia ni utabiri wa Askofu mkuu Zakary Kakobe wa kanisa la Kipentekoste Full Gospel, itakumbukwa kwamba mwezi marchi 2013 Askofu huyo alitabiri
kusambaratika kwa serikali ya chama hiki tawala, mithili ya mnara wa Babeli.
Kakobe akiwa ni mtumishi wa Mungu, mimi siwezi kumdharau kwani
Mungu ana njia zake za kufikisha ujumbe kwake tofauti na tunavyofikiria sisi
wanadamu. Unapoona jinsi makundi
yanavyojipamba au kupasuana, wakati wa kuteua mgombea wa urais basi unaweza
kutambua maana ya utabiri ule wa Askofu Kakobe.
Utabiri wa Askofu mkuu Kakobe, ulikuwa ukisema msambaratiko
ndani ya CCM utatokea hatua kwa hatua na hili tunaendelea kuliona kila kukicha. Yesu aliwaambia wasikilizaji wake kwamba, utawala uliogawanyika haufai, kama
uongozi umegawanyika basi utawezaje kuwaunganisha wananchi?
Ndani ya Chama cha mapinduzi hivi sasa kuna makundi kibao, na
kila kundi likijigamba kuwa na mgombea wao ambaye wanataka apeperushe bendera wakati wa kampeni
mwezi Oktoba, tamaa ya urais imekuwa ni kubwa mno.
Enzi za Mwalimu Julius Nyerere, nakumbuka kwamba ilikuwa mtu
kujitangaza tangaza magazetini, katika luninga, radio na katika majukwaa ya
kisiasa na wengine hata kwenda katika nyumba
za ibada isingewezekana. Kiongozi wa kweli anapendekezwa na wananchi na siyo
kujipendekeza. Hakuna mtu anayeweza kujifanya mwenyewe kama kiongozi wa watu, bali
anachaguliwa na watu wanaomuona anafaa kuwaongoza.
Hata hivyo kutokana na minyukano ya makundi hayo ndani ya chama
hicho, kila kundi linajitahidi kujipigia debe na kuwaponda wenzao kwa kadiri
liwezavyo na sasa hata kuna baadhi ya wazee, maarufu ndani ya chama kama Mheshimiwa
Kingunge aliyejitokeza na kusema kwamba, wote waliotangaza kuwania urais hakuna
mwenye sifa hata mmoja.
Inawezekana kabisa mzee Kingunge yupo sahihi, sasa kama
hakuna hata mmoja bado watanzania mzee
wetu ametusaidia kutoa elimu ya urais, naiona
kauli yam zee huyu ni ya kinabii na ya kimapinduzi kuelekea uchaguzi
mkuu, Oktoba mwaka huu.
Maovu yanayoendelea kujitokeza katika siasa kuelekea uchaguzi
mkuu hakika mimi nasema yatupasa tubadilike na kuyaacha ikiwemo hata yale ya
kihuni, kiharamia, kijasusi na ya kijambazi ndiyo maana nathubutu kwa kutumia
safu hii kuwaelimisha watanzania wenzangu; Mungu atuepushe na maovu kuelekea
uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Mwandishi wa
makala haya anapatikana kwa barua pepe; frmapunda91@gmail.com
No comments:
Post a Comment