Kassian
Nyandindi,
Songea.
OFISI ya Chama Kikuu Cha Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT) mkoani
Ruvuma, imeingia katika kashfa mpya baada ya uongozi wa chama cha kuweka na
kukopa, Kihulila juu SACCOS wilaya ya Mbinga mkoani humo, kuishushia lawama
kwamba imeshindwa kushughulikia lalamiko lao kwa muda mrefu la kurejeshewa,
shilingi milioni 3,122,000 baada ya kujitoa uanachama miaka mingi iliyopita.
Walisema licha ya ofisi hiyo kuwa na taarifa kamili juu ya
jambo hilo na ufuatiliaji wa madai hayo, kuanza kufanyika tokea Februari 16 mwaka
2010 na SACCOS hiyo ilipojitoa uanachama kwa hiari, Desemba 30 mwaka 2008
hakuna jitihada zilizozaa matunda mpaka sasa.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake Katibu wa idara ya
mikopo Kihulila juu SACCOS, Kelvin Ndunguru alisema kawaida tokea siku
walipojitoa uanachama, baada ya siku 90 ilibidi SCCULT warejeshe mafao yao yaliyotokana
na michango mbalimbali waliyokuwa wakichangia.
Ndunguru alifafanua kuwa tatizo hilo lipo hata mezani kwa Mrajisi
msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo, na viongozi wengine wa wilaya ya
Mbinga, lakini hakuna majibu sahihi wanayopewa juu ya madai hayo huku siku
zikiendelea kupita.
Vilevile alieleza kuwa wanachama wa SACCOS hiyo hawauelewi
uongozi wa ushirika uliopo madarakani mkoani Ruvuma, juu ya mwenendo wa suala
hilo unavyotekelezwa huku wakidai kwamba fedha zao zipo nje ya chama chao kwa
muda mrefu jambo ambalo, linasababisha kuzorota kwa maendeleo yao na chama kwa
ujumla.
“Mpaka nafikia hatua ya kukaa na wewe kukueleza jambo hili,
bodi ya uongozi wa chama chetu cha kuweka na kukopa tulikaa kikao na kuridhia
malalamiko yetu haya tuyafikishe hata kwenu waandishi wa habari, ili kilio
chetu serikali ikisikie na kukifanyia kazi huenda tukapata haki yetu ya msingi
kwa sababu tumelalamika maeneo mengi hakuna tuliposikilizwa”, alisema.
Alisema kuwa pamoja na kuandika barua nyingi za kukumbusha
juu ya suala hilo na kuzipeleka katika ofisi husika (nakala tunazo) wanaiomba
serikali, kupitia Wizara yake ya kilimo chakula na ushirika kuingilia kati ili
waweze kupata fedha zao ambazo wanaendelea kudai miaka mingi sasa imepita.
Pamoja na mambo mengine, gazeti hili inayo barua yenye
kumbukumbu namba SCCULT/RUR/KHJ/VOL 1/31 ya Februari 23 mwaka 2012, yenye
kuonyesha inatoka kwa Meneja mkuu wa mkoa wa Ruvuma (SCCULT) ikikiri kudaiwa
madai hayo na Kihulila juu SACCOS huku nakala ikipelekwa kwa Katibu mtendaji wa
chama hicho kikuu cha akiba na mikopo Tanzania na Mrajisi msaidizi wa vyama vya
ushirika mkoani humo kwa utekelezaji zaidi, jambo ambalo limekaliwa kwa muda mrefu huku likiendelea kuleta
sintofahamu miongoni mwa wanachama.
Barua hiyo ambayo inakubaliana na madai hayo inasema, “ni
kweli kwamba Kihulila juu SACCOS ilikuwa mwanachama na mshiriki mzuri wa
maazimio ya mikutano mikuu ya SCCULT na iliamua kujitoa uanachama wa hiari, kwa
barua ya kwanza ya Desemba 30 mwaka 2008,
“Kufuatia maombi hayo ya kujitoa uanachama katika mkutano
mkuu wa SCCULT uliofanyika mkoa wa Mtwara, Februari 16 mwaka 2010 waliridhia
ombi hilo “, inasema barua hiyo.
Aidha uchunguzi umebaini kuwa kwa kuzingatia sheria ya
ushirika baada ya wanachama kuridhia kujitoa uanachama, SCCULT walikuwa na
wajibu wa kuandaa malipo stahiki ya SACCOS hiyo kwa mchanganuo ufuatao; ambapo Akiba
na faida ya juu ilikuwa walipe shilingi milioni 2,717,080.00, Hisa shilingi 345,000.00
na Ada ya mkopo ilikuwa shilingi 60,000.00 na kufanya jumla kuu ya deni
wanalodaiwa kuwa ni shilingi milioni 3,122,080.00.
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma, Fausta
Kasuga hakuweza kupatikana ili aweze kutolea maelezo ya kina juu ya madai hayo
ya chama cha kuweka na kukopa, Kihulila juu SACCOS kilichopo wilayani Mbinga.
Hata hivyo jitihada ya kumpata Meneja wa mkoa wa Ruvuma, wa Chama
Kikuu Cha Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT) Hezron Luvanda kwa njia ya simu ili
naye aweze kuzungumzia malalamiko hayo, zilifanikiwa ambapo alikiri juu ya
wanachama wa SACCOS hiyo kudai fedha hizo.
Luvanda alisema “mimi nimekwisha acha kazi sipo Ruvuma, na
ofisi yetu hapo imefungwa siku nyingi, hakuna mtu wakuweza kukupatia ufafanuzi
juu ya jambo hili”.
No comments:
Post a Comment