Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. |
Ruvuma.
BAADHI ya Madiwani na Wadau wa elimu wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, wameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) kuacha kufumbia macho tatizo la mgogoro uliopo kati ya
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein Ngaga na baadhi ya
watumishi wake wa idara ya elimu msingi huku wakieleza kuwa hatua
zisipochukuliwa mapema huenda wilaya hiyo ikarudi nyuma kimaendeleo, hususani
katika sekta ya elimu ambayo wilaya inaonekana kwa sasa ikifanya vizuri.
Wadau hao wameinyoshea kidole ofisi ya TAMISEMI wakidai kuwa,
imekuwa ikimbeba Mkurugenzi huyo licha ya matatizo yaliyopo hapa wilayani
kuwafikia.
Aidha walisema kuwa Ngaga amekuwa chanzo cha migogoro kazini,
ambapo muda mwingi haelewani na baadhi ya watumishi wenzake, hususani wa idara
ya elimu msingi.
Imedaiwa kuwa matatizo hayo yapo mezani kwa viongozi wa
TAMISEMI ikiwemo hata kwa Katibu Mkuu, Jumanne Sagini lakini wanashangaa kuona
kutochukua hatua madhubuti ikiwemo kumwajibisha mkurugenzi huyo, ambaye sasa
amekuwa kero kwa madiwani hao na wananchi wa wilaya hiyo.
Walisema ni wakati sasa kwa ofisi hiyo kuchukua hatua na sio
kukaa kimya, ukizingatia kwamba kilio cha wanambinga juu ya kukerwa na migongano
kazini ambayo anaiendekeza mkurugenzi huyo, imedumu kwa muda mrefu.
Hivi sasa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, imekuwa ikiyumba
kimaendeleo hususani katika sekta ya elimu ya msingi ambapo mkurugenzi mtendaji
wa wilaya hiyo Ngaga analalamikiwa na madiwani wake kuchukua hatua ya kumsimamisha
kazi afisa elimu msingi, Mathias Mkali bila kuzingatia taratibu za kiutumishi
wa umma ikiwemo hata baraza lake la madiwani lililoketi mara ya mwisho, Oktoba
27 mwaka jana halikumtuma afanye hivyo.
Nimezungumza na baadhi ya Madiwani wa wilaya hiyo walisema,
Ngaga amekuwa akichukua maamuzi peke yake kwa kudharau maagizo yanayotolewa na
baraza la madiwani kupitia vikao halali, na hata wakati mwingine amekuwa
akifikia hatua ya kubadilisha mihtasari ya makubaliano husika ya vikao vya
kamati mbalimbali, kwa malengo yake binafsi.
Walisema hivi karibuni kamati za madiwani ambazo zimekuwa
zikiketi katika vikao vyake, wajumbe wameshangazwa na mkurugenzi huyo muda
mwingi baadhi ya mambo yaliyokuwa yamejadiliwa na kujenga makubaliano, yeye huyabadilisha
na kuweka mambo tofauti na makubaliano husika hatimaye ndani ya vikao
husababisha kurushiana maneno na watu kujengeana chuki pasipokuwa na ulazima.
Ambapo walitolea mfano kuwa, katika kikao walichoketi Novemba
25 mwaka jana cha kamati ya mipango na fedha, Ngaga alileta muhtasari kwa
kamati hiyo ambao ulikuwa ukieleza kuwa Waratibu elimu kata haikupitishwa na
baraza kwamba wapewe mafuta, jambo ambalo wajumbe walimshangaa na kumweleza sio
kweli bali baraza hilo lilikubaliana wapewe ili waweze kuweka kwenye pikipiki zao,
ziwarahisishie waweze kufanya ufuatiliaji wa mazoezi ya mitihani kwa wanafunzi
wa darasa la saba katika kata husika, ikiwa ni lengo la kuboresha taaluma
wilayani humo.
“Baada ya mkurugenzi huyu kumkosoa kwenye jambo hili
alionekana kuwa mkali huku akitutishia kwa maneno makali na kulazimisha
tupitishe mambo anayoyataka yeye, mjumbe mwenzetu mmoja aliamua kutoka nje ya
kikao baada ya kushindana kwa muda mrefu na kutofikia muafaka”, walisema.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga
Hussein Ngaga alipotafutwa ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo,
hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa
na imekuwa ni tabia yake ya kutopokea simu, na kukataa kuhojiwa au kuzungumza na
waandishi wa habari pale panapokuwa na tatizo katika halmashauri hiyo.
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Jumanne Sagini juu ya ofisi
yake kama inalifahamu suala hilo kama madiwani hao na wadau mbalimbali wa elimu
wanavyodai alisema, kuhusiana na madai kwamba ofisi yake inambeba mkurugenzi
huyo alikana huku akiongeza kuwa endapo anasikia kama kuna mtumishi yeyote wa
serikali za mitaa ambaye anakiuka maadili ya utumishi wa umma, yupo tayari
kumwajibisha kwa namna moja au nyingine.
Pamoja na mambo mengine alionyesha kushangaa na kuwalaumu madiwani wa
Mbinga na kusema kuwa, wao ndio wenye rungu na mamlaka kupitia vikao vyao baraza
la madiwani, wanaweza kumwajibisha mkurugenzi huyo pale wanapoona anakosea na kuipeleka
wilaya yao vibaya tofauti na maadili ya utumishi wa umma.
“Nakuambia ofisi yangu haiwezi kumuacha mtumishi wa namna
hiyo, hao wanaosema kwamba mkurugenzi wa Mbinga mimi nambeba sio kweli,
nikibaini kuna mtumishi anayekiuka taratibu husika nitambamiza tu, siwezi
kumuacha na sijawa na mtu ambaye ninambeba”, alisema Sagini.
Kadhalika alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya ofisi yake
kama inafahamu juu ya matatizo haya yanayoendelea sasa wilayani Mbinga, alisema
hana nafasi ya kuweza kuongea kwa muda mrefu kutokana na kubanwa na vikao huku
akimtaka mwandishi wetu, ampigie kwa muda mwingine ili aweze kutolea ufafanuzi
zaidi.
“Ndugu yangu nakutakia siku njema, naomba nitafute leo majira
ya saa 10 tuweze kuzungumza zaidi juu ya jambo hili, hapa nilipo naingia kwenye
kikao nimebanwa kwa kweli, aliishia kukata simu”, alisema.
No comments:
Post a Comment