Saturday, January 10, 2015

WAFANYABIASHARA MBINGA WALALAMIKIA SERIKALI KUPANDISHA KODI YA MAPATO

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
CHEMBA ya Wanyafabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imeshangazwa na kitendo cha serikali kupandisha kodi kwa asilimia miamoja huku ikielezwa kuwa ongezeko hilo halilingani na ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo ni vyema mahesabu hayo ya kodi ambayo yalipitishwa na Bunge yakaangaliwa upya na kufanyiwa marekebisho, ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara yanayoendelea kujitokeza miongoni mwa jamii.

Aidha walihoji ni kiwango kipi kilitumika na serikali kukokotoa na kuweka ongezeko hilo ambalo ni kubwa, wakati wakijua fika hali ya uchumi wa nchi kwa sasa sio nzuri na kwamba kufanya hivyo ni sawa na kuwaumiza wafanyabishara, hasa kwa wale wenye mitaji midogo.

Hayo yalisemwa na wafanyabiashara hao, katika kikao cha pamoja walichoketi kwenye ukumbi wa chuo cha maendeleo ya wananchi (FDC) mjini hapa, na kuhudhuriwa na Afisa msemaji mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Hamis Lupenja, ambaye alikuwa akimwakilisha Kamishna mkuu wa mamlaka hiyo hapa nchini.

Philemon Msigwa ambaye ni afisa mtendaji mkuu wa TCCIA wilayani humo, alisema wafanyabiashara wa wilaya hiyo kwa muda mrefu wamekuwa pia wakilalamikia kodi ya mapato wanayolipa hapa Mbinga ni kubwa, kutokana na makampuni yanayofanyabiashara wilayani humo kulipa kodi nje ya wilaya hiyo.

Alisema katika kumpunguzia mfanyabiashara wa wilaya ya Mbinga mzigo mkubwa wa kulipa kodi ya mapato, ni vyema serikali kupitia mamlaka husika ikaweka utaratibu wa kuyabana makampuni hayo yalipie wilayani humo, ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

“Sawa tunajua sheria inasema ulipaji wa kodi kwa kampuni yoyote ile inaruhusiwa kulipa makao makuu ya kampuni husika, lakini sisi kama jumuiya ya wafanyabiashara hapa Mbinga tunaiomba serikali itusaidie jambo hili, kwa sababu hawa wenzetu wanafanyabiashara ya kununua kahawa kwa wingi na makaa ya mawe yanachimbwa kule katika kata ya Ruanda lakini mzigo wa kulipa kodi tunaachiwa sisi wafanyabiashara wadogo,

“Hesabu za kodi kwa makampuni haya yanayolipa kodi ya mapato nje ya wilaya hii, ni vizuri zirudi sehemu waliyonunulia bidhaa na kuweza kufidia pengo la ulipaji kodi, wafanyabiashara wa Mbinga tunabeba mzigo mkubwa wa kodi wakati kuna wafanyabiashara wakubwa wanaolipa kodi nje ya Mbinga huku wakiendelea kufanyabiashara hapa kwetu”, alisema Msigwa.

Vilevile Benedict Luena aliongeza kuwa hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangia utoroshaji wa mapato ya wilaya, hivyo kuna kila sababu kwa serikali ikaridhia ulipaji wa kodi zao ukafanywa hapa wilayani kwa makampuni hayo, kwa lengo la kuongeza mapato ya ndani na taifa kwa ujumla.

Naye mfanyabiashara, Marietha Mponda alieleza kuwa viwango vipya vya ulipaji kodi vilivyowekwa na bunge ambavyo utekelezaji wake unapaswa kufanyika kuanzia sasa, wamevipokea kwa shingo upande na kwamba kuna kila sababu kwa waliohusika kupitisha suala hili (Wabunge) waone ni namna gani wanalifanyia tena upembuzi yakinifu ili kuondoa malalamiko ambayo yanaendelea kujitokeza kwa nchi nzima.

Kadhalika mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Osmund Kapinga alisema, kupanda huku kwa kodi ya mapato kunasababishwa na wataalamu husika wa mamlaka ya mapato nchini kutengeneza hesabu za juu bila kushirikisha wadau husika, yaani wafanyabiashara ambao wangeweza kutoa ushirikiano wa karibu kabla ya kupelekwa bungeni.

Kapinga alifafanua kuwa katika jambo hili ni sawa na mamlaka hiyo imetumia ubabe, wakati wanatengeneza viwango hivyo vipya na ndio maana leo vinaumiza wananchi na kusababisha kuichukuia serikali yao.

“TRA tumewasikia hapa mkisingizia wabunge ndio walioweka viwango hivi na kupandisha kodi ya mapato, lakini nataka niwaambie ukweli ni kwamba ninyi watu wa mamlaka ya mapato ndio mnao husika katika kuandaa viwango hivi na baadae vinapelekwa bungeni, hapa tusifike mahali tunadanganyana kama watoto wadogo”, alisema.

Awali akijibu hoja za wafanyabiashara hao wa wilaya ya Mbinga, Afisa msemaji mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Hamis Lupenja alisema, kilio hiki cha ongezeko la kodi ya mapato ambacho wanambinga wanakipigia kelele tayari hata kwa mikoa mingine hapa nchini wanakifahamu na kwamba mfumo huu wa sasa wa serikali kuingia kwenye viwango maalum vya ulipaji wa kodi, ulitokana na wafanyabiashara wengi kutokuwa na mazoea ya kutunza kumbukumbu (vitabu) vya mahesabu ya biashara wanayofanya kwa kila siku.

Lupenja alisema, viwango vipya vya kodi ambavyo vimewekwa na bunge ni muhimu kuzingatiwa na vianze kutekelezwa mpaka serikali kupitia bunge lake itakapotoa maamuzi mengine.

Hata hivyo kuhusiana na suala la makampuni makubwa yanayofanyabiashara wilayani humo, na kulipia kodi nje ya wilaya hiyo aliahidi atakwenda kulifanyia kazi na utekelezaji utafanyika ili kuweza kuweka utaratibu wa kuanza kulipia ndani ya wilaya hiyo.

No comments: