Gaudence Kayombo. |
Ruvuma.
WAFANYABIASHARA wa wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametishia
kutomchagua tena Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Gaudence Kayombo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi
Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, kwa kile walichodai kwamba ameshindwa
kuwatetea Bungeni na badala yake ameunga mkono ongezeko la kodi la asilimia
100.
Aidha walisema Mbunge huyo mara kwa mara wanapomtaka
azungumze na wafanyabiashara hao kupitia vikao mbalimbali, kwa lengo la
kusikiliza kero zao amekuwa hajitokezi huku wakidai amekuwa akitoa sababu
nyingi kwamba amebanwa na majukumu.
Hayo yalijiri walipokuwa wakizungumza kwenye kikao cha
wafanyabiashara hao kilichoketi kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (FDC)
mjini hapa, na baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka
makao makuu ya mamlaka hiyo na mkoa huo, mmoja wa wafanyabiashara hao, Benedict
Luena alisema wameumizwa na Mbunge wao kushindwa kuwatetea kuhusu suala hilo.
“Hatukumtuma bungeni kwenda kulala, bali kutuwakilisha
kutokana na kutugeuka nasi tumejipanga kumwajibisha kwa namna yoyote ile,
ikiwemo hata kumwangusha katika uchaguzi ujao kwani hatuwezi kuwa na mbunge
asiyejali kero za wananchi wake,” alisema Luena.
Mfanyabiashara mwingine, Ally Mbunda alisema kwa muda mrefu
wamekuwa wakiomba kukutana na mbunge huyo ili waweze kuzungumzia kero zao zinazowasumbua,
lakini amekuwa akisema amebanwa na majukumu mengine.
Kayombo alipohojiwa kwa njia ya simu, alikiri kusikia
malalamiko hayo lakini akashangazwa na taarifa hizo akisema, tangu kikao kilipomalizika
hakuna viongozi wala wafanyabiashara waliomfuata kumweleza hatua zilizofikiwa
juu ya kikao hicho.
Alisema anashangaa kwa nini malalamiko hayo yanatokea kipindi
hiki cha kampeni, “siyo wafanyabiashara peke yao wanaopiga kura, kwanza sheria
inapitishwa na wabunge wote na inatumika nchi nzima hivyo sioni haja ya wao
kuniadhibu”, alisema Kayombo.
No comments:
Post a Comment