Dkt. Joachim Henjewele. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kwamba, hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi
katika Halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
inaendelea kukua kwa kasi ambapo hivi sasa kwa pamoja halmashauri hizo zimekuwa
zikiongoza kwa asilimia 9.6 ya maambukizi ya ugonjwa huo, ukilinganisha na
kiwango cha mkoa huo ambacho ni asilimia 7.2.
Takwimu hizo zimetolewa katika kipindi cha miezi sita kuanzia
mwezi Oktoba mwaka jana hadi Machi mwaka huu, ambapo jumla ya watu 2,890
waliweza kupimwa na kwamba waliogundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo
kati ya hao walikuwa ni watu 278.
Hayo yalisemwa na Dkt. Joachim Henjewele ambaye ni Meneja
Mkuu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Health Promotion Tanzania (HDT)
lililopo mjini hapa, ambalo linajishughulisha na udhibiti wa maambukizi mapya
ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) ndani ya halmashauri hizo wakati alipokuwa
akizungumza juzi na waandishi wa habari ofisini kwake.
“Kwa picha hii hali ya maambukizi Mbinga bado ipo juu
ukilinganisha na kiwango cha mkoa huu ambacho ni 7.2 na kitaifa ni 5.1 hivyo
jitihada za kuendelea kuelimisha jamii ili iweze kuepukana na maambukizi mapya
ya Virusi vya ukimwi inahitajika kwa kiasi kikubwa”, alisema Henjewele.
Katika maambukizi hayo Dkt. Henjewele alifafanua kuwa makundi
yanayoongoza kuwa na maambukizi ni makundi ya wanawake wanaofanya biashara ya
ngono ambayo maambukizi yake yamefikia asilimia 18, kundi la mme na mwenza wake
asilimia 15.8 na mwisho ni kundi maalumu la wasichana wanaofikia umri wa
kubalehe lenye asilimia 11.7.
Henjewele alisema kuwa maeneo yanayotisha kwa maambukizi
katika eneo la halmashauri ya mji wa Mbinga ni kata ya Mbinga mjini A na B,
Masumuni, Betlehemu, Mpepai na Mbambi.
Kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga maeneo
yanayoongoza kuwa ni kata ya Mapera, Ruanda, Amani makolo, Langiro, Kihangi
mahuka, Mkako na Amani makolo.
Alieleza kuwa zoezi hilo la upimaji linatekelezwa kwa
kuwatumia watoa huduma za magonjwa majumbani, waelimishaji rika, upimaji wa
nyumba kwa nyumba na upimaji wa mme na mwenza wake.
Hata hivyo shirika la HDT aliongeza kuwa limekuwa likifanya
kazi kwa kata 25 ambapo halmashauri ya mji wa Mbinga limekuwa likifanya kazi
zake kwa kata 10 na wilaya ya Mbinga kwa kata 15 ambazo zina maambukizi makubwa
ya VVU.
No comments:
Post a Comment