Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye akihutubia katika mkutano wa wadau wa kahawa uliofanyika juzi mjini hapa. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MAKAMPUNI yanayonunua zao la kahawa katika halmashauri
ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma yamepigwa marufuku kuhifadhi
zao hilo kwa kutumia maturubai, badala yake wanapaswa kuhifadhi kwenye maghala
ili kuweza kudhibiti ubora wake.
Vilevile agizo limetolewa kwamba ili kuweza kuendelea kuongeza
ubora wakati wa mavuno ya zao hilo, makampuni hayo yanapaswa kukoboa kahawa kwa
kutumia mashine za CPU’S kuliko kuwaachia wakulima wakoboe majumbani kwa njia
ya kawaida.
Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alitoa agizo hilo
juzi kwenye kikao cha wadau wa kahawa ambacho kiliketi mjini hapa kwa lengo la
kujenga mikakati ya uendelezaji wa zao hilo.
“Sisi kama viongozi tutaendelea kusimamia sheria za
kilimo cha zao hili nawataka pia makampuni yote yanayonunua kahawa jengeni
ushirikiano na serikali tuweze kuwa pamoja, sote tunaamini wafanyabiashara na
serikali tukiwa pamoja ndiyo tunaweza kuendesha maendeleo ndani ya nchi yetu”,
alisema.
Kadhalika aliongeza kuwa kwa makampuni, vyama vya
ushirika na vikundi vya wakulima ambavyo vitaonekana kufanya vibaya kwa kukiuka
taratibu na sheria ameapa kwamba atavifutia usajili wake.
Alisema kuwa kuendelea kuviacha huku vikionekana wazi kuumiza
wakulima itakuwa sio busara, bali dawa yake ni kuvifuta kwani vimekuwa
vikichangia kwa kiasi kikubwa kumzorotesha mkulima bila uwepo wa sababu yoyote
ile ya msingi.
Vilevile alisisitiza kuwa kwa makampuni ambayo
hayajalipa malipo yake ya pili msimu wa mavuno ya kahawa mwaka jana kwa mkulima
ni lazima wakalipe, vinginevyo atahakikisha anayachukulia pia hatua kali za
kisheria.
Naye kwa upande wake Meneja mkuu wa Bodi ya Kahawa
Tanzania (TCB) Kanda ya Ruvuma, Peter Bubelwa alisisitiza makampuni hayo
kuzingatia sheria zilizowekwa ikiwemo kila kampuni kuwa na leseni inayomruhusu
kununua zao hilo wakati wa msimu wa mavuno.
Pia alizungumzia juu ya ubora wa kahawa ambapo Bubelwa
alisema kuwa endapo tunahitaji ongezeko la uzalishaji wa zao hilo itakuwa ni
ndoto kama miti iliyozeeka huko shambani kwa mkulima, haitaboreshwa ipasavyo
hivyo wataalamu husika wanapaswa kuendelea kwenda vijijini kuelimisha wakulima
hao kwa kuwapatia elimu namna ya kuzingatia kanuni za kilimo bora.
Aliongeza kuwa katika msimu wa mavuno mwaka huu mkoa wa
Ruvuma umejiwekea lengo la kufikia tani 18,000 za uzalishaji wa kahawa.
Pamoja na mambo mengine kwa upande wao wadau wa kahawa
wilayani Mbinga nao walisema kuwa wapo tayari kushirikiana na serikali hivyo walishauri
taasisi za fedha kama vile benki, nazo zione umuhimu wa kumsaidia mkulima wa
zao hilo kwa kumkopesha fedha kwa masharti nafuu atakayoweza kununua pembejeo
za kuendeleza zao la kahawa.
Akichangia hoja katika kikao hicho mmoja kati ya wadau
hao, Mario Millinga alisema kuwa umefika wakati sasa mkulima huyo pia anapaswa
kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha ili aweze pia kuachana na ugumu wa maisha
anayokabiliana nayo sasa kule kijijini mara baada ya kuuza mazao yake shambani.
Millinga alisisitiza kuwa endapo mkulima huyo atakuwa na
tabia ya kuweka akiba ya fedha zake za mauzo ya kahawa kwa kila msimu wa mavuno
itakuwa rahisi kwake kununua pembejeo zitakazoweza kuboresha mashamba yake
hatimaye kuweza kuondokana na ugumu huo wa maisha.
No comments:
Post a Comment