Na Mwandishi wetu,
Songea.
MBUNGE wa Jimbo la Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,
Joseph Mhagama amewataka walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo kuona
umuhimu wakufanya kazi kwa bidii, katika kuwafundisha watoto darasani masomo ya
sayansi na kuacha visingizio kwamba wilaya hiyo ina uhaba mkubwa wa walimu wa
masomo hayo.
Kauli hiyo ya Mbunge huyo aliitoa juzi wakati alipokuwa
akikagua utekelezaji wa miradi mbalimbali katika jimbo hilo, ikiwemo ujenzi wa
madarasa manne ya shule ya sekondari Mahanje na shule ya msingi Nkwera zilizopo
wilayani hapa.
Mbunge huyo ambaye alichangia pia shilingi milioni 2.1
kwa ajili ya kununulia vifaa vya ujenzi wa majengo hayo ili yaweze kukamilika
ujenzi wake kwa wakati na yaweze kuanza kutumika.
Alisema kumekuwa na visingizio vya ajabu vikitoka kwa
walimu kuwa katika wilaya hiyo wanafunzi wanaofeli masomo ya sayansi inatokana
na uhaba wa walimu jambo ambalo sio la kweli kwani walimu waliopo wanaouwezo wa
kufundisha kwa bidii na weledi na wanafunzi wakaweza kufaulu masomo hayo.
‘’Kuanzia sasa mimi Mbunge wenu wa jimbo hili sitakubali
kuona uzembe wa mtindo huu ukiendelea kufanyika na watoto hawa wakiendelea
kufeli mitihani ya masomo haya, nahitaji kuona mabadiliko”, alisisitiza
Mhagama.
Vilevile aliongeza kuwa serikali imekuwa ikifanya
jitihada ya kuboresha maslahi ya watumishi wake kazini hivyo nao wanapaswa
kuonesha moyo wa kufanya kazi na sio vinginevyo.
No comments:
Post a Comment