Sunday, April 16, 2017

KAMPUNI YA PANNAR TANZANIA LIMITED YAENDELEA KUJIVUNIA MAFANIKIO YAKE MKOANI RUVUMA

Ofisa masoko wa Kampuni ya Pannar Tanzania Limited mikoa ya Nyanda za juu kusini, Sabasaba Manase upande wa kushoto mwenye miwani akiwaonesha baadhi ya wakulima ambao hawapo pichani shamba darasa lililofanikiwa uzalishaji wa mahindi baada ya kutumia mbegu aina ya Pannar 691 katika kijiji cha Namabengo wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, kulia kwake ni mmiliki wa shamba hilo Agnellus Komba.
Na Julius Konala,     
Namtumbo.

MKULIMA mmoja wa kijiji cha Namabengo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Agnellus Komba ameipongeza Kampuni ya Pannar Tanzania Limited kwa kumwezesha elimu juu ya kilimo bora cha kisasa kwa kutumia mbegu za kampuni hiyo akidai kwamba, imeweza kumuinua kiuchumi na kumfanya aondokane na umaskini.

Hayo yalisemwa juzi na mkulima huyo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu kijijini hapo, akielezea siri ya mafanikio na mbinu mbalimbali zilizomfanya aweze kufanikiwa katika kuendesha shughuli zake za kilimo kwa kutumia mbegu bora za mahindi za Pannar.

Komba alisema kuwa tangu aanze kuendesha kilimo hicho kwa kutumia mbegu hizo ameweza kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kujenga nyumba bora, kufungua duka, kununua usafiri, kusomesha watoto wake pamoja na kufuga kuku na ngombe ambapo amedai kuwa awali kabla ya kupata elimu hiyo alikuwa analima kwa njia za kawaida ambazo zilikuwa hazina tija kwake.


Alisema kuwa katika msimu wa kilimo mwaka jana aliweza kupata tani 80 za mahindi ambapo amedai kuwa kwa msimu wa mwaka huu anategemea kupata zaidi ya tani 100 na kwamba tangu aanze shughuli hizo za kilimo hakuwahi kupata mavuno kwa kiasi hicho.

“Hakuna mbinu yoyote ya uchawi katika kufanikiwa kwenye kilimo zaidi ya kutumia kanuni bora za kilimo kama vile kuandaa shamba, kulima na kupanda vizuri muda wa kutia mbolea ya kupandia na kukuzia pamoja na kufanya usafi wa shamba kwa wakati”, alisema Komba.

Kwa upande wake Ofisa masoko wa kampuni ya Pannar mikoa ya Nyanda za juu kusini, Sabasaba Manase alisema kuwa mpango wa kampuni hiyo ni kuubadili mkoa wa Ruvuma kuwa kitovu cha mbegu za Pannar kwa lengo la kuwaondoa wakulima toka kwenye kilimo cha zamani na kuwapeleka katika kilimo cha biashara.


Manase alisema kuwa wakulima wengi wanafeli katika suala la kilimo kutokana na kujaribu jaribu mbegu, kutozingatia kanuni bora za kilimo, kufanya usafi kwenye mashamba yao, kuzingatia kalenda ya kilimo pamoja na kuwa jirani na maofisa ugani na kwamba amewashauri wakulima hao kutumia mbegu za Pannar ili waweze kuondokana na umaskini.

No comments: