Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
PAMOJA na Serikali kuendelea kusisitiza wahalifu wanaowapatia
mimba wanafunzi wa kike kufungwa miaka thelathini jela, bado baadhi ya jamii imekuwa ikiendelea na
tabia hiyo kitendo ambacho kimekuwa kikikatisha ndoto za maendeleo ya maisha
kwa watoto hao.
Aidha wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, tabia hiyo imekuwa
ikiendelea kufanyika licha ya viongozi husika wilayani humo kukemea kwa nguvu
na kupiga marufuku baada ya kuona kwamba imekuwa ikitishia maendeleo ya
wanafunzi hao.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa tatizo
hilo limekuwa likiendelea kushamiri wilayani hapa, kutokana na jamii kutotoa
ushirikiano wa kutosha kwa serikali hasa pale inapotaka kusimamia sheria ikiwemo
kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wenye tabia hiyo.
Imeelezwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano
wa kutosha badala yake ndiyo wamekuwa chanzo cha kuvuruga madai husika yasiweze
kusonga mbele katika vyombo vya sheria ikiwa ni lengo la kuepuka kufungwa miaka
30 jela.
Hivi karibuni mzee mmoja, Philibert Komba (61) ambaye ni
mkazi wa kijiji cha Lukimwa wilayani Namtumbo anadaiwa kumpatia ujauzito mjukuu
wake (Jina tunalo) mwenye umri wa miaka 16 ambaye anasoma kidato cha pili shule
ya sekondari Lukimwa iliyopo wilayani humo.
Imedaiwa kuwa jamii inayoishi katika kijiji hicho ilikuwa
ikifahamu fika tabia ya mzee huyo, baada ya mjukuu wake alipobanwa aeleze ni
nani mhusika aliyempatia ujauzito huo ndipo alipomtaja na hatimaye babu huyo
alikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Shauri hilo lilipofikishwa katika Mahakama ya mwanzo Mkongo
wilayani hapa, ndipo binti huyo alibainisha mazingira hayo na kueleza kuwa mzee
huyo alikuwa akimfuata chumbani kwake anakolala majira ya usiku na kumlazimisha
kufanya naye tendo hilo la ndoa.
“Alikuwa akiingia chumbani kwangu majira ya usiku na
kunilazimisha kufanya naye mapenzi, huku akiniambia nikipiga kelele ataniua”,
alisema mwanafunzi huyo.
Hata hivyo Polisi wilayani Namtumbo wamekuwa wakiendelea
kumtafuta mtuhumiwa huyo ili aweze kufikishwa katika Mahakama hiyo na kujibu
mashtaka hayo yanayomakabili.
No comments:
Post a Comment