Saturday, April 29, 2017

DC NA MADIWANI WAKERWA NA HALI YA MJI WA MBINGA KUWA MCHAFU

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye, akihutubia jana baraza la Madiwani halmashauri ya mji wa Mbinga.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


KUFUATIA kuwepo kwa hali ya kushamiri kwa uchafu katika mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye ameutaka uongozi wa mji huo uchukue hatua kwa kuhakikisha kwamba taka zote zilizopo kwenye maghuba zinaondolewa haraka iwezekanavyo na maeneo mengine ya mji yanakuwa katika hali nzuri ya usafi.

Aidha Nshenye alisema kila siku amechoka kupokea malalamiko Ofisini kwake kutoka kwa wakazi wa mji huo, ambapo ametaka kero hiyo ya kuuweka mji katika hali ya usafi kwa kuondoa taka zilizorundikana kwa muda mrefu kwenye maghuba inatekelezwa ili kuweza kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.

Nshenye alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa Mji wa Mbinga, lililoketi katika ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

“Kila siku watu wanakuja kulalamika ofisini kwangu juu ya suala hili la uchafu, naagiza wekeni mikakati ya kuondoa taka hizi mapema ili zisiweze kuleta madhara kwa wananchi”, alisisitiza Nshenye.

Vilevile wakichangia hoja kwa nyakati tofauti katika baraza hilo, Madiwani hao walipendekeza kuwa viongozi husika waliopewa dhamana ya kusimamia jambo hilo, wanapaswa kuendelea kukusanya michango ya fedha kutoka kwa wadau mbalimbali ili ziweze kusaidia katika zoezi hilo la uzoaji taka.

“Mheshimiwa Mwenyekiti tunakoelekea hivi sasa tunaelekea kwenye hali ya magonjwa ya mlipuko, afisa afya anatakiwa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha tatizo hili linafanyiwa utekelezaji wa haraka”, alisema Raphael Kambanga Diwani wa kata ya Masumuni.

Kambanga aliongeza kuwa maghuba ya kuhifadhia taka yaliyopo mjini humo, mengine hivi sasa yanatia aibu kutokana na kufikia hatua ya kurundikana taka kwa muda mrefu bila kuzolewa huku yakifikia hatua ya kutoa harufu.

“Niwaambie hakuna kitu kibaya katika maisha ya binadamu kama uchafu, kuna maghuba mengine yanatia aibu yamefikia hatua ya kutoa harufu na kuziba hata njia za kupita watu hali hii inaendelea kuuweka mji wetu kuwa mchafu, mimi nasema kweli huu mji ni mchafu”, alisema.

Kwa upande wake akihitimisha hoja hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Kipwele Ndunguru alisema kuwa agizo la Mkuu wa wilaya hiyo litatekelezwa kwa kuhakikisha kwamba wanaweka mikakati ya kuondoa taka zote zilizopo kwenye maghuba hayo na kwenda kuziteketeza katika eneo husika kwa kushirikiana na wananchi.

Pamoja na mambo mengine mkakati wa kwanza katika kikao hicho alitoa tangazo kwa kuwataka Madiwani, watendaji kata na wataalamu wa halmashauri ya mji huo kukutana na kufanya kikao Mei 2 mwaka huu kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati madhubuti juu ya namna ya kumaliza tatizo hilo.

No comments: