Na Muhidin Amri,
Songea.
VIJANA katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameaswa
wasikubali kugawanywa au kutumika kwa misingi ya dini, kabila au itikadi
za kisiasa kwa maslahi ya watu wachache kwani kufanya hivyo watakuwa wana
tenda dhambi kubwa kwa makundi mengine katika jamii ambayo inahitaji haki na
usawa.
Aidha wametakiwa kuwa imara na kujitambua kutumia muda wao
mwingi katika shughuli za kujiletea maendeleo, sambamba na kujiepusha na
vitendo ambavyo vinaweza kukatisha ndoto za maisha yao ya baadaye.
Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji alisema hayo juzi alipokuwa
akizungumza na vijana hao kutoka kata za Manispaa hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo
juu ya namna ya kutafuta njia bora katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili
katika maisha yao.
Alisema kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa, hivyo ni lazima
wakatae kutumika na watu wenye tamaa ya madaraka ambao wanataka kuwatumia kama
ngazi ya kufanikisha dhamira yao.
Mshaweji aliongeza kuwa badala yake vijana hao wanatakiwa
kutumia nguvu zao katika kutafuta riziki ya maisha yao halali na endapo watafanya
hivyo wataweza kuondokana na tabia ya kuwa omba omba.
Hata hivyo aliwaeleza kuwa katika kata ya Subira Manispaa ya
Songea serikali imetenga eneo kwa ajili ya shughuli za kilimo, viwanda vidogo
na vikubwa huku akiwataka vijana na wananchi wenye uwezo wa
kifedha kuchangamkia fursa hiyo kupata maeneo hayo kwa ajili ya kufanya uwekezaji
huo.
No comments:
Post a Comment