Tuesday, April 25, 2017

TAKUKURU RUVUMA YAFANYA JITIHADA YA KUOKOA MAMILIONI YA FEDHA

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Ruvuma, imeweza kuokoa kiasi cha shilingi milioni 91.811 katika idara ya elimu na kilimo mkoani humo ikiwa ni mishahara hewa ambayo walikuwa wakilipwa watumishi ambao hawakuwa kazini.
Yustina Chagaka.

Uokoaji huo umefanywa kuanzia mwezi Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu ambapo kati ya fedha hizo, sekta ya elimu iliokoa shilingi milioni 61.078 na kilimo milioni 2.233.

Aidha katika sekta ya ujenzi sehemu ya fedha hizo waliweza kuokoa milioni 28.5 baada ya kulipwa mkandarasi ambaye alikuwa katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Mpitimbi B hadi Mbinga Mhalule, halmashauri ya wilaya ya Songea kwa kazi ambazo hazikufanyika na kwamba aliamriwa kuzirejesha.

Mkuu wa taasisi hiyo mkoani hapa, Yustina Chagaka alibainisha hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji wa TAKUKURU katika miezi hiyo, kwa waandishi wa habari ofisini kwake mjini Songea.

Katika hatua nyingine alifafanua kuwa wameweza kupokea taarifa 173 kutoka kwa wananchi katika kipindi hicho kupitia vyanzo mbalimbali.


Alisema kuwa kupitia taarifa hizo idara ambayo inayoongoza kulalamikiwa ni TAMISEMI ambapo ilipokea malalamiko 40, elimu 26, kilimo 21, afya 18, ujenzi 17, ardhi 16, mahakama 14, maji 10, polisi 9 na watu binafsi malalamiko mawili. 

Vilevile aliongeza kuwa kumekuwa na mashauri mbalimbali ambayo yanaendelea mahakamani na kufikia idadi ya 13 ambayo yapo katika ngazi ya wilaya ambapo wilaya ya Songea kuna kesi saba, pia zinazohusu TAMISEMI zipo tatu na kesi nne zinahusu idara ya mahakama, afya, ujenzi na sekta binafsi.

Chagaka alieleza kuwa wilaya ya Mbinga kuna kesi tano zote zinahusu TAMISEMI kwa wilaya ya Namtumbo kuna kesi moja ya idara ya ardhi na kwamba kesi mpya zilizofunguliwa mahakamani kwa kipindi hicho ni kumi na tano huku kesi tatu zikiwa katika mahakama ya wilaya ya Namtumbo na zote zikihusisha idara ya ardhi kutoka kwenye mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ya ardhi katika kata.

Katika wilaya ya Tunduru alisema kuna kesi tano ambapo tatu zinahusu TAMISEMI moja mahakama na nyingine ni ya idara ya ardhi, kesi sita zipo wilaya ya Mbinga ambapo tano zinahusu TAMISEMI na moja ni ya idara ya elimu hivyo kwa upande wa Songea ilifunguliwa kesi moja tu inayohusu sekta ya usafirishaji.

Sambamba na hilo, Chagaka alisema katika kuhakikisha kwamba mianya hiyo ya rushwa inaendelea kuzibwa TAKUKURU mkoani Ruvuma katika kipindi hicho imeweza kufanya kazi za udhibiti (Uchambuzi wa mifumo) ambapo wilaya ya Songea zimefanyika dhibiti nne kuhusu mianya ya rushwa na upendeleo katika zoezi la uteuzi wa kaya maskini zinazonufaika na mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu.

Alisema mbali na mpango huo wa TASAF pia wamefanikiwa kudhibiti mianya ya rushwa katika utoaji wa huduma za afya hospitali ya Mjimwema iliyopo Manispaa ya Songea, udhibiti wa mianya ya rushwa kwenye zabuni katika miradi ya ujenzi halmashauri za wilaya na Manispaa hiyo.

Hata hivyo alisema kuwa lengo hilo la kufanya tafiti au uchambuzi wa mifumo na udhibiti ni kuweza kubaini mianya ya rushwa na kushauri njia madhubuti za kuweza kuiziba kwa kuitisha warsha za wadau mbalimbali na kujadili mianya hiyo namna ya kuidhibiti.

No comments: