Sunday, April 30, 2017

NAMTUMBO WAPOKEA WALIMU WA MASOMO YA SAYANSI

Na Yeremias Ngerangera,    
Namtumbo.

WAKATI Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya elimu hapa nchini, Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma inatarajia kukamilisha kupokea walimu 25 wa masomo ya sayansi, ambao wamepangiwa kwenda kufundisha katika shule mbalimbali zilizopo wilayani humo.

Taarifa iliyotolewa na Afisa elimu wa halmashauri hiyo, Patrick Athanas inafafanua kuwa walimu hao watapelekwa katika shule hizo za sekondari ambapo kati yao wakiume wapo 22 na wa kike watatu.

“Mpaka sasa halmashauri yetu imepokea walimu 24 na kwamba mmoja bado hajaripoti, lakini baada ya siku chache atakuwa tayari ameripoti na kupelekwa katika kituo chake cha kazi”, alisema Athanas.


Alisema kuwa walimu wote walioripoti tayari wamekwisha sambazwa kwenye vituo vyao vya kazi ambavyo wamepangiwa na serikali.

Mkurugenzi  mtendaji  wa halmashauri  ya wilaya  ya Namtumbo, Christopher Kilungu amewataka walimu hao  kufanya kazi kwa bidii ili kuweza  kufikia malengo yaliyowekwa na serikali ikiwemo la kuinua kiwango cha taaluma katika shule za  sekondari.

Pamoja na mambo mengine, halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina jumla ya shule za sekondari 34 ambapo katika ya hizo shule zinazomilikiwa na serikali zipo 24 na 10 ni za mashirika ya dini.

No comments: