Na Julius Konala,
Songea.
BAADHI ya wakulima wanaoishi katika maeneo ya Mletele kata ya
Tanga Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wataondokana na tatizo la njaa baada ya
kuhamasika kutumia mbegu ya mahindi ya muda mfupi aina ya Panner 15 msimu wa
kilimo wa mwaka jana, ambapo mbegu hiyo imeonesha mafanikio makubwa katika
ongezeko la mavuno.
Hayo yalisemwa jana wakati walipokuwa wakizungumza na
mwandishi wetu kwa nyakati tofauti mjini hapa, mara baada ya kutembelea katika kata
hiyo kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali za kilimo zilizofanywa na
wakulima hao.
Waliyataja mafanikio mengine yaliyotokana na mbegu hiyo kwamba
inao uwezo wa kuhimili ukame na magonjwa mbalimbali ya kutu ya majani, jambo
ambalo walidai kuwa limewafanya wahamasike kupanua ukubwa wa mashamba yao na
kutumia mbegu hiyo ya Panner katika msimu ujao wa kilimo.
Mmoja wa mashuhuda waliotumia mbegu hiyo Said Kajanja, Erasto
Makoti na Ania Nkilima wote wakazi wa Mlete wameipongeza kampuni ya Panner kwa
kutoa elimu ya matumizi bora ya mbegu kwa wakulima hao.
Walisema kuwa elimu waliyoipata imechangia kuongeza tija
katika kilimo cha mahindi hali iliyowafanya waweze kuondokana na baa la njaa,
kumudu gharama za kusomesha watoto wao, kujiwekea akiba ya chakula na kujenga
nyumba bora ikilinganishwa na kilimo cha zamani ambacho hakikuwa na tija kwao.
Kwa upande wake Ofisa masoko wa kampuni ya Panner Nyanda za
juu kusini Sabasaba Manase alisema kuwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa
kampuni yake iliamua kufanya utafiti kwa ajili ya kutumia mbegu hiyo kwa lengo la
kukabiliana na ukame na baa la njaa pindi inapotokea.
Manase alisema kuwa sifa nyingine ya mbegu hiyo mazao
yanapokauka yanainama chini kiasi kwamba mvua inaponyesha hayawezi kuharibika, majani
yake yanafunga na mbegu yake inatoa magunia 35 ya mahindi kwa ekari moja hivyo
amewashauri wakulima hao kutumia mbegu hizo kipindi cha hali ya hewa kinapokuwa
kibaya.
Pia aliongeza kuwa lengo la kampuni ya Panner ni kuwafikishia
elimu ya shamba darasa wakulima hao ili waweze kutoka kwenye kilimo cha kawaida
na kuwapeleka katika kilimo cha biashara, ili waweze kusomesha vijana wao na
kujenga nyumba bora huku akidai kuwa mpango wa kampuni kwa siku za mbele ni
kuwafanya wakulima waweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusaga mahindi na
kuuza unga.
No comments:
Post a Comment