Na Kassian Nyandindi,
Songea.
SHIRIKA la Ndege ATCL hapa nchini kupitia ndege zake za
Bombadier kwa mara ya kwanza litaanza safari zake Aprili 30 mwaka huu,
kusafirisha abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Songea mkoani Ruvuma.
Kuanza kwa safari hizo mkoani hapa ni ishara nzuri kwa
serikali ya awamu ya tano iliyodhamiria kuboresha huduma zake kwa
wananchi,hususani katika sekta ya anga kwa lengo la kukuza uchumi wa Tanzania.
Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini hapa, Mkuu
wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge alisema kuwa ndege hiyo
itawasili uwanja wa ndege wa Songea majira ya saa mbili asubuhi ambapo
itafanya safari zake mara tatu kwa wiki yaani siku ya Jumatatu, Jumatano na
Jumamosi.
Dkt. Mahenge amempongeza na kumshukuru Rais Dkt. John
Magufuli kwa kitendo chake cha kujenga historia kwa muda mfupi tangu aingie
madarakani na kuweza kuboresha sekta ya anga, kwa kufungua viwanja vya
ndege ambavyo vilikuwa havifanyi kazi inayostahili kwa muda mrefu.
Alisema kuwa kiwanja cha ndege Songea ni mojawapo kati
ya viwanja hapa nchini ambavyo vilishindwa kufanya kazi vizuri, tena kwa
muda mrefu na kusababisha kukosekana kwa usafiri huo ambao ni wa haraka na
kuaminika na wananchi wengi ndani ya mkoa huo.
Kadhalika alieleza kuwa hali hiyo imesababisha kwa kiasi
kikubwa kudorola kwa maendeleo ya watu ikiwemo kuja kwa wawekezaji mbalimbali
ambao wangeweza kuwekeza ndani ya mkoa hasa katika sekta ya utalii ukizingatia
kwamba mkoa wa Ruvuma unao fursa nyingi za uwekezaji kama vile ardhi, mito
inayotiririsha maji kwa majira yote ya mwaka, madini, misitu na wanyama wa aina
mbalimbali.
Alisema hivi sasa kutokana na uwepo wa uhakika wa
usafiri huo wa anga sekta nyingi zitakua kiuchumi kutokana na kupata wageni na wawekezaji
wengi wa kutoka katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa alifafanua kuwa uwepo wa
usafiri huo wa ndege za ATCL anao uhakika kwamba utasaidia ushiriki wa wananchi
wa Ruvuma katika shughuli za kukuza uchumi wao na kuongeza kipato ikiwemo
wanaoendesha biashara za hoteli, kusafirisha abiria kwa magari kama vile taxi
na sekta zingine za kiuchumi.
Pia alieleza kuwa kitendo cha ATCL kuanza safari zake
mkoani hapa vilevile kutaleta nafuu kwa wananchi wa mkoa huo na mikoa mingine
ya jirani, kutokana na gharama zake kuwa nafuu ikilinganishwa na makampuni
mengine yaliyoanza safari zake mkoani Ruvuma kuwa na bei juu.
“Hatua hii ni ya kujivunia kwa wananchi na serikali ya
mkoa huu kwa sababu fursa hii haijawahi kutokea kwa muda mrefu kwani gharama ya
usafiri wa ndege hizi ni nafuu”, alisema Dkt. Mahenge.
Kwa upande wake Meneja wa shirika hilo la ndege mkoani
Ruvuma na Mtwara, Esther Mahiga naye alisema kuwa bei ya safari moja kutoka
Songea kwenda Dar es Salaam ni shilingi 270,000 ambapo kwa mtu anayekata tiketi
ya kwenda na kurudi atalipa shilingi 400,000 tu.
Mahiga aliwataka Wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa
wingi kutumia usafiri huo wa umma na Wafanyabiashara wataweza pia kusafirisha
mizigo yao kwa haraka na gharama nafuu.
No comments:
Post a Comment