Na Julius Konala,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea
mkoani Ruvuma, imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.325 katika mwaka wa
fedha 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya miradi ya maji, kwa lengo
la kuwafikishia wananchi wa Manispaa hiyo huduma ya maji safi na salama.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na
Mhandisi wa maji wa Manispaa ya Songea, Samwel Sanya alipokuwa akizungumza na mwandishi
wetu ofisini kwake kwa lengo la kuelezea utekelezaji mbalimbali wa miradi ya maji
katika Manispaa hiyo.
Sanya alisema kuwa tangu mwaka 2007
halmashauri hiyo inaendelea kutekeleza programu ya maji na usafi wa mazingira
katika mitaa 10 ikwemo Mahilo, Chandarua, Muhombezi, Muungano, Mahinya, Ngandula,
Ruhuwiko kanisani, Mitendewawa, Ruhila kati na Liwumbu.
Alisema kuwa utekelezaji wa ujenzi wa
miundombinu hiyo bado unaendelea katika baadhi ya mitaa ambapo mitaa ya Mahilo,
Chandarua, Muhombezi, Muungano na Mahinya utekelezaji wake umekamilika huku
akiitaja mitaa ambayo utekelezaji wake unaendelea kuwa ni Ruhuwiko kanisani, Mitendewawa
na Ruhila kati.
Alifafanua
kuwa hatua ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya maji kwa kila mtaa ni
kama ifuatavyo ambapo Ruhuwiko kanisani umefikia asilimia 95 na utahudumia watu
3504, Mitendewawa asilimia 20 utahudumia watu 852 ambapo Ruhila kati umefikia
asilimia 30 na kwamba utaweza kuhudumia watu 941.
Pia alieleza
kwamba kulingana na mikataba yenye jumla ya kiasi cha shilingi biliioni 1.37
zinatakiwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya maji kwa mwaka wa
fedha 2016/2017 ambapo halmashauri ya Manispaa ya Songea kupitia Wizara ya maji
na umwagiliaji imeomba kuongezewa fedha kiasi cha shilingi milioni 107.344 ili
ziweze kukidhi mahitaji ya ununuzi wa pampu 89 za maji.
Kadhalika aliongeza kuwa mpango wa matumizi
ya fedha inayobaki kiasi cha shilingi milioni 187.655 kwa mwaka wa fedha
2016/2017 ni kwa ajili ya kukarabati visima vya mikono katika mitaa 89 ambapo
amedai kuwa tayari mzabuni wa ununuzi wa pampu hizo kwa ajili ya kuongeza
utoaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wapatao 22,250 huku akidai
kwamba jumla ya kiasi cha shilingi milioni 295 kitatumika kununulia pampu 89.
No comments:
Post a Comment