Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKURUGENZI wa halmashauri ya mji, Robert Mageni na
wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito mkoani Ruvuma wametakiwa kusimamia na
kufuatilia maendeleo ya wakulima wa kahawa vijijini, ili waweze kujua ni
matatizo gani wanakabiliana nayo katika uzalishaji na uendelezaji wa zao hilo
na kuyatafutia ufumbuzi wa haraka.
Aidha maofisa ugani katika halmashauri hizo nao
wamenyoshewa kidole wakilalamikiwa kwamba muda mwingi wamekuwa wakikaa
maofisini kwa kutotembelea mara kwa mara wakulima hao kwa lengo la kuweza kuwapatia
elimu namna ya uzalishaji bora wa zao hilo.
Hayo yalitokea juzi katika kikao cha wadau wa kahawa
kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa ambapo Mkuu wa
wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye aliwataka viongozi hao na maofisa kilimo kuhakikisha
kwamba sasa wanatekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kusimamia sheria na taratibu
zilizowekwa ikiwemo kwenda kwa wakulima vijijini kutatua matatizo katika sekta
ya kilimo yanayowakabili.
“Nawataka Wakurugenzi wote wawili na maofisa kilimo
simamieni na fuatilieni hili suala la maendeleo ya wakulima hawa ni lazima wapitieni
huko waliko ili kuweza kujua wana matatizo gani yanayowakabili”, alisisitiza
Nshenye.
Nshenye aliongeza pia wanapaswa wahamasishe wakulima hao
wajiunge kwenye vikundi vya wakulima ili waweze kukopesheka kwa urahisi na
hatimaye fedha za mikopo watakazopata, waweze kununua pembejeo za kilimo kwa kuendeleza
mazao yao shambani na kuondokana na biashara haramu ya magoma ya kahawa ambayo
huwafanya waendelee kuwa maskini.
Awali kwa mujibu wa taarifa ya uendelezaji wa zao la
kahawa katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga ilielezwa kuwa halmashauri hiyo
inampango wa kuongeza eneo la uzalishaji toka hekta 28,848 zilizopo sasa hadi
kufikia hekta 31,554.6 ifikapo mwaka 2020.
Taarifa hiyo ambayo ilitolewa na Ofisa mazao wa wilaya
hiyo, Deodatus Kissima alisema kuwa katika kufanikisha mpango huo halmashauri
pia katika msimu wa mwaka 2017/2018 inatarajia kuzalisha miche 1,200,000 ya
kahawa ikiwa ni miche itakayozalishwa na vikundi vya wakulima, makampuni na
watu binafsi kwa njia ya vikonyo na mbegu.
Kissima alifafanua kuwa katika msimu wa mwaka huu halmashauri
pia imepanga kukamilisha ujenzi wa mitambo ambayo ilikuwa haijaisha ujenzi wake
ambapo imetenga fedha shilingi milioni 275,901,000 kumalizia ujenzi huo.
Vilevile kwa upande wa halmashauri ya mji wa Mbinga imejiwekea
mikakati ya uendelezaji wa zao hilo kwa kuhakikisha kwamba wanaongeza
uzalishaji kutoka hekta 7,458 hadi kufikia hekta 10,000 ifikapo mwaka 2020
ambapo mkakati huo utaenda sambamba na uzalishaji wa miche katika bustani mama
13 za kahawa ya vikonyo zilizopo sasa.
Ofisa kilimo wa halmashauri hiyo Maganga Ngahy alisema
hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mikakati hiyo na kuongeza kuwa
halmashauri itahakikisha inawawezesha wataalamu wa ugani kupita kutoa elimu kwa
wakulima juu ya uboreshaji na utunzaji wa mashamba hususani kuzingatia kanuni
bora za kilimo cha zao hilo.
No comments:
Post a Comment