Wavuvi wakiwa katika ziwa Nyasa mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limesema kuwa tukio la kufa
maji mwanafunzi wa kidato cha tatu, Yahaya Rashid (19) katika ziwa Nyasa mkoani
humo limesababishwa na uzembe wa Walimu ambao walikuwa wameambatana na
wanafunzi wenzake waliokwenda katika ziwa hilo kujifunza mambo ya utalii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa
mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 23 mwaka
huu majira ya saa 11 jioni katika mji mdogo wa Mbamba bay wilaya ya Nyasa.
Alisema kuwa mwanafunzi huyo ambaye amekutwa na umauti ni mkazi
wa Mbinga mjini, ambapo anasoma shule ya Sekondari Makita iliyopo halmashauri
ya mji wa Mbinga mkoani hapa.
Mwombeji alisema kuwa Rashid alikuwa ameambatana na wanafunzi
wenzake pamoja na walimu wa shule hiyo ambao walikwenda wilayani Nyasa, kwa
lengo la kwenda kujifunza masuala ya utalii, mawimbi ya ziwani pamoja na
mipangilio ya miamba iliyopo katika ziwa hilo.
“Usimamizi wa walimu ambao walikuwa wameambatana na hawa
watoto haukuwa mzuri ndio maana ulisababisha mtoto huyu kufa maji, kwa sababu
baada ya kumaliza mafunzo yao ndipo walikuja kubaini nguo na viatu vya marehemu
vikiwa mchangani ufukweni huku yeye haonekani”, alisema.
Vilevile aliongeza kuwa baada ya kuona mwanafunzi huyo haonekani,
ndipo walimu walioambatana na watoto hao walikwenda kuripoti Kituo kikuu cha Polisi
wilaya ya Nyasa, ambapo askari Polisi kwa kushirikiana na Wavuvi walianza kazi
ya kuutafuta mwili wa marehemu huyo na kufanikiwa kuupata leo Septemba 24 mwaka
huu majira ya saa 5 asubuhi.
Hata hivyo alieleza kuwa mwili huo ulipatikana ukiwa chini ya maji na kufanikiwa kuutoa nje ya ziwa hilo majira hayo ya asubuhi na kukabidhiwa mikononi mwa viongozi wa halmashauri ya mji wa Mbinga, kwa ajili ya kuendelea na taratibu za mazishi na kwamba uchunguzi juu ya tukio hilo bado unaendelea.
No comments:
Post a Comment