Na Julius Konala,
Songea.
BAADHI ya wakulima mkoani Ruvuma, wamefurahia utaratibu
uliopangwa na serikali kupitia kitengo chake cha Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula
Tanzania (NFRA) kanda ya Songea mkoani humo, kwa kufungua vituo vya ununuzi wa
mahindi katika vijiji mbalimbali kwa kile walichoeleza kuwa kufanya hivyo kumeweza
kutoa fursa kwa wakulima wadogo wadogo, kuuza mazao yao pamoja na kuondoa
malalamiko yasiyokuwa na msingi.
Pongezi hizo zilitolewa na wakulima hao mwishoni mwa wiki
mbele ya Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa katika ziara yake ya
kikazi kutembelea vituo hivyo vilivyotengwa kwa ajili ya ununuzi wa mahindi msimu
wa mwaka 2016/2017 mkoani hapa.
Walisema kuwa awali utaratibu huo ulikuwa ukiwanufaisha
walanguzi na wafanyabiashara wakubwa na sio kwa wakulima wadogo kama ilivyo
sasa.
Akizungumza na wakulima hao kwenye vituo mbalimbali vya
kununulia mahindi hapa mkoani Ruvuma, Meneja wa NFRA kanda ya Songea Majuto
Chabruma alisema kuwa msimu wa mwaka 2016/2017 kanda hiyo imepangiwa kununua
tani 20,000 za mahindi, ambazo zitagawanywa kwa kila wilaya kutokana na idadi
ya uzalishaji husika.
Chabruma amewataka wakulima hao kuuza mahindi yao kwa
kuzingatia ubora na kwamba amezitaja changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni
kuuziwa mahindi yenye takataka, uhaba wa fedha pamoja na wakulima kulalamikia
utaratibu wa kupima gunia kumi kumi.
Akihutubia kwenye vituo hivyo vya ununuzi wa mahindi, Mkuu wa
mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge amewataka wakulima hao kujiwekea akiba ya
chakula badala ya kuuza mahindi yote na kwamba amewaagiza Wakuu wa wilaya zote mkoani
humo, kufanya ukaguzi wa nyumba hadi nyumba kwa lengo la kuwabaini waliouza
ziada ya chakula walichojiwekea.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa uendeshaji Wakala wa taifa
hifadhi ya chakula katika kanda hiyo, Nicodemus Massao alisema kuwa wanampango
wa kupanua wigo katika kuboresha huduma zake ikiwemo pamoja na kujenga kiwanda
cha nafaka, maabara ya kisasa na uzio kuzunguka kituo hicho.
No comments:
Post a Comment