Na Kassian Nyandindi,
Songea.
IMEELEZWA kwamba ifikapo mwaka 2018, mji wa Songea ambao ni
makao makuu ya mkoa wa Ruvuma unatarajiwa kuunganishwa na umeme wa gridi ya taifa
kutoka Makambako mkoa wa Njombe.
Leonidas Gama. |
Hayo yalisemwa na Mbunge wa Songea mjini, Leonidas Gama alipokuwa
akizungumza na wananchi wa kata ya Misufuni mjini hapa na kuongeza kuwa serikali
imekwisha anza mchakato wa kukamilisha kazi hiyo, ili utekelezaji wake uweze
kuanza mara moja.
“Nataka kuwahakikishia kwamba mkandarasi ameanza kazi mwaka
huu kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa kuweza kuleta umeme huu wa gridi ya taifa,
kutoka Makambako ambao utapitia Madaba hadi Songea mjini makao makuu ya mkoa wetu
wa Ruvuma”, alisema Gama.
Alisema kuwa umeme huo utakapokuwa umefika Songea fursa
nyingi za uwekezaji zitakuwepo, ikiwemo ujenzi wa viwanda vikubwa vitakavyoweza
kutoa ajira kwa watu wengi hususani vijana na kuweza kuongeza kasi ya kukua kiuchumi.
Mji wa Songea kwa miaka mingi kutokana na kutokuwepo umeme wa
uhakika hali hiyo inasababisha hadi sasa kutokuwepo kwa viwanda hivyo, jambo
ambalo linachelewesha hata kukua kwa maendeleo ya wananchi na mkoa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo alisema kuwa serikali
inatarajia kujenga pia hospitali kubwa ya kisasa, yenye viwango vya kukidhi
matibabu ya hali ya juu katika eneo la Mwengemshindo Manispaa ya Songea mkoani
humo.
Gama alisema kuwa tayari wataalamu kutoka Wizara ya wa afya hapa
nchini, wamekagua katika eneo hilo itakapojengwa hospitali na kwamba ujenzi
wake utakapokamilika itakuwa mkombozi mkubwa, hasa kwa wananchi waishio nyanda
za juu Kusini kwa kile alichoeleza kuwa hawatakuwa na sababu tena ya wagonjwa
kupewa rufaa kwenda hospitali ya taifa Muhimbili.
No comments:
Post a Comment