Tuesday, September 20, 2016

SUMATRA NA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI WALALAMIKIWA TUNDURU

Na Muhidin Amri,
Tunduru.

BAADHI ya Wananchi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamelalamikia hatua ya wamiliki wa mabasi yanayofanya safari zake kati ya Tunduru mjini kwenda Masasi mkoani Mtwara, kuendelea kutoza nauli kubwa licha ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Dkt. Binilith Mahenge Mkuu wa mkoa wa Ruvuma.
Aidha wameilalamikia Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Usafiri wa  nchi kavu na Majini (SUMATRA) mkoani Ruvuma, kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka dhidi ya tatizo hilo ambalo sasa limefikia hatua ya kuwa kero katika jamii.

Walisema kuwa SUMATRA imeshindwa kuyachukulia hatua Makampuni husika yanayosafirisha abiria, ambayo yanaendelea kuwakandamiza wananchi na kuwa kero kubwa kwao.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona wamiliki  wa mabasi hayo, kuendelea na mchezo huo mchafu wa kutoza nauli ya shilingi 12,000 kutoka Tunduru hadi  Masasi badala ya shilingi 7,000 hadi 8,000.


Kassim Hassan mkazi wa kijiji cha Majimaji Tunduru mjini alisema kuwa, kinachoonekana ni kwamba SUMATRA na Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani, wanashindwa kusimamia majukumu yao na kwamba wanaonekana kuendelea kuwalinda wamiliki wa makampuni hayo yanayotoa huduma ya usafirishaji kwa manufaa yao binafsi.

Hassan ameitaka mamlaka husika kuchukua hatua sasa kabla ya tatizo hilo halijafikia hatua ya kuwa sugu, ili kuondoa malalamiko hayo yasiyokuwa ya lazima.

Naye Khadija Mponda alisema kujengwa kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kumesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo hasa kwa akina mama wajawazito na watoto kwa kile alichoongeza kuwa kumerahisisha kwao hata kuhudhuria Kliniki ili waweze kujifungua wakiwa salama.

Pia Mponda ameiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma baadhi ya wananchi waliovunjiwa nyumba zao wakati ujenzi huo ulipokuwa ukifanyika, kutokana na hadi sasa kutolipwa fidia zao huku wakiendelea kuteseka kutokana na maisha magumu waliyonayo sasa.

Naye Mohamed Kajimbu amemtaka Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Ruvuma, kuharakisha kuweka mizani ya dharula katika barabara hiyo ili kuweza kulinda isiharibike mapema kutokana na baadhi ya wasafirishaji mizigo hasa malori makubwa kupita huku yakiwa na shehena kubwa, ambazo hazilingani na uwezo wa barabara hiyo.

No comments: