Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MASHAMBA ya wakulima wanaozalisha zao la kahawa wilayani Mbinga
mkoa wa Ruvuma, yamewekwa katika mpango wa kupimwa kisheria ili wakulima hao
waweze kuwa na hati miliki za kimila, ambazo zitawasaidia waweze kusonga mbele kimaendeleo.
Aidha upimaji huo wa mashamba unalenga pia kuifanya serikali
iweze kutambua ni wakulima wangapi wilayani humo wanamashamba ya kahawa, ili
hapo baadaye iweze kutengeneza takwimu zake halisi zitakazowatambua wazalishaji
wake wa zao hilo.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya hiyo, Gombo Samandito alipokuwa akitolea ufafanuzi juu ya faida za
upimaji ardhi katika kikao cha wadau wa kahawa kilichofanyika juzi mjini hapa.
Samandito alifafanua kuwa upimaji huo utaenda sambamba na kupimwa
ardhi inayozalishwa mazao mengine pamoja na ile ya makazi ya watu, ikiwa ni
lengo la kuhakikisha kwamba kila mwananchi anayemiliki ardhi anakuwa na hati
miliki ya kimila ambayo itaweza kumsaidia katika kuinua uchumi wake.
“Wadau wetu wa kahawa kuna umuhimu mkubwa wa kupima ardhi
yenu, zoezi hili tunatarajia kulianza wakati wowote kuanzia sasa mara baada ya
taratibu husika kukamilika, hivyo tutakapoanza kufanya kazi hii tunahitaji
ushirikiano wenu wa kutosha”, alisisitiza Samandito.
Pamoja na mambo mengine, kwa mujibu wa taarifa ya maendeleo
ya zao la kahawa wilayani Mbinga, zinaeleza kuwa katika msimu wa mavuno mwaka
2015/2016 jumla ya tani 15,000 za kahawa kavu zilizalishwa kutoka kwa wakulima
wa zao hilo.
Vilevile katika kipindi cha mwaka 2016/2017 wilaya hiyo
inatarajia kuvuna tani 13,000 na kwamba upungufu huo wa uzalishaji, unatokana na
mikahawa mingi kuzaa kwa wingi msimu uliopita pamoja na kushambuliwa na wadudu
waharibifu aina ya Vidung’ata.
Hata hivyo tokea msimu wa kahawa ufunguliwe Julai Mosi mwaka
huu, mpaka sasa jumla ya tani milioni 3,737171.1 zimekusanywa na kukobolewa
katika viwanda vya kukoboa kahawa vilivyopo wilayani humo.
No comments:
Post a Comment