Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amezitaka Halmashauri
za wilaya mkoani humo, mpaka kufikia mwishoni wa mwezi Disemba mwaka huu
zihakikishe kwamba zimekamilisha zoezi la ujenzi wa vyoo katika shule za msingi
na sekondari.
Aidha ameagiza utekelezaji wa kuboresha miundombinu ya sekta
ya afya ambapo kila kijiji na kata wataalamu husika, wanatakiwa kusimamia na
kutekeleza ujenzi wa majengo ya zahanati na vituo vya afya.
Dkt. Mahenge alitoa agizo hilo juzi alipokuwa mgeni rasmi
katika sherehe za kufunga mafunzo ya miezi mitatu kwa mujibu wa sheria, Operesheni Magufuli kwa
vijana waliomaliza kidato cha sita katika maeneo mbalimbali hapa nchini katika
kikosi cha Jeshi Mlale 842KJ zilizofanyika mkoani hapa.
“Pia naagiza halmashauri zote katika mkoa huu, watumie jeshi
hili kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za ujenzi wa majengo ya maabara,
shule na hata ujenzi wa matundu ya kisasa ya vyoo ili tuweze kuwafanya watoto
wetu mashuleni waweze kuepukana na magonjwa ya mlipuko”, alisema Dkt. Mahenge.
Mkuu huyo wa mkoa alifafanua kuwa lengo la serikali kuanzisha
mafunzo hayo kwa vijana wanaohitimu kidato cha sita, ni kuwaandaa kuwa
wazalendo kwa nchi yao na kuitumikia kwa dhati katika nyanja zote za kiuchumi,
siasa na kijamii.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo huwafanya waweze kuondoa tofauti
za kielimu, kikabila, kidini, kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa
kwa lengo pia la kuthamini na kupenda kazi za mikono na kujiajiri wao wenyewe
na sio kuwa na mawazo ya kupata ajira serikalini tu.
Kwa upande wake akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) hapa nchini, Kanali John Mbungo wa kikosi cha JKT Mlale
mkoani Ruvuma aliwataka vijana hao huko waendako waache kushabikia mambo yenye
kujenga mgawanyiko katika jamii kwa sababu ya itikadi za kisiasa.
Kanali Mbungo alieleza kuwa huko waendako wakashirikiane na
wananchi kupambana na wakwepa kodi na kulijenga taifa katika kutekeleza kauli
mbiu ya Hapa kazi tu, na kuleta mabadiliko chanya miongoni mwa jamii.
Alisema kuwa serikali itaendelea kuboresha na kushughulikia
changamoto mbalimbali zilizopo katika vikosi vya mafunzo ya Jeshi, ikiwemo
kununua vifaa husika vya mafunzo kwa ajili ya kuweza kuwafanya vijana waweze
kushiriki vyema wanapokuwa katika mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment