Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Masasi mkoani
Mtwara, Dkt. James Almasi amekemea tabia ya baadhi ya wanasiasa hapa nchini kutumia
migongo ya waumini kupitia mashirika ya dini, kwa ajili ya manufaa yao binafsi
na kuwataka kuacha mara moja tabia hiyo kwa kile alichoeleza kuwa kufanya hivyo
ni dhambi na kumchukiza mwenyezi Mungu.
Badala yake alifafanua kuwa ni vyema wanasiasa wakatafuta
njia nyingine mbadala ambayo itawafanya waweze kuwa salama mbele ya Mungu,
kwa kutumia kipato wanachopata kwa ajili ya kuchangia na kusaidia shughuli
mbalimbali za maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.
Dkt. Almasi alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati alipokuwa akikabidhi vifaa
tiba, vitanda pamoja na baiskeli za magurudumu matatu kwa ajili ya
zahanati, vituo vya afya na hospitali katika vijiji 66 kwa Mkuu wa wilaya ya
Tunduru mkoani Ruvuma, Juma Homera.
Alisema kuwa Dayosisi hiyo imekuwa mstari wa mbele kutekeleza
shabaha yake kuu ya pili ya kumwezesha na kumwendeleza kila binadamu kujikomboa
kifikra na kuondokana na umaskini, ikiwemo kuboresha maisha yake kwa kutumia
rasilimali zinazomzunguka katika mazingira yake.
Aliongeza kuwa shabaha hiyo ndiyo inayoifanya Doyasisi ya
Masasi, kushughulika na huduma za kijamii kwa kuanzisha miradi ya maendeleo katika
jamii ili kuweza kuboresha afya na maisha yao.
Kwa mujibu wa Askofu Dkt. Almasi alieleza kuwa katika kipindi
cha miaka 10 kuanzia mwaka 2006 Dayosisi hiyo imeweza kushughulikia miradi
mikubwa ya kijamii ikiwemo pia mradi wa ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa ambao
huwapatia wananchi waliojiunga katika vikundi vya ujasiriamali.
Dkt. Almasi alisema mradi huo ulitekelezwa katika kipindi cha
miaka mitano kunzia mwaka 2006 hadi 2011 na kwamba ulihusisha usambazaji wa
ng'ombe wa maziwa, mbuzi wa maziwa, ng’ombe wanaotumika kwa ajili ya kazi
za kilimo cha maksai, ufugaji samaki na nyuki kwa wananachi wenye kipato cha
chini.
Alisema kuwa katika kipindi hicho familia zipatazo 12,640
zenye jumla ya watu 398,160 katika wilaya za Mtwara Mikindani, Tandahimba, Newala,
Masasi, Nanyumbu, Kilwa, Lindi mjini na vijijini, Ruangwa, Nachingwea na Liwale
zilinufaika na mradi huo.
Pia aliongeza kuwa mradi wa pili ni wa huduma ya afya
ya jamii na uboreshaji wa mazingira ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka
2012 na utamalizika mwaka 2017 ambapo
unalenga kuboresha afya ya jamii katika vijiji 20 vya wilaya ya
Nachingwea.
Alisema kuwa huduma zinazotolewa ni elimu ya afya, vifaa tiba
na madawa katika zahanati 18 ambazo ni za serikali na usambazaji wa mifugo
ikiwemo ng’ombe wa maziwa, mbuzi na uendelezaji kuku wa kienyeji.
Pamoja na mambo mengine Askofu Dkt. Almasi alitaja miradi
mingine kuwa ni usambazaji mbegu za nafaka ili kuongeza kiwango cha uzalishaji
wa mazao ya chakula na biashara, katika jamii na familia unaokwenda pamoja
na uchimbaji visima virefu 28 vya maji safi na salama ambapo umekusudia
kuwanufaisha wananchi wapatao 64,560 wa vijiji hivyo.
No comments:
Post a Comment