Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
BENKI ya CRDB tawi la Songea mkoani Ruvuma, imetoa msaada wa
madawati 90 yenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa halmashauri ya wilaya ya
Namtumbo mkoani humo, ili yaweze kusaidia kukabiliana na tatizo la upungufu
wa madawati kwa watoto wa shule za msingi wilayani humo.
Akikabidhi madawati hayo juzi Meneja wa tawi hilo, Enock
Lugenge alisema kuwa msaada huo uliotolewa ni utaratibu waliojiwekea benki hiyo
ambapo kila mwaka inagawa faida inayopatikana kwa wanahisa wake
na sehemu ya faida inayobaki inarudishwa katika nyanja mbalimbali kwa kuchangia
huduma za afya, elimu, maji na shughuli nyingine za maendeleo hapa nchini.
Lugenge alifafanua kuwa katika kusogeza huduma karibu na
wananchi pia benki hiyo ya CRDB imefungua tawi dogo mjini Namtumbo, ambapo hutoa huduma za kifedha wakati wote wa masaa
ya kazi.
Alisema kuwa benki hiyo imelazimika kufungua tawi hilo kwa
lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za kibenki
kama vile kufungua akaunti, kuweka na kutoa fedha, huduma za ATM, bima kwa mali
na magari pamoja na huduma za mikopo kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza
miradi ya wananchi kiuchumi.
Pia Lugenge alieleza kuwa mbali na huduma hizo, CRDB
inatoa mikopo kwa ajili ya watumishi, wafanyabiashara sambamba na mikopo ya
pembejeo za kilimo kwa wanachama wa vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS).
Kwa upande wake akipokea msaada wa madawati hayo Makamu Mwenyekiti
wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, Titus Ng’oma ameishukuru benki hiyo kwa
kutoa madawati hayo ambayo yatamaliza tatizo la wanafunzi kukaa chini kwa shule
za msingi wilayani humo.
Ng’oma alitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kwa wingi
kusaidia wananchi wa wilaya hiyo hasa katika sekta ya afya, maji, miundombinu ya
barabara, maji na kilimo ambayo ujenzi wake bado haujakamilika.
No comments:
Post a Comment