Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akiwa katika ziara yake ya kikazi juzi wilayani Namtumbo. (Picha na Yeremias Ngerangera) |
Na Julius Konala,
Namtumbo.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge, amefanya ziara
ya kushitukiza katika shule ya msingi Sasawala iliyopo wilayani Namtumbo mkoani
humo na kubaini shule hiyo kuwa na ukosefu wa vyoo bora vya kisasa kwa ajili ya kujisaidia wanafunzi.
Mahenge alikumbana na changamoto hiyo juzi baada ya kufanya
ziara hiyo iliyolenga kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo
kuhimiza suala la ufyatuaji wa matofali 100,000 kwa kila kijiji kwa ajili ya
kusaidia ujenzi wa zahanati, madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu pamoja
na vyumba vya maabara.
Alisema kuwa hali hiyo inaweza kusababisha magonjwa ya
mlipuko kwa wanafunzi wa shule hiyo ambapo ameutaka uongozi wa wilaya hiyo,
kuhakikisha kwamba unaanza mchakato wa ujenzi wa vyoo shuleni hapo haraka
iwezekanavyo ili kuweza kunusuru afya za watoto hao.
“Kwa kweli nimesikitishwa sana kuona karne hii ya leo bado
kuna baadhi ya shule za msingi wanafunzi wake, wanatumia vyoo vilivyojengwa kwa
kuzungushiwa nyasi na havina milango jambo hili nasema ni udhalilishaji mkubwa
hasa kwa watoto wa kike”, alisema Dkt. Mahenge.
Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa mkoa amemuagiza Mkuu wa
wilaya ya Namtumbo, Luckness Amlima na Mkurugenzi wake wa halmashauri ya wilaya
hiyo, Christopher Kilungu kuhakikisha kwamba wanafanya ziara ya kutembelea
shule zote za msingi na sekondari zilizopo wilayani humo kwa lengo la kujionea
changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo walimu na wanafunzi.
“Tembeleeni shule hizi mtaweza kuwa na takwimu za maabara, matundu
ya vyoo, madarasa na nyumba za walimu katika kila shule, badala ya kusubiri
taarifa ziwafikie mezani kutoka kwa wataalamu wenu”, alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Amlima alisema
kuwa amepokea maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu huyo wa mkoa na kuahidi
kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo huku akiwataka wananchi kushirikiana na
serikali, katika shughuli za maendeleo ili ifikapo mwezi Novemba mwaka huu ujenzi
huo wa vyoo uwe umekamilika.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Kilungu alisema kuwa suala la ujenzi wa vyoo katika shule za msingi na sekondari wilayani humo tayari upo katika mpango, hivyo kinachoendelea ni kuanza hatua ya utekelezaji wa haraka ikiwemo kuwashirikisha wananchi katika kuchangia nguvu zao na serikali kutoa vifaa vya kiwandani.
No comments:
Post a Comment