Tuesday, September 20, 2016

BASI LA NEW FORCE LAPATA AJALI LAUA 12 NA KUJERUHI 30

Na Kassian Nyandindi,         
Songea.

WATU 12 wamefariki dunia na wengine 30 kujeruhiwa vibaya kufuatia ajali ya basi la Kampuni ya New Force, linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Songea mkoani Ruvuma kuacha njia na kupinduka mara tatu katika kata ya Kifanya wilaya ya Njombe mkoani Njombe.

Tukio hilo lilitokea jana majira ya usiku katika kijiji cha Lilombwi kata ya Kifanya wilaya ya Njombe mkoani  Njombe, kabla ya kufika mpakani mwa mikoa ya Njombe na Ruvuma.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Pudenciana Protas amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa  lilitokea Septemba 19 mwaka huu majira ya saa 1.40 usiku, huku chanzo cha ajali hiyo kikielezwa kuwa ni uzembe wa dereva kutokana na kuendesha kwa mwendo kasi.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Polisi alifafanua kuwa gari lililohusika na ajali hiyo ni lenye namba za usajili T 429 aina ya Zongtong, ambalo lilikuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Songea mkoani Ruvuma likiwa linaendeshwa na dereva aliyetambuliwa kwa jina la Charles Chilwa ambaye amekimbia na kutokomea kusikojulikana.


Protas alisema kuwa miili ya marehemu 11 bado haijatambuliwa na ipo katika hospitali ya mkoa mjini Njombe na mwili mmoja kati ya  hao 12 tayari umetambuliwa ambapo marehemu amefahamika kwa jina la, Bruno Kayombo (5) mkazi wa Morogoro na umehifadhiwa kituo cha afya Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na raia wema tunaendelea kumtafuta dereva huyu, ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria na kwamba tunawaomba wananchi popote pale watakapomuona watoe taarifa kituo chochote cha Polisi kilichopo karibu nao”, alisema Protas.

Alisema kuwa kati ya majeruhi hao 30, wamepelekwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma (HOMSO) na wengine 11 wamepelekwa hospitali ya mkoa Njombe na majeruhi waliolazwa ni 11 ambapo  majeruhi 3 wamelazwa katika hospitali ya rufaa Songea na 8 wamepelekwa hospitali ya mkoa wa Njombe na kwamba wengine wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kwenda makwao.

Pia kwa mujibu wa baadhi ya abiria walionusurika katika jali hiyo waliwaeleza waandishi wa habari kwamba, kabla ya kutokea ajali hiyo basi hilo lilinusurika kuanguka zaidi ya mara mbili katika maeneo tofauti katika barabara ya Njombe Songea kutokana na mwendo kasi wa dereva huyo.

Hata hivyo abiria hao ambao hawakutaka kutaja majina yao na ambao wamelazwa katika hospitali hiyo ya mkoa wa Ruvuma mjini Songea, walisema kuwa licha ya kumuonya dereva huyo mara nyingi apunguze mwendo wake hakutaka kusikia badala yake alikuwa akiendelea kuendesha kwa kasi na kusababisha ajali hiyo.

No comments: