Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
MTU mmoja mkazi wa kijiji cha Myangayanga Tanga pachani halmashauri
ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Anna Ndunguru (40) amefariki dunia baada ya
lori lililokuwa limebeba shehena ya magunia ya mahindi, kuacha njia na
kuparamia nyumba waliyokuwa wanaishi wakati akiwa amekaa ndani ya nyumba hiyo na
wenzake wakipata mlo wa mchana.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa,
lilitokea Septemba 8 mwaka huu majira ya saa 6:32 mchana ambapo lori hilo lenye
namba za usajili T 231 BCH mali ya mfanyabiashara mmoja maarufu mjini hapa,
Medson Ulendo lilikuwa likitokea katika kijiji cha Kilindi kata ya Matiri
wilayani hapa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Festo Sangana ambaye
ndiye mmiliki wa nyumba ambayo lori hilo liliparamia na kubomoa sehemu kubwa ya
kuta za nyumba hiyo alisema kuwa, ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva
kutokana na kuwa katika mwendo kasi ambapo gari lilimshinda kukata kona ndipo
alisababisha ajali hiyo.
Sangana alifafanua kuwa baada ya dereva kusababisha tatizo
hilo alitokomea kusikojulikana ambapo marehemu Ndunguru, alifikwa na umauti
baada ya kukimbizwa hospitali ya misheni Litembo kutokana na kujeruhiwa vibaya
mwilini mwake.
Kadhalika majeruhi wengine waliokumbwa na mkasa huo kuwa ni Frank
Ndunguru (30), Shukran Sangana (26) na mtoto mmoja mdogo aliyetajwa kwa jina la
Sabina Komba mwenye umri wa mwaka mmoja, wote wakazi wa Myangayanga Tanga
pachani mjini hapa.
Mganga mfawidhi hospitali ya halmashauri ya mji wa Mbinga
Dkt. Robert Elisha alikiri kuwapokea majeruhi hao na kuongeza kuwa hali zao
zinaendelea vizuri na kwamba Anna Ndunguru, alipewa rufaa ya kupelekwa
hospitali ya Misheni Litembo kwa matibabu zaidi kutokana na kuwa na hali mbaya
ambako amepoteza maisha.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na Jeshi hilo linamshikilia dereva wa gari
hilo Erick Mbelle mkazi wa Tangi la maji Mbinga mjini, ambaye anadaiwa
kuendesha huku akiwa amelewa ndio maana alisababisha ajali hiyo na kwamba
wakati wowote atafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
“Huyu dereva baada ya kusababisha ajali hii alikimbia katika
eneo la tukio hakuweza kupatikana, baada ya siku chache kupita alijileta
mwenyewe kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga ndipo tulipomkamata na sasa
tunamshikilia ili tuweze kumfikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria”,
alisema Mwombeji.
No comments:
Post a Comment